Jafo aeleza maagizo ya mwisho aliyopewa na Magufuli
Muktasari:
- Mawaziri walioko Serikali iliyoongozwa na Rais John Magufuli jana walisimulia walivyofanya naye kazi, huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo akieleza maagizo ya mwisho aliyopewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu akizungumzia miaka mitano ya kuwa pamoja naye.
Dar es Salaam. Mawaziri walioko Serikali iliyoongozwa na Rais John Magufuli jana walisimulia walivyofanya naye kazi, huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo akieleza maagizo ya mwisho aliyopewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu akizungumzia miaka mitano ya kuwa pamoja naye.
Jafo alisema usimamizi wa kodi za majengo na ushuru wa mabango kwa ufanisi ni miongoni mwa maelekezo aliyopewa na Magufuli kabla ya kifo chake.
Jafo, mbunge wa Kisarawe alieleza hayo jana wakati wa shughuli ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Magufuli katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Alisema yapo mambo mengi aliyozungumza na Magufuli kabla ya kufariki, akisema kifo chake ni msiba mkubwa, huku akikumbushia namna kiongozi huyo alivyosaidia kuboresha miundombinu, ikiwamo vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Jafo alisema Hayati Magufuli aliamua ukusanyaji wa ushuru wa mabango na majengo kurudishwa Tamisemi kutoka Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA), ili kuleta ufanisi katika eneo hilo.
“Aliamini Tamisemi inaweza kufanya hivi ikiongozwa na mimi nikishirikiana na watendaji wengine. Tulikuwa tumeshamaliza uhakiki wa majengo na Machi 23 tulikuwa tuanze kampeni za ukusanyaji wa kodi.
“Hata hivyo, mchakato huo tumeusogeza mbele kidogo, lakini tutafanya kabla ya Juni. Tunawaomba Watanzania watupe ushirikiano tutakapoanza kampeni ya ukusanyaji wa kodi ya majengo ili kumpa heshima Magufuli,” alisema Jafo.
Wakati Jafo akieleza hayo, WaziriUmmy amesimulia jinsi atakavyomkumbuka kiongozi huyo hasa katika kukabiliana na ugonjwa wa corona, wakati akiwa Waziri wa Afya.
Alisema katika miaka mitano aliyofanya kazi na Rais Magufuli akiwa Waziri wa Afya, alijifunza kwamba alikuwa mwalimu mzuri aliyewafundisha kazi na alitamani kuona matokeo ya kile wanachokifanya. Alisema hata kwenye ugonjwa wa corona aliweka msimamo na kuwatoa hofu Watanzania ili waendelee na shughuli zao za kila siku bila woga.
“Binafsi nimefanya kazi kwa ukaribu na Rais John Magufuli kuanzia mwaka 2015 aliponiteua kuwa Waziri wa Afya na hadi sasa aliponiteua katika wizara nyingine. Rais Magufuli amenifundisha mambo makubwa matatu; kwanza kuchapa kazi, uzalendo wa kuipenda nchi na Watanzania na ujasiri na kujiamini,” alisema Ummy.
Alisema Rais Magufuli alikuwa anapenda viongozi wafanye kazi na matokeo yaonekane ambayo yanasaidia kutatua kero za Watanzania wa hali ya chini.
Alisema kipindi cha Rais Magufuli kimemjenga kama kiongozi, akitolea mfano kwenye mapambano dhidi ya corona kuvuka changamoto zote zilizojitokeza kwa sababu nyuma yake alikuwa anapewa miongozo.
Ummy alisema anamtakia kila la kheri na apumzike salama kwa kuwa kazi alizofanya zinaonekana, hususan katika sekta ya afya, kwani amefanya makubwa ikiwamo kujenga vituo vya afya zaidi ya 400 ndani ya miaka yake mitano.
“Hospitali za wilaya zaidi ya 70, hospitali za rufaa za mikoa 10, hospitali za rufaa za kanda tatu,” alisema waziri huyo.
Alisema Rais Magufuli aliwahi kumpigia simu akimweleza hapendi kuona Watanzania wakienda kupata matibabu nje ya nchi, hivyo alimtaka kuboresha hospitali za ndani kila kona ya nchi.
“Baada ya kupata ujumbe huo nikakaa na wataalamu wa afya kuanza kutengeneza mipango ya kuanzisha huduma za matibabu ya kibingwa, uzuri Magufuli ukiwa na jambo zuri anakupa fedha.
“Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tulianza upandikizaji wa figo, sasa tunahudumia wagonjwa zaidi ya 70 kuanzia mwaka 2017. Tunaona kazi nzuri kwenye Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) asilimia 60 ya wagonjwa waliokuwa wakienda kutibiwa nje sasa wanapata huduma ndani,” alisema.
Wakati huohuo, mwanamke mmoja, Magretha Anyango ametoka kaunti ya Kisumu nchini Kenya, kuja Dar es Salaam kuaga mwili wa Hayati Magufuli.
Anyango alisema amekuja Tanzania kumuaga kiongozi huyo ambaye anapendwa sana Kisumu kwa sababu amekuwa akitetea wananchi masikini, hasa wanawake ambao wamekuwa wakinyanyaswa katika nchi mbalimbali.
“Tunampenda sana Rais Magufuli, kule kwetu tunamwita King Solomon kwa sababu amekuwa rafiki wa maskini na mtetezi wa wanyonge. Ni kiongozi pekee anayeangalia maslahi ya masikini,” alisema Anyango. Aliwataka viongozi waliobaki wafuate nyayo zake hasa katika kuwasaidia wananchi masikini wanaohitaji huruma ya viongozi wao.
Imeandikwa na Peter Elias, Bakari Kiango na Fortune Francis.