Wanayopitia wasafirishaji, wananchi bei ya mafuta ikiuma
Muktasari:
- Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza ongezeko la bei za mafuta, linaloelezwa kuchochewa na mgogoro wa kimataifa unaoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Dar es Salaam. Ikiwa imeingia siku ya tatu tangu kutangazwa kupanda kwa bei ya mafuta, wadau wa usafirishaji waeleza athari wanazokumbana nazo na kutoa ushauri wa nini kifanyike ili kukabiliana na athari hizo kwa muda mfupi.
Aprili Mosi, 2026, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza ongezeko hilo la bei za mafuta, linaloelezwa kuchochewa na mgogoro wa kimataifa unaoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ulioanza Februari 28, 2026.
Tayari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo, ametangaza kuitisha kikao cha wadau wa usafirishaji Aprili 8, 2026 jijini Dar es Salaam, ambacho kitajadili suala hilo na kutoka na uamuzi.
Mgogoro huo umeathiri uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ghafi duniani, hasa baada ya kufungwa kwa Mlango wa Hormuz, ambao hupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani.
Vilevile, kushambuliwa kwa visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na viwanda vya kuyasafisha kumeigusa moja kwa moja Tanzania, ambayo inaagiza mafuta kwa kiasi kikubwa, jambo linalotajwa kuongeza gharama za usafirishaji kutokana na kukosekana kwa meli za kuyasafirisha.
Hali hiyo imesababisha ongezeko kubwa ambalo halijashuhudiwa kwa zaidi ya miaka 20, na kuilazimisha Serikali kukaza mikakati ya kupunguza athari hizo, kama alivyoeleza Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba.
Dk Mwigulu amebainisha mambo mawili wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo jana Alhamisi, Aprili 2, 2026, kwamba sasa Serikali itajielekeza katika kuongeza shughuli za uchimbaji madini na kubana matumizi.
Walichosema wasafirishaji
Baadhi ya wasafirishaji wamesema hali hiyo imeanza kuwauma. Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Usafiri wa Barabara, Shukuru Mlawa, amesema magari yameanza kupungua barabarani kutokana na matajiri na madereva kushindana hesabu.
“Hali ya mafuta inaonekana, lakini unakuta tajiri kakomaa na kutaka hesabu ileile unayotaka dereva achukue; gari hutaki liache. Hii kiukweli inawatesa madereva wengi, ukizingatia ndio kazi inayowaendesha maisha yao,” amesema Mlawa.
Katika hesabu hizo, wapo wanaotakiwa kupeleka Sh80,000 hadi Sh200,000 kwa siku. Hata hivyo, amesema siku mbili zijazo wanatarajia kukutana ili kutoa msimamo wao wa nini kifanyike ili kuwanusuru na hali hiyo.
Mkamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Rahim Dossa, amesema mzigo wa usafirishaji umekuwa ukiwaelemea, ukizingatia kuwa wanafanya biashara na nchi za jirani, ambapo mikataba yao iliingia kabla ya kutangazwa kwa mabadiliko ya bei hiyo ya mafuta.
Amesema kwa safari ya Zambia pekee, kutokana na ongezeko hilo la bei ya mafuta, gharama zimepanda kwa dola 750 katika safari moja, ikiwa ni zaidi ya Sh1.9 milioni.
Dossa anashauri kuwa ni vema, ikizingatiwa mabadiliko kama hayo, kuwapatia taarifa mwezi mmoja kabla, ili kuweza kuwaandaa na wateja wao. Vilevile, anasema mikataba iliyosainiwa kabla ya ongezeko la bei haiwezi kubadilishwa ghafla bila kueleweka na wateja.
“Pia, kwa taratibu zetu za ufanyaji biashara, kama kuna mabadiliko, unapaswa kumwambia mteja wako mwezi mmoja kabla. Kwa hali ilivyo sasa, mzigo huu wa gharama unaubeba wasafirishaji wenyewe,” amesema Makamu Mwenyekiti huyo.
