Aliyemlipua mpenzi kwa petroli hadharani, arejeshwa Peru kuyakabili mashtaka

Muktasari:

  • Sergio Tarache Parra anashtakiwa kwa kumwagia petroli Katherine Gomez (18) na kumchoma moto katikati mwa mji mkuu wa Peru, Machi 2023.

Lima, Peru/ AFP.  Mwanamume mmoja wa Venezuela anayetuhumiwa kumchoma moto mpenzi wake wa zamani katika uwanja wa wazi nchini Peru amekamatwa na kurejeshwa mjini Lima, jana Jumanne.

Sergio Tarache Parra anashtakiwa kwa kumwagia petroli Katherine Gomez (18) na kumchoma moto katikati mwa mji mkuu wa Peru, Machi 2023.

Taarifa zinasema mtuhumiwa alikuwa ameachana naye siku zilizopita kabla ya uamuzi huo.

Tarache alifuatiliwa na kukamatwa nchini Colombia alikokimbilia mwezi uliofuata.

Kamera za usalama zilimnasa mshambuliaji wa Gomez akitoroka eneo la uhalifu na polisi wa Peru walitoa zawadi sawa na $12,500 kwa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwake, lakini haikufahamika kama kuna mtu aliyelipwa kiwango hicho kinachokaribia Sh30 milioni.

Baada ya tukio hilo, Gomez alilazwa hospitalini akiwa na majeraha ya moto kwa asilimia 60 kwenye mwili wake na alifariki dunia baada ya siku sita chungu, katika tukio lililowasikitisha raia wa Peru.

Katika kesi inayomkabili Tarache, waendesha mashtaka wanaomba kifungo cha maisha jela.

Katika katika tukio jingine kama hilo nchini humo, mwanamume mmoja aliyekuwa ndani ya basi mjini Lima mwaka 2018, alimmwagia petroli mpenzi wake wa zamani, Eva Agreda na kumchoma moto. Eva alikufa siku chache baadaye.