Tanzania ijifunze yatokanayo na uchaguzi Marekani

Tulishuhudia na tulisikia jinsi uchaguzi nchini Marekani ulivyoendeshwa. Kwa wenzetu, yapo masuala ambayo yako juu ya kila mtu na yalishapangiwa utaratibu unaofuatwa bila mchezo kwa miongo nenda rudi, mojawapo ni suala la uchaguzi. Kwa sababu Wamarekani wamemaliza kazi yao, Tanzania na nchi za Afrika zinayo mambo ya kujifunza. Nataka tuangazie masuala manne muhimu.

 

Utolewaji wa matokeo

Jambo moja ambalo Tanzania na Afrika zinapaswa kujifunza ni mfumo wa utoaji matokeo wa Marekani. Marekani ni nchi inayoundwa na majimbo/mataifa yaliyoungana yapatayo 50. Ina kilomita za mraba milioni 9.8 na ina watu milioni 324. Kwa hiyo hii ni nchi ya tatu kwa ukubwa wa eneo la jumla duniani na ni nchi ya nne kwa ukubwa wa eneo la ardhi duniani.

Marekani ilifanya uchaguzi Novemba 8, 2016 (kila baada ya miaka minne taifa hilo huchagua Rais na wajumbe wa mabaraza mawili ya maamuzi kwa tarehe hiyo hiyo, Novemba 8). Kesho yake, Novemba 9, 2016, ndani ya saa 12 tangu kufungwa kwa vituo vya kupigia kura, Wamarekani walimjua rais wao na alitangazwa bila kucheleweshwa. Tanzania yetu ina eneo la kilomita za mraba 950,000, unahitaji Tanzania 10 ili uwe na Marekani moja, kwa ukubwa, lakini wenzetu wanakamilisha uchaguzi wao ndani ya saa kadhaa. Hapa kwetu, matokeo ya jimbo moja la uchaguzi, tena la mjini, inaweza kuchukua siku tano masanduku hayajulikani yako wapi, hakika lazima tunalo la kujifunza.

 

Uwazi wa kura

Uchaguzi wa Marekani umetupatia ushahidi mwingine kwamba wenzetu wanaendesha mambo yao kwa uwazi mkubwa. Hadi mgombea anatangazwa, hatukusikia mahali popote kumetokea wizi wa kura au ujanja na wala hatujasikia mahali kokote kura zinarudiwa kuhesabiwa kwa sababu zozote, hili ni funzo kubwa.

Ifahamike kuwa Tume ya Uchaguzi ya Marekani haihusiki katika kusimamia uchaguzi wala kutangaza mshindi, tume hiyo inahusika na kudhibiti matumizi ya fedha tu katika kampeni za wagombea wote. Chaguzi zinasimamiwa kwa uwazi na mamlaka mbalimbali za kiserikali ambazo ziko kwenye majimbo mbalimbali.

Huu ni mfumo ambao hauwezi kujaribiwa huku kwetu, kwamba umpe rafiki yangu “Paul Makonda” kusimamia uchaguzi wa Dar es Salaam ambao John Magufuli anagombea na Edward Lowassa. Pamoja na uaminifu wa Makonda kwenye masuala mengine, kwenye hili lazima ataweka masilahi ya chama chake mbele.

Kwa Marekani hiyo si shida, pale Arusha Mjini uchaguzi unaweza kusimamiwa na Godbless Lema na bado mgombea wa CCM akawa mshindi na akatangazwa. Kwa hiyo uwazi katika uchaguzi ni jambo lililojiri sana, hivi sasa Wamarekani wanagombana na kuona aibu kwa nini Trump amechaguliwa, hawasemi kaiba kura, wanalaumiana kwa nini amepigiwa kura zote hizo.

Tanzania tunayajua yaliyotokea Zanzibar mwaka jana na tunayajua yaliyotokea Dar es Saalam katika kituo cha kukusanyia matokeo ya mgombea wa Ukawa. Wakati Marekani wanakaribisha uwazi kwenye uchaguzi, nchini tunataka kura zihesabiwe gizani.

 

Umuhimu wa midahalo

Katika Bara la Afrika kama kuna masuala yanayoogopwa sana na viongozi, hasa wa vyama vikongwe, ni midahalo. Viongozi hao hawapendi kuona mapambano ya hoja baina ya pande zinazoshindana katika uchaguzi.

Ama, vyama hivyo vitakubali midahalo katika uchaguzi ambao vina mgombea mzuri na mwenye mvuto na hoja kuliko wagombea wengine, zaidi ya hapo haiwezekani kukawa na midahalo.

Uchaguzi wa Marekani umetuonyesha kuwa uoga huo hauna umuhimu unaopewa. Hillary Clinton na Donald Trump walichuana kwenye midahalo mitatu, na yeyote aliyeangalia midahalo ile anafahamu kuwa Hillary alimshinda Trump, lakini kumbe hiyo haikuwa na maana kuwa Hillary atashinda urais.

Mwaka jana hapa Tanzania, Magufuli na Lowassa wangelishindana kwenye midahalo kadhaa na bado midahalo hiyo isingeliamua nani atakuwa rais. Mdahalo si mwisho wa uchaguzi, ni kipengele tu kinachowasaidia wapigakura kuwaelewa wagombea wao lakini kinawasaidia wagombea kueleza kwa kina vipaumbele vyao na namna walivyo na majibu ya masuala muhimu na maalumu ya wananchi.

