Chanjo nyingine ya Ebola yazinduliwa DRC

Kinshasa. Mamlaka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimezindua chanjo ya nyingine kukinga dhidi ya virusi vya Ebola, Chama cha Madaktari wasio na mipaka (MSF) kimesema.

Kimesema chanjo hiyo ilitengenezwa na kampuni ya Johnson & Johnson na Ubelgiji, inalenga kuwakinga wati 50,000 ndani ya miezi minne.

Watu zaidi ya 250,000 katika eneo hilo wamekwishapata chanjo nyingine mwaka jana.

DRC iliitangaza Ebola janga Agosti 2018 katika maeneo yenye mapigano ya Kivu Kaskazini, Kusini  na Ituri katika mpaka wake na uganda, rwanda na Burundi.

Ugonjwa huo unaoambukiza tayari umeua watu 2,193 kwa mujibu wa taarifa rasmi za Serikali.

Juhudi za kukabiliana na janga hilo zimekuwa zinakwamishwa si tu na mapambano, bali na kukosa utayari wa jamii kufuata taratibu za kinga na huduma kwa wagonjwa na mazishi salama.

Wahudumu wa afya wanaopambana na Ebola wameshambuliwa na wananchi karibu mara 300 na kati yao sita wamefariki na 70m kujeruhiwa tangu Januari mwaka huu, waziri wa afya wa nchi hiyo alisema mapema mwezi huu.

Mapema leo asubuhi, watu 15 wamechomwa sindano ya chanjo katika moja ya vituo viwili vya MSF kaskazini mwa Kivu, msemaji wa taasisi hiyo amesema.

Kwa mujibu wa MSF chanjo hiyo inatolewa kwa awamu mbili, kwamba wanaopata mara ya kwanza wanaeleza warudi tena mara ya pili kukamilisha.

Chanjo ya J&J awali ilikataliwa na Waziri wa zamani wa Afya wa Congo, Oly Ilunga, akieleza athari za kuitoa katika jamii ambazo kutoaminiana kuhusu Ebola bado kuko juu.

Lakini kujiuzulu kwa Ilunga Julai mwaka huu kunaonekana kufungua milango kwa chanjo hiyo kuruhusiwa. Kwa saa anakabiliwa na mashtaka ya kutumia vibaya fedha zilizotengwa kwa mapambano dhidi ya Ebola.

Chanjo hiyo imezinduliwa siku tatu baada ya Tume ya Ulaya kuidhinisha uuzaji wa chanjo nyingine ya ugonjwa wa Ebola. 

Akizungumza Jumatatu Novemba 11, nchini Ubeligi, Kamishna wa Afya, Vytenis Andriukaitis alisema kuwa kupata chanjo dhidi ya virusi hivyo hatari haraka iwezekanavyo ni kipaumbele kwa jamii ya kimataifa.

Andriukaitis alisema baada ya majaribio yaliyofanywa na wakala wa dawa wa Ulaya (Ema) itairuhusu kampuni kubwa ya kuuza dawa Marekani, Merck kuanza kuisambaza kwa jina la Everbo.