Bunge la Seneti lapunguza makali muswada wa uhusiano wake na Tanzania
Muonekano wa ndani ya Bunge la Semeti la Marekani. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Marekebisho ya muswada wa Seneti ya Marekani yameondoa kusitishwa kwa misaada ya usalama kwa Tanzania, lakini yamebakiza vikwazo vya ufadhili wa maendeleo, fedha za MCC, na hatua dhidi ya watu binafsi kupitia sheria ya Global Magnitsky.
Dar es Salaam. Bunge la Seneti la Marekani limefanya marekebisho ya muswada unaohusu uhusiano kati ya Marekani na Tanzania, kwa kuondoa pendekezo la kusitisha misaada ya usalama na ushirikiano wa kijeshi kwa Tanzania.
Lakini, Bunge hilo limebakiza vikwazo vinavyohusu ufadhili wa maendeleo na hatua nyingine zilizopendekezwa awali.
Toleo jipya la muswada huo wa S.4577, linatarajiwa kujadiliwa na Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni Juni 17, mwaka huu, kwa mujibu wa waraka wa uliotolewa leo, Juni 11, 2026.
Waraka huo unaeleza kuwa, marekebisho hayo yaliyowasilishwa na Seneta, Jeanne Shaheen yamebadilisha kwa kiasi kikubwa muswada wa awali kwa kuhakikisha kuwa ushirikiano wa kiusalama kati ya Tanzania na Marekani unaendelea kuwepo.
“Muswada wa awali ulipendekeza kusitishwa kwa misaada ya usalama na ufadhili wa maendeleo. Marekebisho haya mapya yanahusu kusitisha ufadhili wa maendeleo pekee,” inaeleza.
Muswada huo uliwasilishwa Mei 19 na Seneta Jeanne Shaheen pamoja na Seneta, Ted Cruz baada ya matukio ya Oktoba 29, mwaka 2025 nchini, yaliyohusisha vurugu zilizosababisha mauaji ya watu.
Katika toleo la awali, Marekani ilipendekeza kuzuia misaada ya usalama na ufadhili wa maendeleo kwa Tanzania.
Vikwazo hivyo vingehusisha fedha kutoka Shirika la Kimataifa la Marekani la Ufadhili wa Maendeleo (DFC), Benki ya Mauzo ya Nje na Uagizaji ya Marekani na Shirika la Biashara na Maendeleo la Marekani.
Hata hivyo, marekebisho mapya yameondoa masharti yaliyohusu misaada ya usalama huku yakibakiza vikwazo vinavyohusu ufadhili wa maendeleo.
Muswada huo, uliorekebishwa pia unaendelea kupendekeza kuzuiwa kwa ufadhili wa Shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC) kwa Tanzania hadi masharti maalumu yaliyowekwa yatakapotekelezwa.
Mabadiliko mengine, ni kuingizwa kwa kifungu kinachoruhusu msamaha kwa kuzingatia masilahi ya Taifa la Marekani.
Chini ya marekebisho hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani atakuwa na mamlaka ya kuondoa au kusamehe vikwazo vya misaada na uwekezaji ikiwa ataona hatua hiyo inalinda maslahi ya taifa la Marekani. Kifungu hicho hakikuwepo katika muswada wa awali.
Aidha, marekebisho hayo yamebadilisha mfumo wa vikwazo uliopendekezwa. Badala ya kuanzisha mfumo mpya wa vikwazo, muswada huo sasa unapendekeza matumizi ya sheria iliyopo ya Global Magnitsky, kuwachukulia hatua watu binafsi watakaobainika kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu au vitendo vya rushwa.
Licha ya mabadiliko hayo, baadhi ya vipengele vya muswada huo vimeendelea kubaki bila kubadilishwa.
Muswada huo, bado unataka kufanyika kwa tathmini ya kina ya uhusiano kati ya Marekani na Tanzania, ikiwamo uchambuzi wa mahusiano ya kijeshi, kiuchumi na kisiasa ya Tanzania na China.
Pia, unataka kuandaliwa kwa taarifa itakayowataja maofisa waandamizi wa Serikali, chama tawala, Jeshi la Polisi, jeshi la ulinzi na vyombo vya usalama ambao watabainika kuwajibika au kushiriki katika ukiukwaji wa haki za binadamu unaotajwa ndani ya muswada huo.
Kwa mujibu wa waraka huo, marekebisho yaliyowasilishwa yanaendeleza baadhi ya malengo makuu ya muswada wa awali huku yakipunguza ukubwa wa hatua zilizokuwa zimependekezwa hapo mwanzo.
“Muswada uliorekebishwa unalinda uhusiano wa kiusalama, unatoa mamlaka ya uamuzi kwa Serikali ya Marekani kupitia kifungu cha msamaha na unatumia mfumo uliopo wa vikwazo.
“Hata hivyo, bado unahifadhi vikwazo dhidi ya watu binafsi, kusitishwa kwa ufadhili wa maendeleo, kuzuiwa kwa fedha za MCC na ulazima wa kufanya tathmini mpya ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili,” inaeleza taarifa hiyo.
Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni inatarajiwa kwanza kujadili marekebisho hayo kabla ya kuamua kama muswada huo uliorekebishwa utaendelea na hatua nyingine za kisheria.
Waraka huo umefafanua kuwa, hata kama kamati hiyo itaidhinisha muswada huo, hatua hiyo haitamaanisha kuwa tayari umekuwa sheria.
Muswada huo bado utapaswa kupitishwa na seneti nzima, kisha Baraza la Wawakilishi la Marekani kabla ya kupelekwa kwa Rais wa Marekani kwa ajili ya kutiwa saini kuwa sheria.
Iwapo muswada huo utapitishwa katika mfumo wake wa sasa, ushirikiano wa kiusalama na kijeshi kati ya Tanzania na Marekani utaendelea, sambamba na programu za misaada ya kibinadamu na afya.
Hata hivyo, ufadhili wa maendeleo na fedha za MCC utaendelea kuwa chini ya vikwazo vilivyowekwa ndani ya muswada huo.