Mwaka jana hapa kwetu yapo mashirika ya kiraia yalitaka kuwe na mdahalo wa wagombea lakini jambo hilo halikupewa uzito na wagombea wenyewe wala vyama vyao. Kenya ni mfano bora katika eneo hili na uchaguzi wa mwaka 2012 Uhuru Kenyatta alikuwa moto wa kuotea mbali na huwezi kujua midahalo ile ilimsaidia kiasi gani kuwa rais wa Kenya.

Vyama vya Afrika hukwepa midahalo kwa kuhofia kuanika madhaifu ya wagombea wao, madhaifu ambayo vyama hivyo huona ni bora yajulikane wakiwa Ikulu kuliko kabla ya kuchaguliwa. Woga huu ndiyo unawanyima wapiga kura fursa na haki ya kuwafahamu vizuri viongozi wao watarajiwa.

 

Uchaguzi wa hoja

Uchaguzi uliokwisha Marekani umetuonyesha umuhimu wa hoja zinazotekelezeka, jambo ambalo Tanzania tunalikosa. Majukwaa mengi ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana yalitawaliwa na matusi, kejeli, mashambulio binafsi na upuuzi mwingine mwingi. Hakukuwa na hoja. Sana sana ikiwa wagombea walizungumzia hoja muhimu za wananchi waliishia kutoa ahadi ambazo hazina ufafanuzi wa utekelezaji.

Mambo hayo hayapo Marekani. Donald Trump aliposema ataondoa mpango wa afya ulioasisiwa na Obama “Obamacare”, alieleza madhaifu ya mpango huo na akasema mpango anaokuja kuuleta utakuwa na sura zipi na utakuja kutatua madhaifu yapi, hakuna ujanja.

Hillary alipokuwa anaongelea wahamiaji na wageni kwenye nchi hiyo hakuishia kudai kuwa hatawaondoa nchini, kwanza alizungumzia historia yao, umuhimu wao, madhara ya kuwaondoa na faida za kuwabakiza kisha akasisitiza juu ya mpango wake kabambe wa kuifanya Marekani kuendelea kuwa taifa la watu wote. Ulikuwa ukizifuatilia hoja za wagombea wa Marekani unaziona zinatiririka kutoka mwanzo hadi mwisho, hakuna ujanja wala njia za mkato. Hapa Tanzania mgombea husimama na kusema “ntajenga barabara” na watu hushangilia, hakuna maelezo ya barabara itajengwaje na hakuna maelezo kwa nini barabara ni kipaumbele kuliko maji kwenye eneo hilo.

Mwisho wa siku tumekuwa na taifa ambalo kazi ya mgombea ni kuahidi kuwa atafanya kila kitu ambacho kinawasumbua wananchi. Kila ambacho ni tatizo, mgombea wa Tanzania husema ntatatua, hata yawe masuala 1,000 yote huahidi kuwa atayatatua.

 

Uadilifu wa wagombea

Mgombea wako ni muaminifu na mwadilifu kiasi gani? Rais ajaye, wa nchi yako ni mwaminifu na mwadilifu kiasi gani? Kipi ni kipimo cha uadilifu, uaminifu na mgombea mwaminifu na mwadilifu? Hilo ni swali kubwa na muhimu ambalo limeamua nani atakuwa Rais wa Marekani na Tanzania inapaswa kujifunza.

Trump hana maisha ya kificho, ameoa mara tatu ana watoto kadhaa wasio sirini, ana biashara kubwa ambazo zinafahamika, ana akaunti zenye mamilioni ya dola ambazo zinafahamika, ana majumba ya kuishi, ndege binafsi za maana, magari ya kifahari, viwanja vya gofu, hoteli, casino na mengineyo ya kifahari. Aliyonayo yote yanatambulika, hakuna siri, hakuna kificho.

Hapa Tanzania hadi tunashiriki kupiga kura mwaka jana hakuna aliyekuwa na orodha ya mali halisi anazomiliki mgombea wa Ukawa, Lowassa, wala mgombea wa CCM, Magufuli. Hii ni aibu kubwa sana kwa siasa za Afrika. Uaminifu na uadilifu wa Magufuli na Lowassa ulipimwa majukwaani kwa matusi, vijembe na visingizio na kila upande ulidai mgombea wake ni muadilifu zaidi lakini uadilifu bila vitendo na bila kuwaonyesha wapigakura uadilifu huo.

Leo ukiwauliza Watanzania Rais wao ana nyumba ngapi, hawajui, ana hoteli ngapi hawajui! Wenzetu wanahubiri uadilifu kwa vitendo, sisi tunauhubiri kwa maneno na ujanja ili mgombea wetu apigiwe kura uchaguzi upite. Haya ni madhaifu makubwa kabisa.

Kama tungelikuwa na chaguzi za kweli basi mwaka jana wagombea wenyewe wangebanwa na sheria na taratibu za wazi za kutangaza mali zao na utajiri wa kila mmoja kisha wananchi wangelipewa siku za kutosha kuhakiki mali za viongozi wao watarajiwa na kutoa taarifa kwa chombo kinachohusika ikiwa viongozi hao hawana mali na utajiri zaidi. Kwa nini tuongozwe na watu ambao hatujui wanamiliki nini? Bado tuna mengi ya kujifunza katika nyanja ya demokrasia, ukweli na uwazi.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa, Mtafiti na Mwanasheria. Simu; +255787536759/ Barua Pepe; [email protected]/ Tovuti; juliusmtatiro.com