Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Familia yaomba mwili wa baharia aliyefariki Hormuz urejeshwe haraka

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tasac,  Mongu alifariki dunia Mei 3, 2026 akiwa kazini katika meli ya kuvuta yenye jina la Volans iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Musoma. Familia ya baharia Mtanzania, Mchama Mongu aliyefariki dunia baada ya meli aliyokuwa akihudumu kushambuliwa kwa bomu katika Mfereji wa Hormuz, imeiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kurejesha mwili wake nchini kwa ajili ya mazishi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tasac, Mongu alifariki dunia Mei 3, 2026 akiwa kazini katika meli ya kuvuta yenye jina la Volans iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa meli hiyo ilikuwa safarini kuelekea Oman ikitokea UAE kabla ya kushambuliwa wakati ikivuka Mfereji wa Hormuz, eneo muhimu la kimkakati lililopo kati ya Iran na Oman.

Akizungumza nyumbani kwa familia mjini Musoma leo Alhamisi Mei 7, 2026, baba wa marehemu, Mongu Mabuli amesema mwanawe aliondoka nchini Aprili 13, 2026 baada ya mapumziko ya muda yaliyotokana na hali ya taharuki iliyokuwa imejitokeza kufuatia mvutano wa kijeshi kati ya Marekani na Iran.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa nyumbani kwao baharia mtanzania Mchama Maregesi Mongu mjini Musoma. Mongu alifariki dunia baada ya meli yao kushambuliwa na bomu katika Mfereji wa Hormuz . Picha na Beldina Nyakeke

Amesema hadi sasa familia bado haijapata taarifa rasmi kuhusu lini mwili wa marehemu utawasili nchini kwa ajili ya maziko, hali iliyosababisha ndugu wa karibu pekee kukusanyika wakati wengine wakisubiri taarifa kamili.

“Kwa sasa tuko nyumbani kwa wazazi wa marehemu na si nyumbani kwake. Tunasubiri taarifa rasmi ya lini mwili unawasili ili taratibu za msiba ziweze kuendelea rasmi katika Mtaa wa Makoko ambako ndipo alipokuwa akiishi,” amesema Mabuli.

Amesema kabla ya kuanza kazi ya ubaharia, marehemu alipata elimu nchini na baadaye nchini Kenya, huku taaluma ya ubaharia akiisomea katika Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam.

Baada ya kuhitimu masomo yake, amesema  Mchama alikwenda Dubai ambako alianza rasmi kazi ya ubaharia.

Kwa mujibu wa baba huyo, marehemu alikuwa amefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 10, awali alikuwa akipata mapumziko kila baada ya miezi mitatu kabla ya baadaye kuingia mkataba uliomruhusu kupata likizo mara moja kwa mwaka.

“Likizo yake ya mwisho alikuja mwaka jana na alifika hadi Musoma. Baada ya likizo kuisha alitakiwa kurudi kazini lakini alichelewa kutokana na hali ya vita. Tarehe 13 Aprili alinipigia simu akaniambia hali imetulia na anarudi kazini,” amesimulia mzee huyo.

Familia hiyo imesema inatarajia kumzika marehemu katika makaburi ya Mwisenge baada ya mwili kuwasili nchini na taratibu zote kukamilika.

Aidha, imeelezwa kuwa marehemu ameacha mjane na watoto watano.

Mdogo wa marehemu, Juma Mongu amesema tayari mwili wa ndugu yao umehamishiwa Dubai huku taratibu za kuusafirisha kuja Tanzania zikiendelea.

“Nimewasiliana na nahodha wa kule ambaye amesema taratibu zinaweza kuchukua hadi wiki mbili. Tunaiomba Serikali itusaidie mwili wa kaka yetu urejeshwe mapema nyumbani ili azikwe kwa heshima,” amesema.

Naye mama wa marehemu, Felista Mongu amesema kifo hicho ni pigo kubwa kwa familia kutokana na ukaribu aliokuwa nao na mwanawe.

“Tunaomba Serikali itusaidie haki zote za mwanangu zipatikane na mwili wake urudishwe nyumbani tuje tumzike anavyostahili,” amesema.