Fomu ya urais DR Congo Sh150 milioni

Kinshasa. Wakati wagombea urais wa Tanzania wakitoa Sh5 milioni kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, kwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wagombea urais wanatakiwa kuonyesha risiti ya malipo ya faranga za Congo milioni 160, sawa na zaidi ya Sh150.3 milioni kama ada zisizorejeshwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI).

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kiasi hicho kimepunguzwa kutoka dola 100,000 sawa na zaidi ya Sh250.5 milioni katika uchaguzi uliopita wa 2018.

Mpaka sasa wagombea 25 wameshajitokeza akiwamo Rais wa sasa Felix Tshisekedi akipambana na mpinzani wake wa karibu, Martin Fayulu ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2018 ilidaiwa alishinda ingawa si aliyetangazwa.

Wagombea wengine wakubwa ni pamoja na gavana wa zamani wa jimbo lenye utajiri wa madini la Katanga, Moise Katumbi ambaye ni mmiliki wa timu ya Soka ya TP Mazembe na Waziri Mkuu mstaafu, Dk Denis Mukwege aliyepata tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018 kwa alivyojitolea kufanya kazi na waathiriwa wa unyanyasaji wa ngono.

Pia wapo mawaziri wakuu wa zamani, Adolphe Muzito na Augustin Matata Ponyo, Mbunge Delly Sesanga, mwanaharakati Floribert Anzuluni na Constant Mutamba ambaye yuko karibu na kambi ya Rais mstaafu, Joseph Kabila.

Wamo pia wanawake wawili ambao ni Marie-Josée Ifoku Mputa, aliyekuwa mgombea katika uchaguzi wa urais wa Desemba 2018 na Joëlle Bile.

Wengine ni Noel Tshiani, Seth Kikuni, Radjabho Tebabho Soborabo, Theodore Ngoy, Adolphe Muzito, Tony Bolamba, Jean-Claude Baende, Delly Sesanga, Franck Diongo, Constant Mutamba, Justin Mudekereza, Georges Buse Falay, Rex Kazadi, Abraham Ngalasi, Nkema Liloo Bokonzi, Floribert Anzuluni, Patrice Mwamba, Andre Masalu na Enoch Ngila.


Wapiga kura milioni 44

Kwa mujibu wa kalenda iliyotolewa na CENI, uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Desemba 20, 2023 ukihusisha wapiga kura zaidi ya milioni 44 waliojiandikisha katika nchi hiyo yenye zaidi ya watu milioni 100.

Uchaguzi huo utahusisha nafasi ya urais, nafasi 500 za wabunge, wajumbe wa mabaraza ya majimbo 26 na kwa mabadiliko ya katiba ya sasa kwa mara ya kwanza kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe 300 wa mabaraza ya manispaa.

Kwa mujibu wa CENI, kuna wagombea 25,832 wa ubunge, 44,110 wa majimbo na 31,234 wa mabaraza ya manispaa.

Nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa rasilimali, huku inakabiliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, umasikini na rushwa.


Kampeni

Kampeni za uchaguzi zilianza Jumapili iliyopita, ambapo Rais Tshisekedi anayewania muhula wa pili amekuwa akitumia matukio ya Serikali kujinadi, huku wanaomuunga mkono wakimsifu kwa kazi zake.

Katika mikutano ya wagombea, maelfu ya wananchi wanafurika huku mitaa ikiwa imepambwa na mabango ya wagombea.

Katika ufunguzi huo, Rais Tshisekedi alifanya mkutano katika uwanja maarufu wa michezo wa Martyrs jijini Kinshasa uliofurika watu zaidi ya 80,000 licha ya mvua kunyesha.

“Anasema ukweli na ndiye pekee anayenaisha vitu,” alisema ofisa wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) cha Rais Tshisekedi.

Kwa upande wake Martin Fayulu, ambaye amekuwa akidai kuwa aliporwa ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2018 alifungua kampeni zake karibu na jiji la Kinshasa.

