12 watiwa mbaroni ajali ya moto iliyoua 29 China

Muktasari:

  • Watu 12 wamekamatwa na jeshi la polisi nchini China kufuatia ajali ya moto iliyoua watu 29 katika hospital moja mjini humo.

Beijing. Kufuatia ajali ya moto iliyoua takribani watu 29 katika hospitali moja mjini Beijing nchini China, jeshi la polisi linawashikilia watu 12 kwa mahojiano katika jitihada za kufahamu chanzo cha ajali hiyo.

Moto huo ambao ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi kutokea miaka ya hivi karibuni, ulizuka katika Hospitali ya Changfeng takribani saa 13:00 kwa saa za Beijing jana Jumanne.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) baadhi ya wananchi wamesema hawakulala wakijaribu kutafuta wapendwa wao.

Wakizungumza katika mkutano na wanahabari leo Jumatano Aprili 19, maofisa wa polisi wamesema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa cheche zilizotolewa wakati wa kazi za ukarabati zilikuwa zimewasha rangi iliyohifadhiwa.

Miongoni mwa walikamatwa ni mkurugenzi na naibu mkurugenzi wa hospitali moja mjini Beijing, pamoja na mkuu wa kampuni inayosimamia kazi za ukarabati katika hospitali hiyo.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha wagonjwa wakiruka kutoka madirishani kukimbia huku moshi mzito ukitoka nje ya jengo hilo.

Ndege isiyo na rubani ilitoa tangazo ikiwataka wagonjwa walionaswa kukaa watulivu na kusubiri kuokolewa.

Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba wazima moto waliwahamisha takribani watu 70 na kuzima moto ndani ya saa moja baada ya kuwasili.

Ndugu wa waathiriwa wameeleza kukasirishwa na wasimamizi wa hospitali hiyo wakisema hata saa nane baadaye maofisa wa hospitali hawakuweza kutaja majina ya waliojeruhiwa au waliofariki.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wa China pia wamekosoa ukosefu wa taarifa za kutosha kutoka katika tukio hilo kwa muda muda mrefu jana Jumanne.

"Kinachoshangaza sio tu kupoteza maisha, lakini pia ukimya wa kutisha wa vyombo vya habari ambavyo vilikuwa watazamaji wa tukio hilo. Matangazo rasmi tunayosoma yanaacha huzuni kubwa iliyosababishwa na maafa," ameandika mtumiaji wa mtandao wa Weibo.