Eid el Adh-ha: Ni kumbukumbu ya mtihani aliopewa Nabii Ibrahim (A.S)

Muktasari:

  • Nguzo ya kwanza ni shahada ambayo Muislamu anapaswa atoe shahada kwa kusema kwamba nakiri kuwa hakuna Mungu isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni mjumbe wa Allah.

Leo ni sikukuu ya kuchinja. Ni sikukuu ambayo huadhimishwa baada ya Waislamu kukamilisha ibada ya Hijja ambayo ni nguzo ya tano katika nguzo za Uislamu.

Nguzo ya kwanza ni shahada ambayo Muislamu anapaswa atoe shahada kwa kusema kwamba nakiri kuwa hakuna Mungu isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni mjumbe wa Allah.

Nguzo ya pili ni kuswali swala tano ambazo zimewekewa nyakati maalumu alfajiri, adhuhuri, alasiri, magharibi na ishai (usiku).

Kwa imani ya Uislamu Mtume Muhammad (S.A.W) alipewa amri ya umati wake kuswali wakati alipokwenda Miiraj (safari ya muujiza aliyokwenda Mtume S.A.W kutoka Makka kwenda Baitil Maqdis iliyopo Palestine).

“Ametakasika, aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka msikiti wa mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumwonyeshe baadhi ya ishara zetu...” (Al-Israa 17: 1).

Mwanzo wa amri ilikuwa ni kuswali swala 50 lakini kutokana na hekima za Nabii Mussa (A.S) aliyemshauri Mtume Muhammad kurudi kwa Mola wake kuomba apunguziwe idadi hiyo ya swala kwa sababu wafuasi wake hawataziweza, mwisho zilipunguzwa hadi zikawa tano lakini zenye thawabu ya Swala 50.

Mtume (S.A.W) alisema: “Allah alinipa ufunuo na akasema kuwa ummah wangu wanawajibika kuswali swalah 50 kila siku; usiku na mchana. Nilishuka kwenda kwenye Mbingu ya Mussa (A.S) akaniluza, “Lipi Mola wako amekupatia kwa ajili ya umati wako? Nikasema, “Swala hamsini.” Akasema rejea kwa Mola wako na omba akupunguzie idadi hiyo ya Swalah, maana watu wako hawawezi kubeba mzigo huo mzito.”

Kisha Mtume (S.A.W) akasema, “Nilirejea kwa Mola wangu na kusema, “Ewe Mola wangu, Fanya vitu viwe vyepesi kwa ajili ya Ummah wangu. Allah alipunguza idadi ya Swalah 50 na kuwa tano... [Al-Bukhaariy Juzuu 9 Namba 608].

Kufunga mwezi wa Ramadhan ni nguzo ya tatu katika nguzo tano za Uislamu nayo ilikuja kwa amri iliyoainishwa wazi na Qur’an tukufu: “Enyi mlioamini, mmefaradhishiwa Swaumu kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu (Al Baqara:183).

Nguzo ya nne ya Uislamu ni kutoa Zakka. Hii ni sadaka ya fardhi aliyofaridhishiwa Mtume S.A.W juu ya Waislamu na ni takaso la roho, mali na kiwiliwili.

Zakka imetajwa pamoja na Swala ndani ya Qur’ani Tukufu na hilo laonyesha jinsi amri hii ilivyo muhimu. Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume Muhammad S.A.W kuchukua sadaka kwa Waislamu. Akasema “Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe kwayo na kuwatakasa na uwaombee….” (9:103).

Ibada ya Hijja

Hijja ni nguzo ya tano ya Uislamu na imekuja kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“… Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewawajibikia watu wahiji kwenye nyumba ile (baitil Atiq) kwa yule awezaye njia ya kwendea (mwenye uwezo wa kifedha na kiafya)… Al-Imran 97.

Sikukuu inayoadhimishwa leo duniani kote inatokana na kukamilika kwa ibada ya Hijja ambayo hufanyika mfungo tatu (Dhul Hijja) kila mwaka.

