Mjadala kiapo cha mawaziri baada ya Rais kuapishwa
Muktasari:
- Yadai Rais mpya anaposhika madaraka anateua waziri mkuu mpya, mawaziri, Mwigulu aipinga, wanasheria watofautiana.
Dar es Salaam. Wakati Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kikitoa maoni yake kisheria kuhusu uundwaji wa Serikali kufuatia kifo cha Rais John Magufuli, Waziri wa Sheria na Katiba, Mwigulu Nchemba amepinga mtazamo huo akisema hakuna mkanganyiko wowote wa Katiba.
Mwigulu pia amepinga ushauri wa TLS wa kutaka liundwe baraza jipya la mawaziri akisema tayari baraza lipo, akawataka wanasheria hao kuacha kwanza msiba wa Rais Magufuli upite.
Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.
Kufuatia kifo hicho, aliyekuwa makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliapishwa Machi 19 kushika wadhifa wa urais kwa mujibu wa Katiba.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, TLS imesema baada ya Rais Samia kuapishwa anatakiwa kuteua Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na kuunda upya Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa Katiba.
Hata hivyo, Mwigulu katika andiko lake alilolitoa katika mtandao wa Instagram akijibu taarifa hiyo ya TLS, amesema kwa tamaduni za Kiafrika, Kitanzania na misingi ya utu, haoni kama ni jambo jema sana kuanza kujadili mgawanyo wa madaraka kabla ya kumzika Rais Magufuli.
Alipoulizwa kwa simu jana sababu ya kutoa mwongozo huo sasa, Rais wa TLS, Dk Rugemeleza Nshala alisema ni kutokana na upya wa tukio la kufiwa na Rais aliyekuwa madarakani.
“Nchi yetu haina uzoefu nalo, lilitokea Zanzibar mwaka 1972 na mwaka 1984 baada ya Rais Aboud Jumbe kuondoka madarakani. Kwa hiyo tunatoa ushauri katika kumsaidia Rais katika kipindi hiki kigumu,” alisema Dk Nshala.
Mwongozo wa TLS
Katika mwongozo huo, uliosainiwa na Dk Nshala mwenyewe, TLS imesema baada ya Rais kuapishwa, kinachofanyika baada ya hapo ni kuteua makamu mwingine wa Rais.
“Mteule huyu lazima athibitishwe na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia 50 ya wabunge wote wa Bunge hilo. “Makamu wa Rais mteuliwa kwa mujibu wa Ibara ya 30 (5) naye anatakiwa kuapishwa na Jaji Mkuu, kama ilivyo kwa Rais na Makamu wake wanaopatikana wakati wa uchaguzi mkuu kwa mujibu wa ibara za 42(5) na 49; Au aliyeteuliwa na kuthibitishwa kuwa Makamu wa Rais kwa mujibu wa ibara ya 50(4).”
Kuhusu Baraza la Mawaziri, TLS imetaja ibara ya 51(2) ikisema Rais atamteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi Bungeni kuwa Waziri Mkuu.
Dk Nshala alisema kutokana na ibara ya 37(5), Rais anatakiwa kumteua Waziri Mkuu ndani ya siku 14 baada ya yeye kuwa Rais.
“Ibara ya 51(1) ya Katiba inataka Waziri Mkuu aliyeteuliwa na Rais kabla ya kushika madaraka yake kuapa mbele ya Rais kiapo kilichowekwa na Bunge.
Pia alisema baada ya Rais kumteua Waziri Mkuu, akathibitishwa na Bunge kisha akamuapisha, ndipo anatakiwa kuteua mawaziri wengine na naibu mawaziri kwa mujibu wa Ibara ya 55(1).
“Ibara ya 56 ya Katiba inatamka waziri au naibu waziri hatashika madaraka yake mpaka awe ameapa kwanza mbele ya Rais.
Alifafanua kuwa kiapo hicho lazima kifanywe kwa Rais aliyepo na si yule aliyeondoka madarakani kwani kiapo kwa Rais mmoja hakihamishwi kwa Rais mwingine.
Majibu ya Mwigulu
Lakini akijibu hoja hizo, Waziri Mwigulu ameikosoa TLS huku naye akitaja vifungu vya Katiba.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 42(5) kuna watu wa aina mbili wanaweza kuwa Rais. Moja, Rais mteule ambaye anatokana na Ibara ya 42(1). Mbili, mtu anayeshika kiti cha Rais ambaye anatokana na ibara ya 37(5) na 50(2)(d) ambaye ni Makamu wa Rais,” ameandika.
Amesema katika mazingira ya sasa Makamu wa Rais, baada ya kifo cha Rais, anakuwa Kaimu Rais na baadaye anaapa na kuwa Rais.
Pia amekanusha kuundwa kwa Baraza jipya la mawaziri akisema ibara ya 57(2)(f) ya Katiba haitumiki katika mazingira ya sasa kwani Rais mteule anapatikana kutokana na uchaguzi.
“Kwa mujibu wa sheria, Mheshimiwa Rais alitakiwa kutoa taarifa hii kwenye Baraza la Mawaziri baada ya kuapa na alifanya hivyo, maana yake Baraza lipo...Kwa mujibu wa katiba, Rais anaruhusiwa kuvunja Baraza muda wowote na kupanga atakavyo, hata hivyo sio kwa mazingira ya kuapa kwake,” ameandika.