Wanawake Posta wajipanga zaidi

Wanawake Posta wajipanga zaidi

Muktasari:

  • Wanawake wameadhimisha siku hii kwa kutoa ujumbe mbalimbali huku mikakati ikiwa ni kupeana ujuzi na kuinuana ili kufikia usawa.

Shirika la Posta Tanzania limesema kuwa wanawake ni chachu ya maendeleo ndani ya taasisi hiyo na kwamba, jitihada na umakini kwenye kazi umechangia ongezeko la mapato.


Kauli hiyo imekuja wakati wanawake duniani wakiendelea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambapo, uongozi wa shirika hilo umeahidi kuendelea kutoa kipaumbele kwa wanawake kwenye nafasi za uongozi.


Akizungumzia kuhusu Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa iliadhimishwa Machi 8, 2020, Afisa Mwandamizi wa shirika hilo, Aneth Mdamu ameliambia Mwananchi kuwa taasisi hiyo inatekeleza kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa vitendo.


Amesema shirika hilo litaendelea kutoa kipaumbele kwa wanawake wenye uwezo wa kuongoza nafasi za juu kwa kuwa, wengi wana uwezo katika kuleta mabadiliko chanja.


“Shirika la Posta kama ilivyo mengine limeendelea kutoa nafasi na kipaumbele kwa wanawake katika kushika nyadhifa za juu. Wanawake wameonyesha uwezo mkubwa katika ukuaji na mabadiliko ya shirika hivyo, litaendelea kuwa na usawa kwa wote kwenye kutoa ajira,” amesema Aneth.


Pia, ameongeza kuwa ndani ya shirika hilo, usawa kwa wote ni sera yao kubwa na hivyo imewafanya wanawake kuongoza vitengo mbalimbali huku wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi.


"Ukiangalia ndani ya taasisi yetu kuna ngazi kuu tatu za uongozi ambapo, nafasi moja imeshikiliwa na mwanamke nayo ni Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika, Bodi ya Wakurugenzi iliona haja ya kuwa mwanamke na hilo tunalipongeza sana," amesema na kuongeza:

Katika ngazi ya mikoa kuna wanawake wanaosimamia taasisi na wamekuwa chachu ya kukua kwa shirika na kuongezeka kwa mapato.”


Hata hivyo, kwa mujibu wa Aneth mpango uliopo kwa sasa ni kuhakikisha wanawake wanaendelea kuonyesha ujuzi ili kupata nafasi zaidi na kufikia malengo ya usawa wa 50/50.


Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka huu yalikuwa na kauli mbiu: Wanawake na uongozi chachu ya kufikia dunia yenye usawa.