Gari la Odinga lapigwa risasi, maandamano kuendelea Jumatatu

Raila Odinga akiwa katika maandamano.

Muktasari:

  • Kufutia maandamano nchini Kenya, gari la kiongozi wa upinzani, Raila Odinga limepigwa risasi, huku akidai lilikuwa ni jaribio la kumtoa uhai.

Nairobi. Gari la kiongozi wa Azimio la Umoja nchini Kenya, Raila Odinga limepigwa risasi na maofisa wa polisi katika maandamano ya upinzani dhidi ya serikali nchini humo jana Alhamisi.

Odinga amesema kulikuwa na njama ya kumtoa uhai akisema risasi saba zilipigwa kwenye gari lake.

"Gari langu lilipigwa risasi saba na ukiangalia risasi zenyewe zilikuwa zinanilenga mimi. Watu hawa wamekuwa wakitutishia lakini kinachovunja moyo zaidi ni kuwa marafiki wa taifa hili hawasaidii.

Tazama taarifa zinazotolewa na baadhi ya mabalozi walioko humu nchini utafikiri kuwa wanaishi katika taifa tofauti. Wanachokifanya ni kuzidisha moto kwenye mzozo uliyopo," Raila alisema.

Raila amesema hatakubali polisi kuendelea kuwakabili wafuasi wake kama ambavyo wanafanya wakati wa maandamano ambayo yalinza Machi 20.

Hayo yanajiri kutokana na hali iliyoshuhudiwa Alhamisi Machi 30 wakati wa maandamano katika mitaa ya Mukuru kwa Njenga, Pipeline na Imara Daima. Hali iligeuka na kuwa mbaya wakati polisi wakikabili waandamanaji wakitumia nguvu na fujo.

"Saa hii sasa wanawa piga risasi na kuwaua Wakenya. Hili lazima likome Jumatatu. Muda wao sasa umeisha. Waanze kuhesabu masaa mpaka Jumatatu," alisema Raila.

Raila hajafichua mpango wake wa kuhakikisha Jumatatu mambo yanakuwa tofauti na kuwamaliza nguvu polisi.

Maandamano ya Raila yamekuwa yakishinikiza serikali kujiondoa madarakani au iweke wazi tovuti za Tume Huru ya Uchaguzi ili kila mtu kuona matokeo ya uchaguzi uliopita wa Agosti mwaka jana.

Aidha wanataka pia kushushwa kwa gharama za maisha wakisema serikali imefumbia macho changamoto za Wakenya kiuchumi.

Raila ameshikilia kuwa licha ya kuwa na jaribio la kumuangamiza maandamano ya wiki ijayo yataendelea bila vikwazo vyovyote.