Kenyatta kuondoka Azimio, ajikita kutafuta amani

Muktasari:

Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta anatarajiwa kujiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti wa Baraza la Muungano wa Azimio la Umoja ilikujikita katika masuala ya amani.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta anatarajiwa kujiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti wa Baraza la Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ili ajikite katika ujenzi wa masuala ya amani.

Muungano wa Azimio ndiyo uliomdhamini kiongozi wa upinzani, Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga kugombea urais Agosti mwaka huu, ambapo Rais William Ruto aliyewakilisha chama cha UDA.

Akizungumza na mtandao wa Daily Nation jana, msaidizi wa muda mrefu wa Kenyatta, David Murathe amesema kuwa Azimio wanatarajiwa kuitisha mkutano wa ngazi za juu ili kumpa nafasi Kenyatta kujiuzulu wadhifa wake.

Tangu amemaliza muda wake madarakani, Kenyatta amekuwa akiongoza mazunguzo ya kutafuta amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Aidha, kujiuzulu kwake kumeelezwa na matakwa ya kisheria kwamba hapaswi kushikilia wadhifa wowote wa chama cha siasa ili apate pensheni yake.

Kulingana na Sheria ya Mafao ya Kustaafu ya Rais, 2003, Kenyatta ana nafasi ya hadi Februari 2023 kujiuzulu nafasi hizo.

Pia inaelezwa kujiuzulu kwa Kenyatta huenda kukasababisha mkwamo mkubwa wa kisiasa kwa Odinga, ambaye kwa sasa anajaribu kuunganisha wanajeshi wake kuunda vuguvugu kuu dhidi ya serikali.

Muungano huo, ulioleta pamoja angalau vyama 26 vya kisiasa, uliunda vyombo viwili Baraza la Muungano na Baraza Kuu la Muungano wa Kitaifa (NCEC).