Papa awakumbuka waathiriwa vita Palestina, Israel, Ukraine na ajali Japan

Muktasari:
- Papa amewaombea waathirika hao baada ya Katekesi yake ya kwanza kwa mwaka huu huku akiwasalimu waumini waliokuwa kwenye ukumbi wa Paulo VI
Vatican. Kutokana na madhira yanayoendelea maeneo mbalimbali duniani, kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amewakumbuka wale wote wanaopitia adha hiyo, tovuti ya Vatican News imeandika.
Papa ametoa maombi yake baada ya Katekesi yake ya kwanza kwa mwaka huu huku akiwasalimu waumini waliokuwa kwenye ukumbi wa Paulo VI.
Kupitia maombi hayo, Papa amewakumbuka Wapalestina, Waisraeli na Waukraine na waathiriwa wa tetemeko la ardhi na ajali ya ndege iliyotokea huko Japan.
Papa amewaombea pia waokoaji wa tetemeko la ardhi huko Japan katika vifo vilivyosababishwa na ajali ya ndege jijini Tokyo.
Idadi ya waliopoteza maisha katika tetemeko la mwaka mpya imeongezeka na kufikia watu 64.
Pia, ametoa wito wa kuwaombea amani watu hao na ameomba kusali kwa namna ya pekee kwa ajili ya kile kinachoendelea katika nchi za Mashariki na Ulaya.
“Tunawaombea watu wa Palestina, Israeli, Ukraine na maeneo mengine mengi ambapo kuna vita. Tusiwasahau ndugu zetu wa Rohingya wanaoteswa.
“Tusiwasahau watu walio vitani. Vita ni wazimu na tuombe kuwa na moyo wa kuelekea kwa maskini na wakimbizi,“ amesema.
Pia, ametoa wito wa kumwomba Mwenyezi Mungu, awaajalie moyo unaojali mahitaji ya maskini, wakimbizi na waathirika wa vita.