“Na timizeni Hajj na Umra kwa ajili ya Allah.” Al Baqarah 196.

Siku ya kuchinja

Sikukuu ya kuchinja (Eid el Adh-ha), au wengine huiita Idd kubwa. Ni mojawapo kati ya sikukuu mbili kubwa kwa Waislamu. Moja ikiwa ni sikukuu ya kutoa Zakka – Eid el Fitr baada ya kumaliza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na ya pili ni hii ya kutoa kafara ya mnyama (kuchinja) baada ya kukamilisha ibada ya Hijja.

Sababu kubwa ya kuchinja ni kukumbuka majaribio aliyopewa Nabii Ibrahimu (AS) na Mola wake. Ibrahim alioteshwa amchinje mwanawe Ismail ambaye alimpata baada ya miaka mingi akiwa ameshakuwa mzee na baada ya kukata tamaa kabisa.

Wakati tayari ameshamwekea kisu shingoni Ismail, akabadilishiwa na kuwekewa mnyama aliyetoka mbinguni, hivyo badala ya kumchinja mwanawe, nabii Ibrahim akamchinja mnyama.

Katika sikukuu hii, Waislamu huadhimisha kwa kuchinja wanyama kama vile ngamia kondoo au mbuzi. Nyama inayochinjwa kama sadaka ya siku ya Eid el-Adh-ha zaidi hutolewa kwa watu wengine. Moja ya tatu huliwa na familia na jamaa wa karibu, moja ya tatu hutolewa kwa marafiki na moja ya tatu hutolewa msaada kwa maskini.

Ni muhimu kuelewa kwamba sadaka yenyewe, kama inavyofanywa na Waislamu, haihusiani kwa lolote na dhana ya kuondolewa dhambi wala kwamba kuzisafisha nafsi zao kutokana na dhambi: ﴾“... Si nyama zao au damu zao zimfikiazo Mwenyezi Mungu, bali ni uchamungu wao ufikao kwake﴿ (Quran 22:37).

Yanayojuzu kufanywa siku ya sikukuu

Uislam unahimiza kuamrishana mema na kukatazana maovu. Katika Uislamu siku ya sikukuu ni siku ya kumshukuru Mungu Muumba kwa neema alizowapa waja wake. Anayediriki kuipata sikukuu anapaswa ashukuru kwa kufanya ibada kama vile kuswali, kutembelea wagonjwa, kutembelea wazee (ndugu, jamaa na marafiki), kuvaa nguo nzuri, kula chakula kizuri na kutoa sadaka na zakka.

Sikukuu zote mbili kuu katika Uislam (Eid es Fitr – sikukuu ya kumaliza mfungo na Eid el Adh-ha – sikukuu ya kumaliza ibada ya hijja) zimeambatana na kutoa zakka. Eid el Fitr Waislam wanapaswa watoe zakka ya chakula (Zakatul Fitr) na kwamba bila ya kutoa zakka hiyo funga zao huwa zimening’inizwa (hazipokelewi).

Wakati wa Eid el Adh-ha wanapaswa watoe zakka ya nyama (kwa kuchinja mnyama kama vile ng’ombe, ngamia, mbuzi au kondoo) na kugawa nyama katika mafungu; kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kuwapa masikini na kuwapa majirani.

Hivyo sikukuu katika Uislam ni ibada, si siku ya kufanya uzinifu, kunywa pombe na kufanya kufuru. Ni siku ya kumtakasa Mwenyezi Mungu kwa sana na kuhudhuria katika vikao vya heri.

Aamkapo asubuhi anapaswa aazimie kwenda kuswali Swala ya Eid pamoja na Waislamu wenzake msikitini au kiwanjani na kisha kusalimiana na wenzake kwa kuepana mikono na kutakiana heri. Baada ya hapo Muislam anapaswa arudi nyumbani akale, kunywa na kufurahi na familia yake.

Tunawatakia wasomaji wetu sikukuu yenye heri na fanaka.