Prime
Mahakama yaanza kusikiliza kesi ya Tume ya Jaji Lila
Muktasari:
- Tume hiyo imeundwa na Rais Samia kuchunguza vitendo vya kijinai katika matukio ya vurugu za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, lakini wananchi wawili wameomba ruhusa ya mahakama kupinga uteuzi wa makamishna wake
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma leo, Jumatatu, Juni 8, 2026 imeanza kusikiliza shauri la maombi ya ruhusa ya kupinga uteuzi wa makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Tume hiyo maarufu Tume ya Jaji Lila, inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Lila imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, na mwenyekiti makamishna wake walitangazwa rasmi Mei 18, 2026.
Makamishna wa tume hiyo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Rais Samia ameunda tume kufuatia ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Awali, kufuatia matukio Jeshi la Polisi liliwakamata watu kadhaa maeneo tofauti nchini na kuwafungua kesi za uhaini lakini baadaye wakaachiwa.
Kisha Rais aliunda Tume ya Jaji Chande iliyowasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026, ambayo katika hotuba yake ya kukabidhi ripoti hiyo ilielezwa watu 518 waliuawa na wengine kujeruhiwa, idadi ambayo alisema inaweza kuwa zaidi, ndipo baadaye akaunda tume ya Jaji Lila.
Hata hivyo, kabla tume hiyo haijaapishwa kuanza jukumu hilo, mwanaharakati Buberwa Buberwa na mwenzake Joseph Mabugo, wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, walikwenda mahakamani kuhoji uhalali wake.
Buberwa na Mabugo wamefungua shauri dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), na mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Lila na wajumbe wake hao watatu, Mjemmas, Bawazir na Sumari (mjibu maombi wa pili mpaka wa tano mtawalia).
Katika shauri hilo waombaji hao wanaomba ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya mahakama kuiomba itengue uamuzi huo wa Rais Samia wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo, na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.
Mahakama imeanza kusikiliza shauri hilo kwa kuanzia na hoja za waombaji.
Kiongozi wa jopo la mawakili waombaji, Mpoki, akisaidiana na wakili Mwasipu, ameieleza Mahakama katika hatua hii inapaswa kuangalia kama waombaji wamekidhi vigezo vitatu muhimu vya kupewa ruhusa ya kufungua shauri la msingi la kupinga uteuzi wa makamishna hao kama vilivyokwisha kuwekwa na Mahakama.
Huku akirejea uamuzi wa kesi mbalimbali ikiwamo maarufu ya Emma Bayo dhidi ya Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana na wenzake, amevitaja ni mwombaji kuonesha kuwa kuna hoja inayohitaji kujadiliwa na Mahakama.
Vingine amevitaja kuwa ni mwombaji kuonesha kuwa ana masilahi katika jambo au uamuzi unaolalamikiwa na mwisho maombi kufunguliwa ndani ya muda, yaani miezi sita tangu kutolewa kwa uamuzi au kufanyika kwa jambo linalolalamikiwa.
Huku akirejea aya mbalimbali za kiapo hati ya maelezo ya waombaji na hati ya madai, Wakili Mpoki ameieleza Mahakama kuwa waombaji wamekidhi vigezo hivyo vyote.
Akifafanua zaidi Wakili Mpoki ameeleza kuwa waombaji wameeleza kuwa katika uteuzi wa makamishna hao, Rais ametenda nje ya mamlaka yake kisheria, kwamba uamuzi huo hauna maana si halali na unakiuka Katiba.
Pia ameeleza kuwa waombaji kama raia wa Tanzania ni wahanga wa matukio ya uchaguzi mkuu na shauri hilo limefunguliwa ndani ya muda kwani uteuzi wa makamishna hao ulifanyika Mei 18, 2026 (mpaka sasa hata mwezi mmoja haujaisha).
"Kwa hiyo mheshimiwa Jaji ni rai yetu kwamba waombaji wamekidhi vigezo vyote, hivyo wanastahili kupewa ruhusa kufungua shauri la mapitio ya mahakama kuhoji uteuzi huo wa makamishna hao wa tume hiyo," amesema Wakili Mpoki akihitimisha hoja za waombaji.
Baada ya upande wa waombaji kuhitimisha hoja zao sasa upande wa wajibu maombi utaanza kujibu hoja hizo.
Sababu za kuomba kuipinga tume hiyo
Katika hati ya maelezo na kiapo chao cha pamoja waombaji hao wanadai kuwa kwa Mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchunguzi sura ya 32(R:E 2023) Rais hana mamlaka ya kuunda tume nyingine baada ya Tume ya Jaji Chande kutoa ripoti yake.
Wanabainisha kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 21(1) (a) na (b) Rais baada ya kupokea na kuisoma ripoti ya Jaji Chande alipaswa kuelekeza wale waliotajwa katika ripoti hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.
Pia wanadai kuwa Rais hana mamlaka ya kuunda Tume ya kuchunguza matukio ya kijinai bali hilo ni jukumu la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Mashtaka Sura ya 430 ( Marejeo ya mwaka 2023) kuratibu na kusimamia upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai bila kujali sheria nyingine zozote nchini.
Hivyo wanadai kuwa kama Rais baada ya kusoma ripoti ya Jaji Chande anaona kuna haja ya kuchunguza zaidi anatakiwa kumuagiza DPP kuliagiza Jeshi la Polisi kupeleleza zaidi.
Vilevile wanadai kuwa kitendo cha Rais kuunda tume kuchunguza matukio ambayo aliamuru watuhumiwa waachiwe bila mahakama kutoa uamuzi wowote kuhusu uhusika wao, unakosa mantiki kisheria na ni kitendo cha kibaguzi kinachopingana na ibara ya 13 (1) ya Katiba ya Nchi.