Tshisekedi: Magufuli alikuwa mtetezi wa uhuru wa kiuchumi

Tshisekedi: Magufuli alikuwa mtetezi wa uhuru wa kiuchumi

Muktasari:

  • Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi amesema Hayati John Magufuli alikuwa mpiganaji na mzalendo, mtetezi mkuu wa uhuru wa utamaduni na kiuchumi barani Afrika.

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi amesema Hayati John Magufuli alikuwa mpiganaji na mzalendo, mtetezi mkuu wa uhuru wa utamaduni na kiuchumi barani Afrika.

Tshisekedi ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 22, 2020 katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma wakati wa kuaga mwili wa Magufuli.

Amesema kuondoka kwake kumetikisa Bara la Afrika kwa kuwa ni mwanasiasa mkongwe aliyeboresha maisha na kujali wananchi wake, kutetea na kuendeleza uchumi.

“Tutabaki na kumbukumbu ya mtu mpiganaji na mzalendo, siyo tu kwa maslahi mapana ya Tanzania bali pia kwa umoja wa Afrika, mtetezi mkuu wa uhuru wa kitamaduni na kiuchumi wa bara la Afrika, aliyekuwa analenga kutimiza ndoto ya waasisi wa mataifa yetu uliolenga kuleta umoja kwa Afrika na baina ya mataifa yetu.”

“Aliyekuwa anatamani kuona maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanayotekelezwa na Waafrika kwa niaba ya Waafrika na Watanzania kwa ujumla. Rais wa Tanzania wimbi lililosababishwa na kifo cha Magufuli haitakiwi kamwe kupunguza dhamira yenu na nia yenu kuendeleza dira na dhima aliyokuwa nayo Magufuli,” amesema Tshisekedi.

Katika maelezo yake rais huyo amesema, “hii ni fursa kwenu kuja pamoja na kutimiza ndoto inayolenga kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.  tunaoongelea dhamira na dhima yake ninapenda kutaja kati ya mengi tu mapambano aliyoyaendesha dhidi ya ubadhirifu wa mali, fedha na rushwa ambayo ni kansa iliyokuwa inatafuna na kuchelewesha maendeleo ya bara la Afrika.”