Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu kutoka Finland kuwanoa Watanzania ubunifu kwenye Tehama

Mkurugenzi Mkuu ICTC, Dk Nkundwe Mwasaga akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Juni 22,,2026 jijini Dar es Salaam kuhusu mafunzo ya ubunifu katika Tehama yanayofundishwa na wataalamu kutoka Finland.

Muktasari:

  • Mafunzo hayo yanayotolewa na wataalamu kutoka nchini Finland kupitia Tume ya Tehama Tanzania (ICTC), yatajikita katika bunifu za Tehama ili kuongeza na kupanua wigo wa ushindani wa Watanzania katika soko la kimataifa, ajira na mchango katika uchumi wa kidijitali.

Dar es Salaam. Mafunzo ya ubunifu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) yatakayotolewa kwa siku tano kwa Watanzania wapatao 50 yametajwa kuwa na tija katika kutoa ajira na kuongeza mchango katika uchumi wa kidijitali.

Mafunzo hayo yanayotolewa na wataalamu kutoka nchini Finland kupitia uratibu wa Tume ya Tehama Tanzania (ICTC), yatajikita katika bunifu za Tehama ili kuongeza na kupanua wigo wa ushindani wa Watanzania katika soko la kimataifa.

Akizungumza baada ya kufungua mafunzo hayo jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Juni 22, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga amesema katika siku hizo tano washiriki watajifunza namna ya kufanya ubunifu ili uwe na tija.

Aidha, amesema mafunzo hayo yamelenga kushirikiana na nchi zinazofanya vizuri kwenye eneo hilo la ubunifu ikiwemo Finland kupitia mradi wa Serikali wa Digital for Tanzania unaotekelezwa na Germany, Finland na Estonia.

Washiriki wa mafunzo ya ubunifu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) yanayosimamiwa na Tume ya Tehama na Mawasiliano (ICTC), yakiendeshwa na wataalamu kutoka Finland, wakifuatilia mafunzo hayo yenye lengo la kuimarisha ubunifu na ujuzi wa kidijitali nchini.

"Upande wa Serikali tunaangalia hizo bunifu zinaweza kutengeneza ajira kiasi gani kwa vijana wengi, na mchango wake kisekta, na kuifanya nchi kuwa shindani," amesema.

Amesema zipo nguzo tano za mafunzo ya kidijitali ambazo ni usalama wa mtandao, ujuzi, mifumo ya mawasiliano kuweza kubeba kazi za sasa kama akili unde, uchumi wa kidijitali na utafiti na ubunifu.

"Mafunzo haya yanahusu ubunifu na Tanzania tuna vijana wengi tunataka wasiwe tu watumiaji bali wabunifu na wenye uwezo wa kutengeneza mifumo. Kwa hiyo tunawapa ujuzi wajifunze namna ya kuleta tija kupitia ubunifu," amesisitiza.

Kwa mujibu wake, uchumi wa kidijitali unabebwa na ubunifu ndiyo maana mafunzo hayo ya kwanza yamekuwa njia ya kuelekea mafunzo mengi zaidi.

"Vijana wakishajua nini kinafanywa Finland watajua tija yake. Mfano katika mafunzo haya watajifunza namna ya ununuzi wa ubunifu wa vijana ambao ni jambo jipya," amefafanua.

Amesema yanatengenezwa mazingira ya kuatamia bunifu za vijana ili waweze kushindana katika soko la Afrika Mashariki, Afrika nzima na duniani kote.

Akizungumza Tiina Koivuniemi kutoka Finland, amesema faida kubwa ya mpango huo ni kuwafundisha washiriki mbinu za kivitendo za jinsi ya kusimamia ubunifu pamoja na kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kazi itakayosaidia kuwepo kwa ushirikiano wa karibu katika miradi mbalimbali ya maendeleo hapo baadaye.

"Vijana na wabunifu nchini Tanzania wazidi kuwa wajasiri, kutogopa kufanya majaribio ya mawazo mapya, na kujifunza kuangalia changamoto za kijamii katika mitazamo tofauti," amesema Tiina.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Peace Bisake, mwanzilishi wa ReinoLab AI Powered Digital Science Lab, amesema mafunzo hayo yatawafanya washindane na wabunifu wa kimataifa.

Naye, Rodrick Mshanga, mwanzilishi wa Paki Urban Limited amesema wabunifu wengi hawana elimu ya kukuza biashara na mawazo yao kuwa makubwa ya kiushindani hivyo mafunzo kama hayo yana tija kwa kiwango kikubwa.

Jani Ruuskanen, Mshauri Mkazi wa Mradi Pacha wa Kidijitali (D4T), amesema mradi huo unafanya kazi katika maeneo mahususi ya usalama wa mitandao (Cyber security), ulinzi wa taarifa binafsi, utangamano wa mifumo (interoperability), na msaada wa jumla wa mabadiliko ya kidijitali kwa Tanzania.

"Lazima niseme kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa katika miaka michache iliyopita ambayo tumekuwa tukifanya kazi hapa katika kujenga uchumi wa kidijitali. Na hasa wiki hii, tunapoandaa mafunzo ya ubunifu yanayolenga kampuni changa (startups), ili kusaidia kufikia lengo kubwa la Dira ya 2050. Hivyo, ninafurahia na kujisikia mwenye heshima kuwa hapa kwa mara ya kwanza kuwekeza kwenye programu kama hii nchini Tanzania, na hata Afrika kwa ujumla," amesema.