Babu wa Samunge:JPM awahakikishie wananchi huduma bora za afya

Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwasapila maarufu kama ‘Babu wa Samunge’ anatuma ujumbe mahsusi kwa Rais kuhusu sekta ya afya.

Muktasari:

Katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Samunge wilayani Ngorongoro, Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwasapila maarufu kama ‘Babu wa Samunge’ anatuma ujumbe mahsusi kwa Rais kuhusu sekta ya afya.

Tangu aingie madarakani Novemba5, Rais John Magufuli ameonyesha dhamira ya kufanya mabadiliko katika mfumo wa uongozi na utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo sekta ya afya inayokabiliwa na changamoto kadhaa.

Katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Samunge wilayani Ngorongoro, Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwasapila maarufu kama ‘Babu wa Samunge’ anatuma ujumbe mahsusi kwa Rais kuhusu sekta ya afya.

“Rais Magufuli na Serikali yake mpya ya Awamu ya Tano lazima waboreshe huduma za kiafya. Wananchi wapatiwe uhakika wa tiba bora na nafuu katika maeneo yao,” anasema.

Anasema kwa kipindi kirefu, afya ni kati ya sekta zenye changamoto nyingi nchini kutokana na ufinyu wa bajeti kulinganisha na mahitaji, uhaba wa wataalamu na wakati mwingine kukosekana kwa utashi miongoni mwa wenye dhamana.

Mchungaji Mwasapila anasema ushahidi wa changamoto na uhitaji wa huduma za kiafya miongoni mwa Watanzania unadhihirishwa na idadi kubwa ya waliojitokeza kunywa kikombe alipoanza kutoa huduma mwaka 2010.

Watu kwa maefu, viongozi serikalini, wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa

kwa wadogo na wananchi wa kawaida walimiminika Samunge kunywa ‘kikombe cha Babu wa Loliondo’ kilichoaminika kutibu maradhi sugu ikiwamo kisukari, shinikizo la moyo na saratani.

Rais John Magufuli (wakati huo akiwa waziri), ni kati ya viongozi waliokunywa kikombe hicho.

“Sijui kilichokuwa kikimsumbua (Rais Magufuli), lakini nina imani alipona kama watu wengine walivyopona,” anasema Mchungaji Mwasapila akimzungumzia Dk Magufuli kuwa miongoni mwa wateja wake.

“Ujumbe maalumu ninaoweza kumtumia Rais ni mmoja tu. Aboreshe huduma za afya ili kuwaepusha wananchi na adha ya kukimbilia kwa matabibu wadanganyifu kama tunavyoshuhudia sasa kila mtu akijitangaza kuponya magonjwa sugu,” anaongeza.

Mchungaji Mwasapila anasema wingi wa vibao vya matabibu wa magonjwa sugu kila kona mitaani kuanzia vijijini hadi mijini ni ushahidi wa wananchi kukabiliwa na changamoto ya kiafya na mahitaji ya huduma za afya.

Elimu ya maradhi yasiyoambukiza

“Mafundisho ya Biblia yanazungumzia watu kuangamia kwa kukosa maarifa. Watanzania wengi wanaangamia kwa kukosa maarifa kuhusu maradhi yanayowakabili. Ni jukumu la Serikali kutoa elimu hiyo,” anasema.

Anapendekeza kuwapo kwa idara maalumu ya elimu kwa umma katika kila zahanati, kituo cha afya na hospitali za wilaya, mikoa na rufaa kuwezesha wagonjwa wanaofika kwa matibabu kuelimishwa njia sahihi ya kuepuka na kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza.

“Watu wafundishwe kuwa na nidhamu ya vyakula ili kuepuka maradhi yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na saratani,” anashauri mchungaji huyo.

Maandalizi ya muujiza mwingine

“Mwenyezi Mungu amenipa maono ya kutokea muujiza mwingine mkubwa utakaovutia umati wa watu kuliko ule uliofika Samunge kunywa kikombe,” anasema Mchungaji Mwasapila akizungumzia huduma yake.

Anasema kutokana na ujumbe huo na maelekezo ya Mungu, tayari ameanza maandalizi kwa kujenga kituo maalumu cha tiba eneo la Makao, umbali wa kilomita mbili kutoka alipotoa huduma awali.

“Tayari tumekamilisha ujenzi wa nyumba ya kuhifadhi na kutoa dawa, nyumba za watumishi, askari na waandishi wa habari kutoka ndani na nje ya nchi watakaofika kuripoti tukio hilo kubwa.

“Tumeshapima na kujenga misingi ya nyumba nyingine tisa ikiwamo jengo la utawala na la watu maarufu (VIP) kwa ajili ya viongozi watakaofika kunywa dawa,” anasema.

Tayari Mchungaji Mwasapila amenunua magari matatu aina ya Isuzu (tani saba), Fuso na Land Cruiser kwa ajili ya kuboresha huduma ya tiba itakayoanza karibuni.

Ingawa Mungu hajamdhihirishia ni lini ataanza kutoa huduma hiyo mpya, anasema: “Haitachelewa kama ile ya mwanzo ambayo nilipokea maono mwaka 1991, lakini nikaanza huduma miaka 19 baadaye (mwaka 2009). Hii itawahi kwa sababu napata msukumo mkubwa kutoka kwa Mungu niharakishe ujenzi wa kituo.”

