Bibi adakwa akila njama kumuuza mjukuu wake Sh7 milioni
Muktasari:
- Bibi mmoja jijini Nairobi amejikuta kwenye mazingira ya kutatanisha baada kukamatwa na polisi akila njama za kumuuza mjukuu wake wa siku tano aliyemchukua kwa lengo la kumlea ili mwanaye aendele na masomo.
Nairobi. Mwanamke mmoja (jina limehifadhiwa) jijini Nairobi nchini Kenya ameshtakiwa kwa kosa la kula njama ya kumuuza mjukuu wake kwa Sh400,000 ya nchini humo (Sh6.9 milioni).
Mwanamke huyo mwenye miaka 39 alikamatwa Aprili 9, 2023 na polisi ambao walijifanya wana nia ya kumnunua mtoto huyo mdogo mwenye siku tano.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la nchini humo limeripoti kuwa mtuhumiwa huyo alimchumkua mjukuu wake Kaunti ya Kakamega baada ya mtoto wake mwenye umri wa miaka 16 kujifungua na kumtaka akamlee mjini Nairobi ili binti yake aendelee na masomo.
Baada ya kufika Nairobi, mwanamke huyo alianza kutafuta mteja wa kumuuzia mtoto huyo kabla hajatiwa mikononi mwa polisi
“Walipanga kukutana kwenye mgahawa mmoja jijini Nairobi na hatimaye kuwakamata, wakamwokoa mtoto huyo na kumpeleka kwenye kituo cha kulelea watoto,” tovuti ya Daily Nation imeripoti.
Mshukiwa huyo yupo rumande tangu akamatwe baada ya polisi kupata agizo hilo kutoka mahakamani.
Imeandaliwa na Pelagia Daniel