Bodaboda, bajaji Karatu zalia ukosefu maeneo ya maegesho, CCM yaelekeza
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, akizungumza baada ya kuzindua shina la wakereketwa bodaboda,tawi la Karatu Mjini, Samaria leo Alhamisi Juni 4, 2026 ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya mkoani Arusha ambapo atakuwepo kwa siku tatu, kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Muktasari:
- Madereva wa bodaboda na bajaji wa Wilaya ya Karatu wameeleza changamoto ya ukosefu wa maeneo rasmi ya maegesho na vituo vya kupakia na kushusha abiria.
Karatu. Baadhi ya vijana wa bodaboda na bajaji katika Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, wameeleza kuwa ukosefu wa maeneo rasmi ya maegesho na vituo vya kupakia na kushusha abiria ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.
Wameeleza kuwa uhaba wa maeneo rasmi na salama ya kufanyia kazi umekuwa chanzo cha migogoro ya mara kwa mara kati yao na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mji.
Changamoto hiyo imebainishwa leo Alhamisi Juni 4, 2026 na Mwenyekiti wa shina la wakereketwa bodaboda, Tawi la Karatu Mjini Samaria, Hamisi Msangi, mbele ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi aliyepo ziarani wilayani humo.
Msangi amesema ukosefu wa maeneo rasmi ya vituo na maegesho ya bodaboda na bajaji, hali unawasababishia kuingia kwenye migogoro kati yao na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mji.
"Hadi sasa bado tunakabiliwa na uhaba wa maeneo salama na rasmi ya kupakia na kushusha abiria.Hali hii husababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya madereva na mamlaka na usimamizi wa mji," amesema.
Mbali na changamoto hiyo, amesema vijana hao wanakabiliwa na urasimu katika usajili wa vikundi na vyama vya ushirika, hali inayochelewesha utambuzi wa vikundi vyao kisheria na kuwakatisha tamaa baadhi ya vijana wanaotaka kujiunga katika shughuli za maendeleo.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kutoka katika mapato ya ndani, amesema wanashukuru kurejeshwa kwa mikopo hiyo ambayo imekuwa msaada mkubwa wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ila bado kuna changamoto.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, akizindua shina la wakereketwa bodaboda,tawi la Karatu Mjini, Samaria leo Alhamisi Juni 4, 2026 ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya mkoani Arusha ambapo atakuwepo kwa siku tatu, kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
"Ila kwenye hii mikopo kuna changamoto ya masharti magumu ya kibenki, vijana wengi wa kipato cha chini wanashindwa kufikia vigezo vilivyowekwa na taasisi za kifedha jambo linalowafanya washindwe kunufaika na mikopo hiyo.”
"Pia ucheleweshaji wa utoaji wa fedha, mara nyingi vikundi hukamilisha taratibu zote zinazotakiwa lakini fedha huchukua muda mrefu kutolewa, hali hii huathiri mipango ya biashara na kupunguza ari ya vijana na kujiletea maendeleo. Pia kuna ukosefu wa elimu ya biashara na usimamizi wa fedha jambo linalosababisha wakati mwingine kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati," amesema.
Akijibu hoja hizo, Kihongosi ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya vijiwe vya bodaboda na bajaji ili kuwawezesha vijana kufanya shughuli zao katika mazingira salama na yenye utaratibu.
Amesema bodaboda na bajaji ni ajira halali zinazowezesha maelfu ya vijana kujipatia kipato, kusomesha watoto na kuhudumia familia zao, hivyo zinastahili kutambuliwa na kuwekewa mazingira rafiki ya kufanya kazi.
"Maelekezo ya chama ni wazi. Halmashauri kwa kushirikiana na wataalamu wake itenge maeneo rasmi yatakayowezesha vijana hawa kufanya biashara zao kwa usalama na kwa utaratibu unaostahili," amesema Kihongosi.
Kihongosi amesema kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kutoka katika mapato ya ndani si hisani wala upendeleo wa viongozi, bali ni takwa la kisheria linalopaswa kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi.
Amesema CCM imepokea malalamiko kuhusu urasimu unaojitokeza katika upatikanaji wa mikopo hiyo na kuwataka viongozi wa wilaya na halmashauri kuhakikisha vikundi vyenye sifa vinapatiwa fedha hizo kwa wakati.
"Mikopo hii si hisani. Kila halmashauri ina wajibu wa kutenga sehemu ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Vijana wa Karatu wanapaswa kunufaika na fedha hizi kama ilivyo dhamira ya Serikali," amesema.
Ameagiza pia viongozi wa halmashauri kuhakikisha utekelezaji wa mikopo hiyo hauishii kwenye nyaraka za vikao bali unafika kwa walengwa ili kuwasaidia kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi.
Aidha, amewataka wananchi wa Karatu kuendelea kulinda amani na utulivu, akisema wilaya hiyo ni kitovu muhimu cha utalii na kwamba sekta hiyo haiwezi kustawi bila kuwepo mazingira ya amani.
"Amani ikitoweka, utalii utapungua, biashara zitadorora na wananchi wataathirika. Wajibu wa kulinda amani ni wa kila mwananchi wa Karatu," amesema.