Gaza, Israel ni machozi ya furaha

Muktasari:

  • Hisia kali za upendo zilizochanganyika na huzuni zinashuhudiwa miongoni mwa familia za mateka wa vita ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas ambalo mwisho wa wiki hii walianza kubadilishana mateka kwa makubaliano maalumu.

Gaza/ Israel. Hisia kali za upendo zilizochanganyika na huzuni zinashuhudiwa miongoni mwa familia za mateka wa vita ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas ambalo mwisho wa wiki hii walianza kubalishana mateka kwa makubaliano maalumu.

Tovuti ya CNN imeripoti kuwa mateka 41 walioshikiliwa Gaza wameachiliwa huru huku mapatano kati ya Israel na Hamas yakiingia siku ya tatu kati ya nne walizokubaliana ambapo kati yao raia wa Israel ni 13 na wengine ni wa mataifa mengine.

Pia, jana Jumamosi Novemba 25, 2023 jumla ya mateka 39 wa Palestina waliachiwa huru katika jela za Israel.

Wakati mabadilishano ya mateka yakiendelea katika awamu ya pili licha ya kusuasua kutokana na sababu mbalimbali, familia zilizoungana tena na ndugu zao waliokuwa mateka zimekuwa katika furaha iliyopitiliza.

Mtandao wa Daily Mail leo Jumapili Novemba 26, 2023 umeripoti taarifa ya mtoto wa kike wa miaka tisa aliyejulikana kwa jina la Emilly aliyeshiliwa mateka na kundi la Hamas kwa siku 50 ambaye ameungana tena na familia yake kupitia utaratibu wa kubadilishana mateka.

Mtoto huyo, ambaye awali alihofiwa kuuawa na wapiganaji wa kundi la Hamas wakati wa vita hivyo, alirekodiwa akimkimbilia baba yake ambaye alimkumbatia na kumnyanyua juu.

Mtoto huyo alitekwa Oktoba 7, 2023 akiwa amevaa nguo za kulalia, kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa ilimkuta akiwa mateka.

Hali ya furaha iliyopitiliza na kusababisha vilio pia imeshuhudiwa pia upande wa Gaza ambapo mateka walioachiliwa na Israel waliungana na familia zao.

Marah Bakeer (24) binti wa Kipalestina aliyeshikiliwa kama mateka wa vita kati ya nchi hizo mbili aliachiwa huru jana Jumamosi Novemba 26, 2023 na kukutana na mama yake huku vilio vya furaha vikitawala miongoni mwao.

Kabla ya kufungwa kwake, Marah alikuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari Al-Maimouna katika kitongoji cha Sheikh Jarrah.

Aliingia mikononi mwa wanajeshi wa Israel Oktoba 12, 2015, wanajeshi wa Israel walimpiga risasi na kumkamata kwa madai ya kujaribu kumchoma kisu ofisa wa Israel. Bakeer na familia yake walikanusha tuhuma hizo.