Wavuvi wa dagaa walia kunyonywa

Wavuvi wa dagaa walia kunyonywa

Muktasari:

  • Wavuvi wa dagaa aina ya uono wamelalamikia bei ndogo wanayolipwa na wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hivyo kuiomba Serikali kuingilia kati.

Pangani. Wavuvi wa dagaa aina ya uono wamelalamikia bei ndogo wanayolipwa na wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hivyo kuiomba Serikali kuingilia kati.

Wavuvi hao wa Bahari ya Hindi kutoka maeneo ya pwani ya Pangani Mashariki, Kigombe, Kipumbwi Mkwaja na Mangapwani Zanzibar wamesema huuza dagaa kwa Wakongo kutokana na kukosa soko nchini.

Wakongo wanaelezwa kutoa fedha mapema kila unapofika msimu wa uvuvi wa uono kwa wenye vyombo vya uvuvi ili kuumiliki mzigo wote utakapovuliwa.

“Wanakuja kuwekeza kwa bei ya kati ya Sh3,500 hadi Sh4,000 kwa kipimo cha ndoo ya samli. Kwa hiyo anaweza kuniachia hata Sh3 milioni ukifika msimu wa uvuvi wanaweza kutupandishia bei wakatuuzia Sh4,500 au Sh4,700 sasa akija kuchukua hawezi kukubali bei hiyo,” alisema Mwanaidi Akida.

Mwanaidi alidai kama wananunuzi wa Pangani wangekuwa na mitaji ya kutosha, wangeweza kuwauzia raia hao wa Congo kwa bei ya faida kwa sababu ya gharama za uendeshaji kuwa kubwa hasa za kupakia dagaa kwenye malori. “Gharama tunazoingia hadi kupakia uono kwenye maroli ya kupeleka Congo ni kubwa,” alisema.

Waziri wa Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema wizara ipo katika mkakati wa kuleta mapinduzi ya kiuchumi katika sekta ya uvuvi kwa kununua zana za kisasa za zitakazowawezesha wavuvi kufanya uvuvi wenye tija.