Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu, Mkuu wa Gereza walivyokabana kwa maswali na majibu mahakamani

Muktasari:

  • Katika mwendelezo wa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mawakili wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, wakipinga vikwazo wanavyowekewa na maofisa wa Gereza la Ukonga wanapokwenda kushauriana na Lissu, leo Lissu amemhoji kwa maswali ya dodoso mkuu huyo wa gereza.



Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo Jumatano, Julai 22, 2026, anaendelea na hatua ya kumhoji kwa maswali ya dodoso Mkuu wa Gereza la Ukonga katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mawakili watatu wanaojitambulisha kuwa washauri wake wa kisheria.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 7300/2026 imefunguliwa na mawakili Nashon Nkungu, Paul Kisabo na Kulwa Maduhu, wakipinga vikwazo wanavyodai hukumbana navyo wanapokwenda kumwona na kushauriana naye katika Gereza la Ukonga, ambako Lissu anashikiliwa kwa kesi ya uhaini.

Wanadai wamekuwa wakinyimwa faragha na kuzuiwa kufanya mashauriano ya siri na mteja wao, kinyume na Kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza, huku wakiiomba Mahakama itangaze vitendo hivyo kuwa ni kinyume cha sheria na Katiba.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamishna Mkuu wa Magereza, Mkuu wa Gereza la Ukonga, Tundu Lissu na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambacho kiliunganishwa baadaye katika shauri hilo kama mdaiwa mwenye maslahi.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Amir Mruma, Dk Angelo Rumisha na Dk Everist Longopa, ambalo lilipendekeza isikilizwe kwa njia ya maandishi pamoja na pingamizi la awali lililowekwa na Serikali.

Hata hivyo, Lissu aliomba na akakubaliwa kuwaita na kuwahoji wadai pamoja na mdaiwa wa tatu, Mkuu wa Gereza la Ukonga.

Usikilizwaji wa kesi hiyo katika hatua hiyo ulianza Jumatatu hii, ambapo jopo hilo linaketi Dar es Salaam. Lissu alianza kuwahoji kwa maswali ya dodoso walalamikaji na leo anaendelea na mkuu wa gereza hilo.

Katika maswali hayo, Lissu ameanza kumuuliza Mkuu wa Gereza la Ukonga iwapo Sheria ya Magereza na Kanuni za Magereza zinampa Kamishna Mkuu wa Magereza mamlaka ya kutunga maagizo (Prisons Standing Orders - PSO) yanayohusu wafungwa, au kama mamlaka hayo yanabaki kwa waziri mwenye dhamana.

Mahojiano hayo yalihusisha marejeo ya vifungu mbalimbali vya Sheria ya Magereza na Kanuni za Magereza, huku majaji wakilazimika kuingilia kati mara kadhaa kumwelekeza shahidi kujibu maswali yanayoulizwa.

Lissu: Angalia kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Magereza, waeleze majaji kama mamlaka ya Kamishna Mkuu ya kutunga Prisons Standing Orders yanahusu maofisa wa magereza pekee. Ni kweli au si kweli?

Mkuu wa Gereza: Si kweli.

Lissu: Wasomee majaji kifungu cha 5(2) kinasemaje.

Mkuu wa Gereza: (Akasoma kifungu cha 5(1)).

Lissu: Nimesema usome kifungu cha 5(2).

Mkuu wa Gereza: Naomba urudie swali.

Lissu: Waeleze majaji kama mamlaka ya kamishna mkuu yanahusu wafungwa.

Mkuu wa Gereza: Yanahusu wafungwa na maofisa wa magereza.

Lissu: Naomba ukisome kifungu hicho.

Mkuu wa Gereza: Kinasema prisons na prison officers.

Lissu: Waeleze majaji kama kuna neno prisoners.

Mkuu wa Gereza: Ukisema prisons ni pamoja na wafungwa.

Lissu: Kama prisons ni pamoja na prisoners, je ni pamoja na prison officers? Kwa nini prison officers wametajwa peke yao?

Mkuu wa Gereza: Majaji, mimi si mwanasheria. Mwenye uwezo wa kutafsiri sheria ni mwanasheria.

Lissu: Wewe ndiye shahidi na umetueleza unawajibika na hayo yote, tuendelee. Waeleze majaji kama ni kweli au si kweli mtu pekee mwenye mamlaka ya kutunga kanuni zinazohusu wafungwa ni waziri.

Mkuu wa Gereza: Nimesema mimi si mtaalamu wa sheria.

Hata hivyo, Jaji Mruma alimkumbusha mkuu huyo wa gereza kwamba yeye ndiye mtekelezaji wa sheria.

“Unataka kutuambia huzijui sheria unazozitekeleza?” alihoji Jaji Mruma.

Mkuu wa Gereza: Nazifahamu.

Lissu: Kama unazifahamu, waeleze majaji kama mtu pekee mwenye mamlaka ya kutunga kanuni zinazohusu wafungwa ni waziri peke yake, si kamishna mkuu.

Mkuu wa Gereza: Naomba urudie swali.

Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 105 cha Sheria ya Magereza, mtu pekee mwenye mamlaka ya kutunga kanuni zinazohusu wafungwa ni waziri peke yake?

Mkuu wa Gereza: Hapana.

Lissu: Angalia kifungu cha 105(1).

Mkuu wa Gereza: Nimekiona.

Lissu: Waeleze majaji kama mtu pekee mwenye mamlaka ya kutunga kanuni za kusachi wafungwa, maaskari na wageni ni waziri.

