Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watuhumiwa 117 wakamatwa Songwe katika operesheni ya Mei

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga.

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limekamata watuhumiwa 117 kwa makosa mbalimbali katika operesheni za mwezi mmoja.

Songwe. Watu 117 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali mkoani Songwe katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita huku Jeshi la Polisi likisema operesheni na msako unaoendelea umechangia kupungua kwa vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Taarifa kwa umma iliyotolewa Juni 4, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga kuhusu hali ya usalama mkoani humo, imeeleza watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni tofauti zilizofanyika kuanzia Mei Mosi, 2026 hadi sasa.

Senga amesema miongoni mwa waliokamatwa ni watu wanane waliokutwa wakijihusisha na biashara ya vipodozi vilivyoingizwa nchini kinyume cha sheria na vile vilivyopigwa marufuku.

“Mei 27, 2026 tuliwakamata watuhumiwa wanne wakiwa na gari aina ya Fuso likiwa limebeba boksi 1,892 za vipodozi vilivyoingizwa nchini bila kufuata taratibu za forodha. Watuhumiwa hao tayari wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,” amesema Senga kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma.

Katika tukio jingine lililotokea Juni 4, 2026, eneo la Mzani Mpemba, Tunduma wilayani Momba, Kamanda Senga amesema  watuhumiwa wengine wanne walikamatwa wakisafirisha boksi 70 na vipande 117 vya vipodozi vilivyopigwa marufuku nchini.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, watuhumiwa hao walikuwa wakisafirisha bidhaa hizo kutoka nchi jirani kuelekea Dar es Salaam kwa kutumia lori aina ya Howo mali ya kampuni ya Specialized Hauliers (T) Ltd.

Katika operesheni za kudhibiti dawa za kulevya, Senga amesema jumla ya watu 49 walikamatwa wakiwa na bangi yenye uzito wa kilo 20.876 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Songwe.

“Watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani na kuhukumiwa vifungo vya kuanzia miezi sita hadi miaka miwili kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi pia limepata mafanikio katika mashauri yaliyokuwa mahakamani ambapo watuhumiwa 67 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali vya jela.

Akitolea mfano baadhi ya kesi hizo, Senga amesema Mahakama ya Wilaya ya Songwe Mei 14, 2026 ilimhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Salvatory Rogers (29), mkazi wa Galula, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la ubakaji.

Katika kesi nyingine, Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, Aprili 2, 2026 iliwahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Shukran Juma (32), Maiko Charles (26) na Fredy Enison (29) baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kucheza kamari.

Mbali na operesheni za kiusalama, Senga amesema Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza dhana ya Polisi Jamii kupitia mikutano 713 iliyofanywa na polisi kata katika wilaya za Mbozi, Ileje, Momba na Songwe.

Amesema kupitia mikutano hiyo, vikundi zaidi ya 11 vya ulinzi shirikishi vimeundwa na kupewa elimu ya namna ya kushiriki katika kuimarisha usalama wa maeneo yao.

Wakati huohuo, Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe kimekamata vyombo vya moto 141 vilivyowekwa vimulimuli na taa za nyongeza zinazotumiwa na magari yenye kipaumbele kinyume cha sheria.

Senga amesema magari 51 pamoja na pikipiki na bajaji zilihusika katika makosa hayo, huku vyombo vyote vikitozwa faini na vifaa hivyo kuondolewa.

Pia, amesema kikosi hicho kimekamata jumla ya makosa 6,786 ya usalama barabarani na kuwafungia leseni madereva wawili kwa miezi mitatu baada ya kubainika kuendesha magari wakiwa wamelewa.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kutoa wito kwa wananchi kuachana na vitendo vya uhalifu na kujihusisha na shughuli halali za kiuchumi.

“Tutachukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na biashara haramu, dawa za kulevya, ukwepaji kodi na vitendo vingine vinavyokiuka sheria za nchi,” amesema Senga.

Amesisitiza hakuna mtu atakayekuwa juu ya sheria na kwamba mkono wa sheria utamfikia yeyote atakayekiuka sheria bila kujali hadhi au nafasi yake katika jamii.