Utaratibu kuaga mwili wa Magufuli wabadilishwa

Utaratibu kuaga mwili wa Magufuli wabadilishwa

Muktasari:

  • Viongozi mbalimbali wameanza kuingia katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwa ajili ya mapokezi ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli huku utaratibu ukibadilishwa.

Dodoma. Viongozi mbalimbali wameanza kuingia katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwa ajili ya mapokezi ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli huku utaratibu ukibadilishwa.

Waliofika mapema ni mawaziri wakuu wastaafu Jaji Joseph Warioba, Frederick Sumaye, Mizengo Pinda na John Malecela ambao wote wameambatana na wake zao.

Waziri wa kwanza kufika uwanjani ni Profesa Palamagamba Kabudi na makatibu wakuu wa wizara mbalimbali huku bendera za mataifa mengine zimeanza kupandishwa.

Wakati huo utaratibu wa kuaga mwili wa Magufuli umebadilishwa ambapo sasa wananchi hawatapita mbele ya jeneza lenye mwili wake badala yake walio ndani ya uwanja huo wataaga mwili ukiwa kwenye gari na utazungushwa uwanjani hapo mara tano ukiwa katika gari maalum.

Msherekeshaji ametangaza kuwa watu walioko nje warudi majumbani wakasubiri kujipanga katika mitaa iliyotangazwa ambako mwili utapitishwa.

#LIVE: Kuagwa hayati John Magufuli Kitaifa Dodoma