Mkuu wa Gereza: Si kweli.

Lissu: Kifungu kinasemaje?

Mkuu wa Gereza: (Akasoma kifungu hicho).

Lissu: Kifungu kinasema mamlaka ya waziri ni kutunga kanuni za kusachi wafungwa, maaskari na wageni, ni kweli au si kweli?

Mkuu wa Gereza: Ni kweli.

Lissu: Angalia kifungu cha 105(1)(l), waeleze majaji kama ni kweli kwamba waziri ndiye mwenye mamlaka ya kutunga kanuni zinazohusu usimamizi na utunzaji wa wafungwa.

Mkuu wa Gereza: Ndiyo.

Lissu: Nenda kwenye kifungu cha 105(1)(aa). Waeleze majaji kama ni kweli kwamba waziri ndiye mwenye mamlaka ya kuamua namna kanuni hizo zitakavyotekelezwa.

Mkuu wa Gereza: Ni kweli.

Lissu: Kutokana na majibu hayo, waeleze majaji ni wapi Sheria ya Magereza inamruhusu kamishna mkuu kutunga PSO zinazohusu wafungwa?

Mkuu wa Gereza: Kamishna Jenerali amepewa mamlaka ya kutunga orders. Nilisema Prisons Standing Orders hazihusu askari pekee, zinahusu pia wafungwa.

Lissu: Kwa sheria ipi?

Mkuu wa Gereza: Waziri wa Mambo ya Ndani amempa mamlaka Kamishna Jenerali kutunga kanuni zinazohusu askari magereza na wafungwa.

Lissu: Sahihisha. Waziri humuagiza Kamishna Mkuu, si Kamishna Jenerali kama unavyomuita.

Mkuu wa Gereza: Na wafungwa pia.

Lissu: Sawa. Sitaki ugomvi na mtu anayenilea huko mahabusu.

Lissu: Kanuni ya 33 imeeleza wafungwa wa adhabu ya kifo wanatakiwa wale namna gani?

Mkuu wa Gereza: Inazungumzia prisoners' diet.

Lissu: Afande, unaniangusha, nikusomee?

Mkuu wa Gereza: Soma.

Lissu: Nataka tuondoke hapa tukielewa kuwa hizi kanuni zinaelekeza hadi chakula cha wafungwa.

Mkuu wa Gereza: Jeshi la Magereza haliongozwi na kanuni pekee, linaongozwa na sheria, kanuni na standing orders.

Lissu: Sasa nipo kwenye kanuni.

Lissu aliendelea kumuuliza kuhusu Kanuni ya 33(1A), akitaka afafanue kama wafungwa wa adhabu ya kifo wanapaswa kulindwa na maofisa wawili muda wote.

Mkuu wa Gereza: Inasema hivyo.

Lissu: Waeleze majaji kama mahabusu kama mimi anatakiwa kulindwa usiku na mchana kwa mujibu wa kanuni hizo.

Mkuu wa Gereza: Nimesema Jeshi la Magereza haliongozwi na kanuni peke yake.

Lissu: Asante, umesema linaongozwa na sheria, kanuni na PSO. Kwa kanuni hizi, ni wapi panasema mahabusu kama mimi alindwe usiku na mchana?

Mkuu wa Gereza: Kanuni hazisemi.

Katikati ya maswali na majibu, mmoja wa majaji alimwambia shahidi asijitafutie presha, akisisitiza kuwa kanuni hizo hazijatungwa na shahidi wala jaji, hivyo kama hajui anaweza kusema hajui.

Lissu: Asante, Jaji, kwa kunisaidia. Afande (Mkuu wa gereza) anahisi tunamkaanga, si kosa lako. Kanuni huzitunga mamlaka husika, si wewe, mimi wala majaji.

Lissu aliendelea kwa kurejea Kanuni ya 33(3).

Lissu: Waeleze majaji kama ni kweli kwamba ni wafungwa wa adhabu ya kifo pekee wanaotakiwa kulindwa na mazungumzo yao kusikilizwa wanapotembelewa na wageni.

Mkuu wa Gereza: Kifungu hicho kinazungumzia wafungwa wa adhabu ya kifo.

Lissu: Ndicho ninachouliza.

Mkuu wa Gereza: Kwa mujibu wa kifungu hicho, ni sawa.

Lissu: Kwa kanuni hizi, mahabusu au mfungwa wa kifungo cha maisha, miaka 30 au hata siku moja, hatakiwi kulindwa na askari wawili muda wote kama ilivyo kwa wafungwa wa adhabu ya kifo.

Mkuu wa Gereza: Si kweli.

Lissu: Waoneshe majaji kama mfungwa asiye wa adhabu ya kifo anasimamiwa kwa kanuni hizi kama mwenye adhabu ya kifo.

Mkuu wa Gereza: Jeshi la Magereza linaongozwa na sheria, kanuni na standing orders.

Jaji alimwambia shahidi kwamba, “Kwa sasa tunazungumzia kanuni. Kama kuna sheria nyingine, wakili wako atakuongoza,” na Lissu aliendelea.

Lissu: Waeleze majaji kama kwa kanuni hizi mfungwa asiye wa adhabu ya kifo anaweza kusimamiwa na askari wawili usiku na mchana au anapotembelewa na mawakili au ndugu zake.

Mkuu wa Gereza: Kwa kanuni hii hakipo.


Kesi inaendelea, endelea kufuatilia Mwananchi.