Agundua namna mianzi inavyoweza kutumika badala mbao za magogo

Wasomi kadhaa wamekuwa wakifanya tafiti kuangalia mbadala ya miti, kwa mfano Dk Mathias Lugoye, Mkufunzi wa chuo cha Uhandisi na Teknolojia Kampasi ya Mwalimu Nyerere ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema ‘’Tafiti zinaonyesha mianzi ikitumiwa vizuri inaweza ikawa mbadala wa mbao katika matumizi mbali mbali hivyo kuondoa hatari ya ukataji miti ovyo.’’Picha na Mpigapicha wetu

Muktasari:

Kama ambavyo sasa kumekuwa na jitihada za kusaka mbadala wa umeme uliozoeleka wa maji, kwa kuhangaikia upatikanaji wa gesi na hata umeme wa jua, iko haja ya kuangalia mbadala wa matumizi ya miti ili kuepusha uharibifu wa mazingira.

Dar es Salaam.Wakati taifa linaendelea kujipanga ili kuwa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ni wazi njia mbadala za kuendesha mambo zinapaswa kuzingatiwa.

Kama ambavyo sasa kumekuwa na jitihada za kusaka mbadala wa umeme uliozoeleka wa maji, kwa kuhangaikia upatikanaji wa gesi na hata umeme wa jua, iko haja ya kuangalia mbadala wa matumizi ya miti ili kuepusha uharibifu wa mazingira.

Ni uharibifu uliokithiri wa mazingira ndiyo unaosababisha hata upatikanaji wa mvua katika baadhi ya maeneo nchini kuwa wa shida, hiki ni kiashiria kuwa kutokuwepo kwa njia mbadala ya miti, hali ya mazingira huenda ikawa mbaya katika siku za baadaye.

Msomi aibuka na utafiti

Wasomi kadhaa wamekuwa wakifanya tafiti kuangalia mbadala ya miti, kwa mfano Dk Mathias Lugoye, Mkufunzi wa chuo cha Uhandisi na Teknolojia Kampasi ya Mwalimu Nyerere ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema ‘’Tafiti zinaonyesha mianzi ikitumiwa vizuri inaweza ikawa mbadala wa mbao katika matumizi mbali mbali hivyo kuondoa hatari ya ukataji miti ovyo.’’

Dk. Lugoye amefanya utafiti katika mmea wa mwanzi na kubaini kuwa unaweza kutumika katika matumizi mbadala ya mbao katika kutengeneza dari, sakafu na kuta za mbao.

Anasema mmea wa mwanzi ni mwepesi na wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza kitu chochote.

Mwanzi unaweza kutumika kutengeza paneli za mbao kwa kuunganisha hata kwa kutumia utomvu saini au utomvu asilia kama vile majimaji ya gamba la mbegu ya korosho.

Anasema uzuri wa mmea huo ni kwamba unakua haraka zaidi kuliko jamii ya mti wowote uliopo katika sura ya Dunia. Anasema mmea wa mwanzi huwa unaongezeka urefu kati ya cm 15-18 kwa siku ukiwa mchanga.

Mwanzi ni jamii ya mti, vile vile ni jamii ya nyasi kwa jinsi ya maumbile yake yalivyo.

‘’Ingawa mwanzi ni mwepesi na unakua haraka lakini ni imara kama ilivyo miti mingine inayotumika katika mazao ya mbao, hivyo ndiyo maana nimegundua inaweza kutumika katika kutengenezea vitu mbali mbali,’’ anasema Dk. Lugoye.

Matokeo ya utafiti

Akizungumzia utafiti wake ambao ulichukua miaka isiyopungua sita, Dk Lugoye anasema katika utafiti alioufanya amewezakugundua kuwa mmea wa mwanzi unaweza kuwa mbadala wa mbao katika matumizi mbalimbali kama kujengea sakafu, kuta zitokanazo na mbao pamoja na kutengeneza fanicha kama vitanda, shelfu za vitabu na hata kujengea nyumba.

Anasema duniani kuna aina au spishi nyingi za mianzi, lakini kwa Tanzania alikutana na takribani aina nne kuu ambazo ni mianzi yenye pingili ndefu inayopatikana ukanda wa nyanda za juu za Iringa, Ruvuma, Ulanga Morogoro na Mbeya (Arundinaria Alpina).

Aina nyingine ni mianzi ya yenye rangi za njano na kijani (bambusa vulgaris) ambayo imetapakaa karibu nchi nzima kwa ajili ya utafiti ilitumika mianzi kutoka Kilosa na Kijitonyama.

Mianzi ya kijani yenye pingili fupi (oreobambus buchwaldii) inayopatikana ukanda wa Pwani, Lindi na Morogoro na aina ya mwisho ni mianzi inayotoa ulanzi (oxytenanthera braunii) ambayo inapatikana kwa wingi katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Ruvuma.

Katika utafiti wake alitumia zaidi mianzi kutoka Mbeya yenye pingili ndefu ijulikanayo kwa jina la kisayansi kama arundinaria alpina. Dk. Lugoye anasema alitumia aina hiyo ya mianzi katika tafiti zake ambapo aliweza kutengeneza paneli ambazo zinatokana na miazi kwa kuziunganisha na utomvu sanisi au utomvu asili kama vile asidi ya gamba la fito na mti na maji maji ya gamba la kokwa la korosho.

Matokeo ya utafiti wake

Katika matokeo ya Utafiti huo anasema yanaridhisha kwa kuwa waliweza kugundua kuwa mianzi inaweza kutumika kwa kuwa mbadala wa mbao, hasa katika ujenzi sakafu, kuta na dari.

‘’Karibu mbao zote zilizo achwa wazi kwa muda kwa lengo la kuangalia uimara wake zilionyesha matokeo mazuri kwamba zinaweza kuhimili,’’ anasema Dk Lugoye.

Msomi huyo anafafanua kuwa tafiti zikikumika vizuri, Serikali na jamii kwa ujumla wake zinaweza kuwa na maendeleo katika nyanja mbalimbali hata kupunguza umasikini kwa wananchi.

Kwa kuwa utafiti umesha onyesha mbao za mwazi zinaweza kutumika badala ya mbao za miti na zikawa imara, anashauri Serikali itumie utafiti huo na kuweza kuwafanya vijana kujiari na kuongeza pato la nchi kwa kutengeza vitu vinavyotokana na mbao za mianzi.

Pia akatoa wito kwa Serikali na Tume ya Sayansi na Technolojia iweze kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya watu kufanya tafiti mbali mbali pia kuwepo na bajeti ya kuzifanya tafiti hizo ziweze kufanya kazi katika jamii yetu.

Anafafanua kuwa hata katika baadhi ya nchi zilizoendelea, siyo kila nyumba inatumia udongo, bali zingine zimejengwa kwa miti maalumu au blastiki maalumu nzito.

Dk Lugoye anashauri Watanzania kuangalia namna ya kutumia teknolojia hiyo ambayo kwa mujibu wa utafiti wake itasaidia sana kupunguza matumizi ya mbao kama watu wataizingatia.