Auawa kwa risasi akiongea na wanahabari

Muktasari:

  • Mwanasiasa wa zamani nchini India ameuawa kwa kupigwa risasi pamoja na kaka yake wakati wakiongea na vyombo vya habari walipokuwa wakisindikizwa na maofisa wa Polisi kuelekea Hospitali kwa ajili ya kupima afya zao. 

India. Mbunge wa zamani wa India, Atiq Ahmad ameuawa kwa kupigwa risasi pamoja na kaka yake wakati wakihojiwa na wanahabari kuhusu tuhuma mbalimbali zilizofanya wahukumiwe jela baada ya kukutwa na makosa ya mauaji na utekaji nyara wakati alipokuwa kiongozi. 

 Tukio hilo limetokea jana Aprili 15, 2023 huku tukio hilo likiwa mubashara kwenye runinga wakati wakisindikizwa na maofisa wa polisi huku wakiwa wamefungwa pingu.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi ya leo Jumapili inasema Atiq na kaka yake Ashraf wameuawa na wanaume watatu waliojifanya kama waandishi wa habari waliowalenga vichwani ndugu hao wawili katika mji wa Prayagraj uliopo jimbo la Uttar Pradesh.

Ofisa wa polisi, Ramit Sharma amesema wauaji hao walikuja kwa pikipiki wakijifanya wanahabari. "Walifanikiwa kufika karibu na Atiq na kaka yake kwa kisingizio cha kurekodi lakini waliwafyatulia risasi. Wote walipigwa risasi kichwani."

Katika video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mtu akitoa bunduki karibu na kichwa cha Atiq Ahmad na kaka yake na baadae wote wakianguka chini.

Atiq Ahmad (60), alihukumiwa kwenda jela baada ya kukutwa na hatia ya kumteka nyara wakili aitwaye Umesh Pal, ambaye alitoa ushahidi dhidi yake kama shahidi katika mauaji ya mbunge mwaka 2005. Lakini mnamo Februari, Pal pia aliuawa.

Atiq ambaye alikuwa mbunge kwa awamu nne tofauti alikuwa alikabiliwa na kesi zaidi ya 100 za uhalifu na alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kutoka Uttar Pradesh kufunguliwa mashtaka chini ya sheria kali ya majambazi.


Imeandaliwa na Sute Kamwelwe.