G7 wabariki makubaliano Marekani na Iran, wampa maagizo Trump kuhusu Russia
Viongozi wa G7 wakiongozwa na Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Japan wakutana Evian-les-Bains kujadili masuala ya usalama wa dunia na uchumi, huku mgogoro wa Ukraine na ushindani wa kimataifa ukitawala mjadala.
Muktasari:
- Viongozi wa G7 wameunga mkono makubaliano ya Marekani na Iran kuhusu mpango wa kumaliza vita, huku wakimtaka Rais Donald Trump kuiunga mkono Ukraine na kuongeza vikwazo dhidi ya Russia.
Dar es Salaam. Mataifa saba yenye uchumi mkubwa duniani (G7) yamebariki makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran.
Mwisho mwa wiki iliyopita, Marekani na Iran walitangaza kufikiwa mwafaka wa kusitisha mapigano baada ya kukubaliana mambo kadhaa yakiwemo kufunguliwa kwa mfereji wa Hormuz, kurejesha mali za Iran zinazoshikiliwa huku Iran ikitakiwa kuacha kuzalisha silaha za nyuklia.
Pamoja na kuridhia makubaliano hayo, G7 pia wamemtaka Rais Donald Trump wa Marekani kutumia ushawishi wake kuiunga mkono Ukraine na kuongeza mashinikizo dhidi ya Urusi ili kuifanikisha amani ya kudumu Ulaya.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron wakati akisalimiana na Rais wa Marekani, Donald Trump walipokutana katika Mkutano wa G7 nchini Ufaransa. Picha na Mtandao
Tamko la pamoja la mataifa hayo tajiri zaidi ulimwenguni limelotolewa leo Jumatano June 17, 2026 katika mkutano wa kilele wa G7 mjini Evian-les-Bains, Ufaransa, limekuja baada ya siku kadhaa za mvutano mkubwa ndani ya kundi hilo kuhusu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Mvutano huo umegusia pia kwa kuwango kikubwa kuhusu mustakabali wa vita vya Urusi na Ukraine.
Katika tamko hilo, viongozi hao wamesema wanakaribisha makubaliano yanayolenga kurejesha amani.
“Tunayaunga mkono makubaliano hayo na tuko tayari kuchangia utekelezaji wake,” limesema tamko hilo, huku G7 wakisisitiza pia Iran haitapaswa kumiliki silaha za nyuklia.
Hata hivyo, licha ya kumpa ushindi wa kidiplomasia Trump kuhusu Iran, viongozi hao wameigeukia Marekani katika suala la Ukraine.
Wakiweka wazi mpango wa Ulaya kusimama bega kwa bega na Ukraine katika kulinda uhuru, mamlaka na mipaka yake, wameahidi kuongeza usambazaji wa mifumo ya ulinzi wa anga, makombora ya kuzuia mashambulizi na uwezo wa mashambulizi ya masafa marefu.
Katika hatua hiyo, wamemwomba Rais Trump kuunga mkono juhudi hizo katika kusaidia kumaliza mzozo huo uliodumu kwa miaka kadhaa.
Kwa upande wa Russia, viongozi hao wamekubaliana kuongeza shinikizo kwa uchumi wa vita wa taifa hilo kupitia vikwazo vipya, vikiwamo vinavyolenga sekta za mafuta na gesi, wakieleza kuwa huu ni wakati mwafaka wa kuongeza mbinyo huo baada ya kufunguliwa tena kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz kufuatia makubaliano ya Iran.
Kauli hiyo inaendana na msimamo uliotangazwa mapema na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron katika mazungumzo yake na Chombo cha habari cha Tf1 alipomshawishi Trump asilegeze msimamo dhidi ya Russia.
“Tunaitaka Marekani iseme, tuko pamoja nanyi, tutaendelea kuisaidia Ukraine, na tutazidisha shinikizo dhidi ya Urusi ili kupata majadiliano yenye maana’,” amesema Macron katika mahojiano hayo kabla ya tamko la mwisho la G7.
Kwa tamko lao, G7 wanaashiria hatua ya kusawazisha maslahi mawili makubwa ya dunia kwa wakati mmoja, kwanza kuunga mkono mpango wa Trump wa kupunguza mvutano wa Mashariki ya Kati kupitia makubaliano na Iran, pili kuendeleza mshikamano wa Marekani na Ulaya katika kuendeleza msaada kwa Ukraine na kuibana Russia.
Aidha, mkutano huo umeonyesha licha ya tofauti zilizojitokeza kati ya Trump na washirika wake wa Ulaya, mataifa hayo bado yanaona ushirikiano wao kuwa nguzo muhimu ya usalama wa kimataifa.
Kwa upande wake, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky aliyealikwa kwenye mkutano huo amepongeza maazimio hayo, akitaja ni hatua muhimu itakayoilazimisha Russia kuketi kwenye meza ya mazungumzo kumaliza vita hivyo.
Mktano wa G7 mwaka huu umejumuisha mataifa saba yenye uchumi mkubwa duniani yakiwemo Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza pamoja na Canada na Japan.
Mbali na hayo, zimealikwa pia Kenya, Brazil, Misri, India, Korea Kusini, Qatar, Syria na Ukraine.