Baharia Mtanzania auawa shambulio la bomu Hormuz
Sehemu ya Mlango wa Hormuz. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Shirika hilo linaeleza masikitiko yake kufuatia tukio hilo na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.
Dar es Salaam. Baharia raia wa Tanzania, Mchama Maregesi Mongu amefariki dunia baada ya meli aliyokuwa akihudumu kushambuliwa kwa bomu katika Mfereji wa Hormuz Mei 3, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumanne Mei 5, 2026 na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Mongu alikuwa akifanya kazi katika meli ya kuvuta (tug boat) iitwayo Volans, yenye namba ya usajili ya Shirika la Kimataifa la Bahari (Imo) 929856, iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa mujibu wa Tasac, meli hiyo ilikuwa safarini kutoka UAE kuelekea Oman wakati iliposhambuliwa ilipokuwa ikivuka katika Mfereji wa Hormuz, eneo la kimkakati lililopo kati ya Iran na Oman.
Shirika hilo linaeleza masikitiko yake kufuatia tukio hilo na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.
“Tasac inaungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya kupoteza mpendwa wao,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyochapishwa katika ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram.
Aidha, Tasac inaeleza kuwa, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa za tukio hilo kwa lengo la kuwezesha kuurudisha mwili wa marehemu nchini mara utakapopatikana.
Katika hatua nyingine, Tasac imeungana na Imo kusisitiza umuhimu wa kulindwa kwa maisha ya mabaharia wanapokuwa baharini, hasa katika maeneo yanayohusu haki ya kupita kwa amani kama inavyolindwa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (Unclos).