Simanjiro waiomba CCM kuingilia kati migogoro ya ardhi
Muktasari:
- Ombi hilo lilitolewa na wananchi hao pamoja na Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya mbele ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Alhamisi Juni 4, 2026, katika viwanja vya Naisinyai wilayani humo.
Simanjiro. Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, wamekiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) kuingilia kati migogoro ya ardhi inayowakabili, huku chama hicho kikitoa onyo kwa viongozi wa kata, vijiji na vitongoji wanaouza ardhi kinyume cha sheria.
Ombi hilo lilitolewa na wananchi pamoja na Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, mbele ya Katibu wa NEC wa CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Juni 4, 2026 katika viwanja vya Naisinyai.
Ole Millya, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amesema migogoro ya ardhi imeendelea kuwa kero kubwa kwa wananchi wa Simanjiro na ndiyo malalamiko anayokutana nayo mara kwa mara. Amesema ardhi ya wananchi inaendelea kuuzwa kiholela, jambo linalotishia shughuli za ufugaji na kilimo, na kusisitiza kuwa sheria lazima zifuatwe ili kulinda haki za wananchi.
Pia amewataka wawekezaji wa madini Mererani kuhakikisha wananchi wa Simanjiro wananufaika na rasilimali hizo kupitia ajira, biashara na fursa nyingine za kiuchumi.
Kwa upande wake, Kenani Kihongosi amewaonya viongozi wa kata, vijiji na vitongoji wanaohusika na uuzaji wa ardhi bila kufuata utaratibu wa kisheria, akisisitiza kuwa CCM haitavumilia vitendo vinavyosababisha migogoro na kuwaumiza wananchi.
Jengo la soko la madini ya Tanzanite na vito (Tanzanite Exchange Centre), wakati wa ukaguzi wa jengo hilo lililogharimu Sh5.4 bilioni, lililopo wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara
Aidha, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, pamoja na viongozi wengine wa serikali kusimamia kwa ukali sheria za ardhi ili kuzuia wananchi kupoteza maeneo yao kwa njia zisizo halali. Amesisitiza kuwa chama kitawachukulia hatua viongozi watakaobainika kukiuka sheria na kuathiri maslahi ya wananchi.
Kihongosi pia amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini ubadhirifu wa ardhi, huku akisisitiza umuhimu wa uadilifu kwa viongozi na kutanguliza maslahi ya wananchi badala ya manufaa binafsi.
Baada ya mkutano huo, baadhi ya wananchi waliunga mkono kauli za viongozi hao na kuomba hatua za haraka zichukuliwe kumaliza migogoro ya ardhi.
Mkazi wa Kijiji cha Naisinyai, Moses Mollel, amesema migogoro ya ardhi imekuwa chanzo cha migongano kati ya wafugaji na wakulima na kuathiri uzalishaji, hivyo akataka utekelezaji wa vitendo ili ardhi ilindwe.
Naye mkazi wa Simanjiro, Nasieku Ole Kasaine, amesema wanawake wengi wameathiriwa na migogoro hiyo kutokana na changamoto za kufuatilia mashauri mahakamani. Ametaka sheria zisimamiwe kwa haki na hatua kali zichukuliwe dhidi ya viongozi watakaobainika kushiriki uuzaji holela wa ardhi ili kurejesha imani ya wananchi na kupunguza migogoro ya muda mrefu.