Kutokana na hali hiyo, Dossa anaonyesha wasiwasi wake kwamba nchi zisije kukimbilia bandari za nchi jirani ili kukwepa gharama kubwa, na kushauri Serikali kuanza kutoa kodi mbalimbali zinazotozwa katika mafuta, ili kuleta ahueni ndani ya muda mfupi.
Mwenyekiti wa Chama cha Malori Tanzania (Chawamata), Nuhu Mgodole, ameshauri Serikali isiishie tu kutoa matamko na watendaji wake kukaa ofisini, bali itoke nje kuiona hali halisi, kwa kuwa mwisho wa siku muumiaji mkubwa ni mwananchi wa kawaida atakayebebeshwa gharama hizo.
Mgodole, ambaye yupo safarini akitokea Zambia kwenda Dar es Salaam, amesema hali mbaya imeanza kuonekana maeneo ya Tunduma, ambapo wapo madereva wameketi kwenye vituo vya mafuta wakisubiri huduma kutokana na uhitaji mkubwa.
Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo, amesema Arusha walipokuwa wakienda kununua mafuta ya Sh250,000, kutokana na mabadiliko hayo ya bei, sasa bila Sh500,000 hutoboi, fedha ambayo ni nyingi kwa mmiliki ikizingatiwa nauli bado ni ile ile huku gharama nyingine za uendeshaji zikisubiri pia.
Mwalongo amesema hatua ya haraka inayoweza kuchukuliwa kwa sasa ni kuondoa tozo, kwani mgogoro wa Iran na Marekani bado haijajulikana lini utaisha, na huenda hali ikawa mbaya zaidi siku za usoni.
Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Shakua), Hashim Omar, amesema kihalisia, mafuta yakipanda hali ya uchumi pia inapanda.
Hata hivyo, Latra ikikataza wamiliki wa daladala kupandisha nauli, huko mtaani tayari limeanza kufanyika, na mamlaka imeitakiwa kwenda mtaani kuchukua hatua ili iwe fundisho kwa wengine.
Kuhusu bajaji na bodaboda kupandisha bei zaidi ya mara mbili, Omar amesema asingependa kuongelea, kwa kuwa usafiri huo upo kwa ajili ya kukodiwa na siyo kama daladala; hivyo ni uamuzi wa abiria kupanda au kuacha.
Mmoja wa abiria, aliyejitambulisha kwa jina la Husna, amesema usafiri wa bodaboda na bajaji umekuwa mkombozi kwa wananchi wengi, ukirahisisha gharama kutoka eneo moja kwenda jingine na kuondoa usumbufu wa kukaa muda mrefu barabarani.
Abdallah Juma, mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, amesema gharama za bajaji kutoka Mbezi hadi Mwenge zimepanda, ambapo awali ilikuwa Sh2,000, sasa imefikia kati ya Sh2,500 hadi Sh3,000 kwa kila mmoja.
Sakina Hegga anasema awali alikuwa akipanda bajaji kutoka Kinyerezi hadi Mbezi kwa Sh1,000, sasa imefikia Sh1,500, na kutoka Malamba hadi Mbezi ilikuwa Sh500, sasa imefikia Sh1,000. Kuongeza nauli hizi huongeza nyakati za safari asubuhi au jioni.
Joel Meshack, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Nyama Machinjio ya Vingunguti, amesema ongezeko la bei ya mafuta limewaathiri, kwani gharama za usafirishaji wa mifugo na nyama zimeongezeka pia.
Meshack ametolea mfano gari walilokuwa wakikodi kusafirisha mifugo kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam: walilipa Sh1 milioni, sasa gharama imeongezeka hadi kufikia Sh1.3–1.5 milioni.
“Kama hali itaendelea kuwa hivi, pengine bei ya nyama inaweza kuongezeka; kwa sasa inauzwa kati ya Sh11,000 hadi 12,000 kwa kilo,” amesema Meshack.