Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sintofahamu Iran na Marekani, kigogo akitua kwa Putin

Muktasari:

  • Hali ya sintofahamu imeendelea kutawala katika mgogoro kati ya Iran na Marekani, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi akiwasili nchini Urusi kwa mazungumzo ya dharura na Rais Vladimir Putin

Dar es Salaam. Wakati mgogoro kati ya Iran na Marekani ukiingia siku ya 58, juhudi za kidiplomasia zimechukua sura mpya baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi kuwasili nchini Urusi kwa mazungumzo muhimu na Rais Vladimir Putin.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, Araghchi ametua katika mji wa St. Petersburg ambapo anatarajiwa pia kukutana na waziri mwenzake wa Russia, Sergey Lavrov katika kile kinachoonekana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tehran na Moscow wakati mazungumzo na Washington yakidorora.


Diplomasia yashika kasi, lakini matumaini ya amani yafifia

Ziara hiyo inafuatia mfululizo wa safari za haraka za Araghchi katika nchi za Pakistan na Oman, zilizolenga kutafuta suluhu ya kidiplomasia, kwa mujibu wa CNN.

Hata hivyo, juhudi hizo zinaonekana kukwama baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kusitisha mpango wa wajumbe wake kukutana na upande wa Iran.

Trump amesema mazungumzo yataendelea kwa njia ya simu, akisisitiza kuwa vita hiyo “itafikia mwisho hivi karibuni,” huku akitupa lawama kwa Iran kwa kukataa mazungumzo ya ana kwa ana.


Mgogoro wa Hormuz wazidi kuathiri uchumi wa dunia

Wakati mvutano ukiendelea, usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz umeendelea kudorora kwa kiwango kikubwa, hali inayochochea kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Taarifa zinaonesha idadi ya meli zinazopita katika njia hiyo muhimu ya biashara imeshuka kwa kiasi kikubwa tangu vita kuanza.

Iran imeonesha haitarejea katika hali ya awali ya usafirishaji katika eneo hilo, ikieleza kuwa kudhibiti njia hiyo kunaweza kuathiri hadi asilimia 25 ya uchumi wa dunia.

Katika hatua nyingine, jeshi la Marekani limedai kuzuia meli 38 kuingia au kutoka katika bandari za Iran ndani ya wiki mbili zilizopita, kama sehemu ya operesheni ya kuibana Tehran kiuchumi. Hatua hiyo imezua mjadala kuhusu athari zake kwa soko la nishati duniani.

Hata hivyo, wataalamu wamepinga madai ya Trump kuwa miundombinu ya mafuta ya Iran inaweza kulipuka ndani ya siku chache kutokana na kuzuiwa kwa usafirishaji, wakisema badala yake uzalishaji hupunguzwa pale hifadhi zinapojazwa.


Mapigano Lebanon yaendelea kutishia usitishaji vita

Wakati huohuo, hali ya usalama nchini Lebanon imeendelea kuwa tete licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano. Vikosi vya Israel na kundi la Hezbollah vimeripotiwa kuendeleza mashambulizi ya kulipizana, hali inayotishia kuvunjika kwa makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Marekani.

Ripoti zinaonesha maelfu ya watu wameathirika, huku vifo na majeruhi vikiongezeka tangu mapigano hayo yaanze.

Pamoja na ongezeko la juhudi za kidiplomasia, wachambuzi wanaonya kuwa tofauti kubwa kati ya pande husika zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa cha kufikia suluhu ya kudumu.

Kwa sasa, macho ya dunia yameelekezwa kwenye mkutano wa Vladimir Putin na Abbas Araghchi, ambao huenda ukaashiria mwelekeo mpya wa vita hiyo au kufungua dirisha jipya la mazungumzo ya amani.