Shauri la Tume ya Jaji Lila kusikilizwa leo
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Lila.
Muktasari:
- Tume hiyo imeundwa na Rais Samia kuchunguza vitendo vya kijinai kufuatia matukio ya vurugu za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma leo Jumatatu, Juni 8, 2026 inasikiliza shauri la maombi ya ruhusa ya kupinga Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Tume hiyo, maarufu Tume ya Jaji Lila, inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Lila imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na mwenyekiti na wajumbe wake walitangazwa rasmi Mei 18, 2026.
Wajumbe wa tume hiyo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Rais Samia aliunda Tume hiyo kufuatia ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Hata hivyo, kabla tume hiyo haijaapishwa kuanza jukumu hilo, mwanaharakati Buberwa Buberwa na mwenzake Joseph Mabugo, wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, wamekwenda mahakamani kuhoji uhalali wake.
Buberwa na Mabugo wamefungua shauri dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Lila na wajumbe wake hao watatu, Mjemmas, Bawazir na Sumari (mjibu maombi wa pili mpaka wa tano mtawalia).
Katika shauri hilo waombaji hao wanaomba ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya Mahakama, kuiomba itengue uamuzi huo wa Rais Samia kuunda tume hiyo na uteuzi wa wajumbe wake, pamoja na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.
Shauri hilo limepangwa kusikilizwa leo Jumatatu Juni 8,2026 na Jaji Augustine Rwizile katika hatua hii ya awali, ambapo Mahakama itaangalia na kuamua kama waombaji wanastahili kuruhusiwa kufungua shauri rasmi kuipinga tume hiyo au la.
Awali, shauri hilo lilipangwa kusikilizwa Juni Mosi, lakini liliahirishwa mpaka leo kutokana na wajibu maombi wa kwanza mpaka wa tano (mwenyekiti na wajumbe hao kutofika mahakamani.
Wakili wa Serikali aliyemwakilisha AG, Stanley Kalokola aliieleza Mahakama hawawakilishi wajumbe hao kwa kuwa hakuwa amepata maelekezo ya kuwawakilisha kutoka Ofisi ya AG.
Hivyo mawakili wa waombaji waliomba na mahakama ikaridhie wajumbe hao wa tume hiyo waitwe kwa njia ya tangazo kupitia Gazeti Mwananchi, wafike leo mahakamani.
Katika hati ya maelezo na kiapo chao cha pamoja waombaji hao wanadai kwa Mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchunguzi sura ya 32 (R:E 2023) Rais hana Mamlaka ya kuunda Tume nyingine baada ya Tume ya Jaji Chande kutoa ripoti yake.
Wanabainisha kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 21(1) (a) na (b) Rais kama ataona kuna haja ya kuchunguza zaidi baada ya kusoma ripoti ya Jaji Chande anatakiwa kumuagiza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuliagiza Jeshi la Polisi kupeleleza zaidi.
Pia, wanadai mujibu wa kifungu hicho kama ripoti inajitosheleza waliotajwa wachukuliwe hatua za Kisheria.
Vilevile wanadai Rais hana Mamlaka ya kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio ya Kijinai kwa sababu DPP ndiye mtu pekee mwenye jukumu hilo kikatiba na kisheria.
Wamesisitiza Sheria ya Huduma Mashtaka Sura ya 430 ( Marejeo ya mwaka 2023) inampa DPP mamlaka ya kipekee kufanya jukumu hilo bila kujali Sheria nyingine zozote za nchi hii.
Pia wanaeleza DPP amepewa majukumu ya kikatiba na kisheria kuratibu na kusimamia upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai kasoro makosa yanayohusu mahakama ya kijeshi.
Endelea kufuatilia Mwananchi