Balaa jingine kwa Kenyatta, ashtakiwa kuitisha mkutano haramu

Muktasari:

  • Mwanachama wa chama cha Jubilee nchini Kenya Hassan Osman amemshtaki Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa Kenya, akiitaka kubatilisha mpango wa mkutano wa chama hicho uliopangwa na Kenyatta; akisema ni mkutano haramu.

Kenya. Aliyewahi kuwa Mbunge kupitia chama cha Jubilee nchini Kenya Hassan Osman, ameiandikia barua Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa nchini humo (PPDT), akiitaka kumzuia Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kufanya mkutano wa Kitaifa na wajumbe wa Chama hicho mnamo Mei 22, 2023.

Kwa mujibu wa kituo cha Televisheni cha Citizen, Mbunge huyo wa zamani ambaye ni mwanachama wa Chama cha Jubilee; ametaja kwamba mkutano huo sio halali na huenda ukakivuruga chama hicho.

Osman ameongeza kuwa pande mbili zinazokinzana, mmoja ukiongozwa na wanaomuunga mkono Kenyatta, Jeremiah Kioni na Kagwe Gichohi na upande mwingine wa Sabina Chege na Kanini Kega, zimejaribu kuvunja katiba ya uanachama na uongozi wa chama bila kufuata utaratibu.

Osman ameitaka mahakama kusitisha Mkutano huo akisema kwa sasa matawi ya chama hayafanyi kazi, na kwamba nyaraka za chama hazipatikani kwa urahisi, na hivyo kuzua hofu kuwa huenda wasio wanachama wakashiriki katika mkutano huo.

Hata hivyo mahakama bado haijatoa uamuzi kuhusu suala hilo.

Itakumbukwa kwamba baadhi ya wanachama na viongozi wa Jubilee wakiongozwa na mbunge wa Afrika Mashariki, Kanini Kega walimtimua Kenyatta kutoka kwenye wadhifa wa kiongozi wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa Kamati ya Kitaifa (NEC) Mei 3 mwaka huu, Kega alimtangaza mbunge mteule Sabina Chege kama Kaimu Kiongozi wa chama hicho.

"Mkutano wa Kamati ya Kitaifa uliamua kuwa Sabina Chege atahudumu kama Kaimu Kiongozi wa Chama hadi pale ambapo tutaandaa mkutano wa kitaifa wa wajumbe ambako tutateua Kiongozi ambaye ataongoza chama kwenda mbele," Kega alisema.