“Muda umefika kuibadilisha Congo,” aliwaambia wafuasi wake katika mkutano huo.

Kwa nini Rais Tshisekedi anatabiriwa ushindi?

Rais Tshisekedi anapewa nafasi ya kushinda, pengine kwa kuwa kuna awamu moja tu ya kupiga kura.

Hiyo ni kutokana na kubadilishwa kwa ibara ya 71 ya Katiba inayohusiana na mbinu ya upigaji kura wa urais na kupitishwa kwa sheria mpya kabla ya uchaguzi wa urais wa 2011, Rais wa Jamhuri sasa anachaguliwa kwa kura nyingi zilizopigwa.

Sababu nyingine ni wapinzani kutounganisha nguvu. Hivi karibuni wawakilishi wa makundi makubwa matano ya upinzani walikutana nchini Afrika Kusini kujadili mpango wa kusimamisha mgombea mmoja. Hata hivyo, Martin Fayulu anayepewa nafasi kubwa hakujitokeza.

Katika kujadili kusimamisha mgombea mmoja, Waziri Mkuu wa zamani Matata Ponyo amejitoa kugombea urais na kumwachia Moise Katumbi.

“Hali inaonyesha umuhimu wa kuwa na mgombea mmoja wa upinzani,” alisema Matata katika ujumbe aliouweka mtandao wa Facebook, akiilamu Serikali kwa kuanza mpango aliouita wa “wizi mkubwa wa kura.”


CENI yatiliwa shaka

Miongoni mwa changamoto zinazoikabili CENI ni jinsi ya kupangilia upigaji kura nchi nzima yenye ukubwa wa kilometa za mraba 2.3 milioni ikiwa na miundombinu inayolalamikiwa (mibovu).

Mchambuzi wa masuala ya siasa wa taasisi ya utafiti ya Ebuteli, Tresor Kibangula, alisema inavyoonekana bado masuala ya kiufundi hayajakamilika hivyo uchaguzi unaweza usifanyike kwa wakati kama inavyotarajiwa.

Kwa upande wake Sylvain Lesoye ambaye ni mchungaji jijini Kinshasa alisema, CENI haionyeshi uhakika wa uchaguzi huo akitoa mfano vitambulisho vya kupigia kura alivyosema vina picha na saini hafifu.

“CENI inajua changamoto inazokabiliwa nazo na uwezo wake,” alisema.

Naye Jean-Luc Kong alisema kinachotishia zaidi uchaguzi huo ni mgogoro unaoendelea Mashariki ya nchi hiyo.

Katika eneo hilo la Mashariki kumekuwa na mapigano kwa miongo mitatu na mgogoro umechochewa zaidi na kuibuka kwa kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda likishikilia eneo kubwa la jimbo la Kivu Kaskazini.

Nchi kadhaa zikiwemo Marekani na Ufaransa zimesisitiza kuwa Rwanda ndiyo inalisaidia kundi la M23, japo Kigali imekuwa ikikanusha madai hayo.

Mapigano hayo yanauweka uchaguzi huo katika majaribu katika eneo hilo, lakini huenda mchakato huo ukaathirika endapo waasisi watateka makao makuu ya mji wa Goma.

“M23 haitachukua mji wa Goma,” amesisistiza Rais Tshisekedi, akisema kipaumbele chake ni kumaliza mapigano pamoja na kuimarisha uchumi.

Baadhi ya wapiga kura waliozungumza na France 24 walikuwa na mchanganyiko wa maoni, akiwamo Eunice, mwanafunzi wa gjiografia (20) aliyesema, “ninayo furaha kupiga kura kwa mara ya kwanza.” alisema

Lakini kwa Ezechiel (240 anayesoma Tehama alisema haoni kama kutakuwa na tofauti

“Kutakuwa na wizi kama mwaka 2018, sitakwenda kupoteza muda wangu kupiga kura halafu niliyemchagua asitangazwe mshindi kama akishinda.” alisema