Akizungumza baada ya ziara fupi kuzunguka makazi yake na eneo la kituo kipya cha tiba anachokijenga, Mchungaji Mwasapila aliyefika Loliondo kwa mara ya kwanza miaka ya 1980 akiwa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), anasema huduma mpya pia itahitaji wasaidizi wengi kuliko 50 aliokuwa nao wakati wa huduma ya kwanza.

“Wakati ule nilikuwa na wasaidizi 50 ambao nilisaidiana nao kuhudumia watu zaidi ya 18,000 waliofika kunywa kikombe kila siku. Huduma mpya itahitaji wasaidi hata zaidi ya 100 kwa sababu kazi itakuwa kubwa zaidi,”anasema.

Kuhusu madai ya uganga na utapeli anasema: “Siwezi kuwazuia wanaopenda kuisemea vibaya huduma yangu kwa sababu hiyo ndiyo hulka ya binadamu. Ila Mungu wangu ninayemwabudu na kumtumikia na aliyenipa maono haya ndiye mwamuzi wa haki.”

Anataja kitabu cha Biblia cha Ezekiel sura ya 47:12 kuwa ndiyo misingi ya huduma yake na kuwataka wenye kuisemea vibaya huduma yake ya uponyaji kutambua kuwa Mungu ana njia nyingi za kusaidia wa mwaminio ikiwamo miujiza isiyoeleweka kirahisi kwa akili za kibinadamu.

Samunge ya sasa

“Huduma nyingi za kijamii zimeboreka. Serikali imetujengea mindombinu ya barabara ya uhakika. Tumepata huduma ya majisafi na salama, kampuni za simu zimeleta minara kurahisisha mawasiliano na Samunge (Loliondo), sasa inajulikana duniani kote kutokana na kikombe cha Babu,” anasema.

Anaeleza kwamba kabla ya kuanza kutolewa kwa huduma ya kikombe, eneo hilo pia halikuwa na huduma ya umeme tofauti na sasa ambako wanafaidi umeme wa jua unaoendelea kusambazwa kijijini hapo.

Ombi maalumu kwa Serikali

Akizungumzia uwingi wa watu wanaotarajiwa kumiminika Samunge kupata huduma mpya anayotarajia kutoa, Mchungaji Mwasapila anaiomba Serikali kuanza maandalizi kwa kuboresha na kuimarisha barabara kwenda Kijiji cha Samunge kuepusha jamii na adha ya kukwama njiani kutokana na ubovu wa barabara kama ilivyoshuhudiwa kipindi kilichopita.

Viongozi na mti wa dawa

“Viongozi kadhaa akiwamo Rais mstaafu Jakaya Kikwete waliomba na nikawapatia miche ya mti ninaotumia mizizi yake kutengeneza dawa,” anadai.

Kuhusu iwapo Rais huyo mstaafu ni kati ya waliokunywa kikombe, Mchungaji Mwasapila anasema, “Siwezi kukanusha wala kuthibitisha maana watu wengi wakiwamo viongozi walifika hapa nyakati za usiku kunywa dawa. Sikuchunguza utambulisho wao,”

“Naweza kuthibitisha kuwa Kikwete aliomba na nikampatia miche mitatu ya mti wa Mngamriaga (Kisonjo), au Ngamriaki (Kimasai), ambayo wasaidizi wake waliofika kuichukua wamenihakikishia imestawi shambani kwake huko Msoga.

“Rais Magufuli akihitaji miche ya mti huu wa tiba, nitampatia bila hiana kama nilivyofanya kwa mtangulizi wake.”

Anasema licha ya kutumia mizizi ya mti huo kutoa tiba kulingana na maono, mti huo pia hutumiwa na makabila mbalimbali nchini kwa shughuli mbalimbali ikiwamo tiba.

“Kinachotofautisha tiba ninayoitoa na nyingine ya makabila mengine ni kwamba mimi nimepata maono hayo Kibiblia na tiba yangu ni ya kiimani. Lakini ushuhuda wa wengi ni kwamba mti huo una uwezo wa kutibu na hutumiwa na makabila mengi nchini,” anasema.

“Jamii ya Samunge pia ianze maandalizi kwa wenye uwezo kujenga nyumba za kulala wageni, migahawa na kununua vyombo vya usafiri ili waweze kushiriki neema ya kibiashara itakayoandamana na huduma mpya ya tiba,” anashauri

Jirani anamzungumziaje?

“Kwetu sisi, Mchungaji Mwasapila ni zaidi ya Babu wa Loliondo kama wengine wanavyomfahamu. Huyu ni mkombozi kwa jamii yetu kwa sababu huduma yake imeibua kijiji chetu kutoka kwenye vumbi hadi kileleni,” anasema Josephine Joseph, jirani wa Mchungaji Mwasapila

Akizungumza baada ya kukutwa akikata kuni karibu na kituo kipya cha tiba kinachojengwa na Mchungaji Mwasapila, jirani huo anasema tiba ya Babu wa Loliondo imenufaisha wengi kijijini hapo baada ya kupona maradhi sugu yaliyokuwa yakiwasumbua ikiwamo ugumba.

“Waliokosa watoto kwa kipindi kirefu kiasi cha kukata tamaa sasa wanalea. Baadhi wana watoto wawili hadi watatu baada ya kunywa kikombe cha Mchungaji (Mwasapila),” anasema Josephine

Mchungaji Mwasapila ni mzaliwa wa Rungwe mkoani Mbeya, ingawa hakuwahi kuishi miaka mingi sehemu hiyo.