Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Marekani yatishia vikwazo kwa wanunuzi mafuta ya Iran

Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent

Muktasari:

  • Marekani yaongeza presha kwa Iran kwa kuwatishia  vikwazo wanunuzi wa mafuta, hatua inayoongeza vita ya kiuchumi na kuongeza tishio la usalama wa nishati na uchumi wa dunia.

Dar es Salaam. Mvutano wa vita vya Mashariki ya Kati umeingia hatua mpya, baada ya Marekani kuanza mkakati mkali wa kiuchumi unaolenga kukata mapato ya mafuta ya Iran kwa kuwatishia vikwazo wanunuzi wake duniani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Reuters, Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent amesema wazi kuwa nchi yoyote au taasisi ya kifedha itakayobainika kununua mafuta ya Iran iko hatarini kuwekewa adhabu kali za kiuchumi.

“Tunaziambia nchi kwamba ikiwa unanunua mafuta ya Iran, au fedha za Iran zipo kwenye benki zako, sasa tuko tayari kuweka vikwazo vya kiwango cha juu,” amesema Bessent akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House.

Kauli hiyo inakuja wakati Marekani ikiendelea kutekeleza zuio la kijeshi baharini dhidi ya Iran, hatua iliyoanza Jumatatu wiki hii huku vita hiyo ikiingia wiki ya saba. Zuio hilo linalenga kudhibiti usafirishaji wa mafuta ya Iran katika masoko ya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Bessent ameeleza kuwa Marekani inaamini shinikizo hilo litaathiri moja kwa moja biashara ya mafuta kati ya Iran na China, ambayo kwa muda mrefu imekuwa mnunuzi mkuu.

“Tunaamini kuwa kwa zuio hili kutasitishwa kwa ununuzi wa China,” ameongeza, akionesha matarajio ya Taifa hilo kupunguza mapato ya Iran kupitia vikwazo katika soko lake la mafuta la kimataifa.

Mbali na hilo, Wizara ya Fedha ya Marekani imezitahadharisha benki mbili za China kuhusu uwezekano wa kuchukuliwa hatua kali endapo zitahusishwa na miamala ya fedha za Iran, hatua inayoashiria msimamo wa Taifa hilo kulinda matumizi ya Dola katika biashara ya bidhaa hiyo muhimu duniani.

“Tumeziandikia benki hizo na kuziambia kuwa tukithibitisha fedha za Iran zinapita kwenye akaunti zenu, tuko tayari kuweka vikwazo,” amesema Bessent, katika hatua inayoenda sambamba na uamuzi wa Marekani kuorodhesha zaidi ya watu 20, kampuni na meli zinazohusishwa na usafirishaji wa mafuta ya Iran, ikiwa ni sehemu ya kuvuruga miundombinu ya nishati ya taifa hilo.

Wakati huo huo, Marekani imesisitiza msimamo wake kuwa haitaongeza muda wa msamaha wa vikwazo uliotolewa Machi 20, ulioruhusu kwa muda mafuta ya Iran kuingia kwenye soko la dunia. Msamaha huo ambao Bessent amesema uliwezesha zaidi ya mapipa milioni 140 kufika sokoni ili kupunguza shinikizo la bei.

Hatua kama hiyo pia imechukuliwa kwa mafuta ya Urusi, ambapo msamaha wa awali umeachwa uishe bila kuongezwa, hali inayoashiria  mkakati mpana wa Marekani kuzikaba nchi pinzani katika sekta ya nishati, ambayo ni msingi wa uchumi kwa mataifa hayo.


Tahadhari ya Kiuchumi

Kwa mtazamo mpana, Wachumi wanadokeza kuwa hatua hizi zinaonesha wazi kuwa mzozo huu umevuka mipaka ya kijeshi na sasa umegeuka kuwa vita ya kiuchumi inayolenga mtiririko wa fedha na nishati duniani, wakionya kuwa kutokea madhara makubwa kwa uchumi wa dunia, ikiwa ni kuyumba kwa biashara ya kimataifa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei hasa katika nchi zinazoendelea.

Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema hatua hii inaashiria Marekani anataka kumaliza vita hivyo akisema; “ili kumaliza vita lazia ahakikishe iran haiwezi kufanya biashara yoyote.”

Kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, mchumi huyo anasema zinatakiwa kuendana na uhamo wa dunia kutoka kwenye utegemezi wa mafuta kwenda kwenye nishati safi kama gesi, nishati ya jua.

“Tunayo dira inayoweka kipaumbele kwenye nishati, huwezi kuwa na dira 2050 inayotegemea vita mashariki ya kati iishe, ikiisha itakuja nyingine, si hivi karibuni tu tulikuwa tunaongelea Ukraine?, sisi tuna fursa ya nishati ya jua, tuna nishati ya upepo, makaa mawe na jotoardhi (geothermal) na makaa ya mawe, tutumie fursa hizi tuhame huko,” anasisitiza Mtaalamu huyo wa uchumi huyo.

Mbali na kwamba nishati hizi zinalinda mazingira, anasema, pia haziathiriki zaidi na migogoro ya vita akikosoa alichokiita kudra za Mungu akisema “hii ya kusubiri kudra za Mungu, Trump aache vita haitatuisaidia, hata ikiisha hii ipo siku itatokea nyingine, hii itufanye kujua kuwa ipo siku tutakosa kabisa mafuta, tuhame kwenye utegezi wa nishati hii.”

Kwa sasa, macho na masikio ya dunia yanaendelea kuangazia Washington na Tehran ili kujua hatma ya mzozo huo na athri zake kwa mafuta, huku hatua hizi zikitarajiwa kuamua mwelekeo wa mgogoro ambao tayari umeshaanza kuacha alama kubwa katika uchumi wa kimataifa.