Puto lasababisha mvutano kati ya China, Marekani

Beijing. Maandamano yamefanyika mbele ya ubalozi wa Marekani jijini Beijing kuilaani Marekani kudungua puto la China.

Beijing jana ilizidisha kulaani uamuzi huo wa Washington kudungua puto hilo lililopita kwenye anga ya nchi hiyo na kudai kitendo hicho kinaweza kuwa, “pigo kubwa” kwa uhusiano baina ya nchi mbili hizo.

Makamu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Xie Feng alianzisha maandamano hayo akiishutumu Marekani kukiuka sheria za kimataifa.

Hata hivyo, China inataka busara itumike kuhusu mzozo wa ‘puto la kijasusi’ la China kwenye anga ya Marekani na kuhimiza kushughulikiwa “kwa busara,” mzozo huo.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken alilazimika kukatisha ziara yake mjini Beijing, akisema kuwapo kwa puto linalodaiwa kuwa ni la “kijasusi” ni “kitendo cha kutowajibika.”

Baadaye Marekani iliripoti puto lingine la pili la China lililokuwa likielea juu ya anga la Amerika ya Kusini.

Wakati mvutano huo ukiendelea, wapiga mbizi wa Jeshi la Wanamaji la Marekani wanafanya kazi ya kurejesha mabaki ya puto hilo kwenye pwani ya Carolina Kusini.

Ofisa mkuu wa zamani wa Jeshi la Marekani alisema alitarajia kazi hiyo ingemalizika haraka, ili wataalamu waanze kuchambua vifaa vyake.

Ndege za kivita zililidungua puto hilo kwenye eneo la maji ya Marekani Jumamosi iliyopita na uchafu umetapakaa katika eneo kubwa.

Marekani inaamini kuwa puto hilo lilikuwa likifanya ujasusi juu ya anga la Marekani kwa kufuatilia maeneo nyeti ya kijeshi.

Serikali ya China ilikanusha kuwa puto hilo lilitumika kwa shughuli za ujasusi na kusisitiza lilikuwa puto la hali ya hewa.

Aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Marekani, Mike Mullen, juzi alisema alifikiri kuwa huenda Jeshi la China lilirusha puto hilo makusudi ili kutatiza safari ya Blinken nchini China.

Wanasiasa wa Republican wakati huo huo, walimshutumu Rais wa Marekani Joe Biden kwa kutotimiza wajibu wake kwa kuruhusu puto kuvuka na kuingia katika anga la nchi bila kuzuiliwa.

Marco Rubio, makamu mwenyekiti wa kamati ya kijasusi ya Seneti, aliliambia Shirika la habari la CNN kuwa ni “juhudi kali” ya China kumwaibisha rais kabla ya hotuba yake ya Jumanne (leo). Puto hilo lilidunguliwa kutoka angani na kombora la anga la Sidewinder lililorushwa kutoka kwenye ndege ya kivita ya F-22.

Baadaye jana Jumatatu China ilithibitisha kuwa puto ya pili lililokuwa likiruka juu ya anga la Marekani na Caribean pia lilitoka China, ikilaumu hali ya hewa na uwezo wake mdogo wa kulidhibiti kutokana na “mkengeuko mkubwa kutoka kwenye njia iliyopangwa”. “Ni puto la kiraia lisilo na rubani kutoka China na linatumika kwa majaribio,” msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Mao Ning alisema.


Historia ya maputo ya kijasusi

Maputo yalikuwa mojawapo ya njia za mwanzo kutumika katika vita vya anga. Jukumu lake la awali lilikuwa ni kwa madhumuni ya upelelezi.

Historia ya matumizi ya puto za kijeshi ilianza mwishoni mwa karne ya 18, wakati Montgolfier, Joseph-Michel na Jacques-Étienne, walipoonyesha kwa mara ya kwanza uwezo wa puto za hewa-moto kwa matumizi ya kijeshi.

Matumizi ya kwanza maputo katika jeshi yaliyorekodiwa ni wakati wa Vita vya Mapinduzi vya Ufaransa (mwaka 1782–1783), wakati Jeshi la Ufaransa lilikusanya taarifa za kijasusi juu ya mienendo ya adui. Puto pia zilitumiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani, ambapo zilitumika kwa uchunguzi na mawasiliano.

Mwishoni mwa karne ya 19, maputo ya kijeshi yalianza kubadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia yaliyowezesha maputo hayo kuwa na vifaa vya kisasa zaidi kuwezesha kukusanya taarifa za kijasusi.

Yalitumika zaidi wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, lakini baada ya vita hivyo matumizi yake jeshini yalipungua kutokana na uvumbuzi wa ndege za kivita ambazo ni kiteknolojia iliyopunguza umuhimu wa mapuito hayo.

Kwa maana hii, puto ni mojawapo ya aina za zamani zaidi za teknolojia ya kufanya ujasusi. Wakati wa Vita Kuu ya Pili, wanajeshi wa Japan waliyatumia kurusha mabomu ya moto nchini Marekani mwaka 1941. Pia yalitumiwa sana na Marekani na Umoja wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi.

Baada ya Vita Kuu ya Pili, Jeshi la Marekani lilitengeneza miradi ya kutengeneza maputo yanayokwenda juu zaidi angani kwa ajili ya kugundua na kufuatilia nyuklia. Mojawapo ya miradi hiyo ni Project Mogul ambayo pia hujulikana kama ‘Operation Mogul’, Project Genetrix na Project Moby Dick.

Miongoni mwa maputo hayo ni yale yanayojulikana kama ‘Aerostats’ ambayo yametumiwa na Marekani na vikosi vya kijeshi vya muungano nchini Iraq na Afghanistan.

Kinachofanya maputo yaonekane bora ni uwezo wa kubaki angani kwa muda mrefu kwa sababu hayahitaji kujazwa mafuta mara kwa mara kama ndege na kwa sababu hiyo yanaweza kukusanya taarifa za kijasusi kwa muda mrefu bila kulazimika kutua.

Kwa nini China watumie puto wakati wana satelite? Benjamin Ho mratibu wa mpango wa China katika Chuo cha Rajaratnam cha Singapore nchini China anasema “wana njia nyingine ya kupeleleza miundombinu ya Marekani au kupata taarifa wanazozitaka. Puto lilikuwa kutuma ishara kwa Wamarekani na kuona jinsi ambavyo wangeitikia,” alisema Dk Ho.


Imetafsiriwa na William Shao.