Hali mbaya Sri Lanka

Muktasari:

  • Sri Lanka imepandisha bei ya mafuta jana Jumapili, na kusababisha maumivu zaidi kwa wananchi wa kawaida wakati maofisa kutoka Marekani wakiwasili kwa mazungumzo yenye lengo la kupunguza mzozo mbaya wa kiuchumi wa kisiwa hicho.

  

Colombo. Sri Lanka imepandisha bei ya mafuta jana Jumapili, na kusababisha maumivu zaidi kwa wananchi wa kawaida wakati maofisa kutoka Marekani wakiwasili kwa mazungumzo yenye lengo la kupunguza mzozo mbaya wa kiuchumi wa kisiwa hicho.

Shirika la Petroli la Ceylon (CPC) lilisema limepandisha bei ya dizeli, inayotumika sana katika usafiri wa umma kwa asilimia 15 hadi rupia 460 (Sh2,961) kwa lita huku ikipandisha petroli kwa asilimia 22 hadi rupia 550 (Sh3,544).

Tangazo hilo limekuja siku moja baada ya Waziri wa Nishati, Kanchana Wijesekera kusema kutakuwa na ucheleweshaji wa muda usiojulikana wa kupata shehena mpya ya mafuta.

Wijesekera alisema mafuta yaliyotarajiwa wiki iliyopita hayajafika huku shehena iliyopangwa kuwasili wiki ijayo pia hautafika Sri Lanka kutokana na sababu za “kibenki” ambazo wachunguwa mambo wanasema ni kukosa fedha za kigeni.

Wijesekera aliwaomba radhi madereva wa magari na kuwataka kutojiunga na misururu mirefu nje ya vituo vya kuuzia mafuta. Wengi wameacha magari yao kwenye foleni wakitarajia kujaza mafuta yatakapowasili.

Vyanzo rasmi vilisema mafuta yaliyosalia kisiwani humo yanatosha kwa siku mbili tu, lakini mamlaka hiyo inayahifadhi kwa ajili ya huduma muhimu.

Marekani inatathmini mgogoro

Ujumbe kutoka Hazina ya Marekani na Wizara ya Mambo ya Nje walifika kwa mazungumzo “kuchunguza njia bora zaidi za Marekani kusaidia raia wa Sri Lanka wenye uhitaji,” ubalozi wa Marekani huko Colombo ulisema.

“Wananchi wa Sri Lanka wanavyostahimili baadhi ya changamoto kubwa za kiuchumi katika historia yao, juhudi zetu za kuunga mkono ukuaji wa uchumi na kuimarisha taasisi za kidemokrasia hazijawahi kuwa muhimu zaidi kama sasa,” balozi wa Marekani, Julie Chung, alisema katika taarifa yake.

Ubalozi huo ulisema umetoa dola milioni 158.75 katika ufadhili mpya katika wiki mbili zilizopita kuwasaidia raia wa Sri Lanka.

Umoja wa Mataifa tayari umetoa ombi la dharura la kukusanya dola milioni 47 kusaidioa chakula sehemu zilizo hatarini zaidi, zenye watu milioni 22 wa kisiwa hicho.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, takriban wakazi milioni 1.7 wanahitaji “msaada wa kuokoa maisha” huku watu wanne kati ya watano wakipunguza milo yao kutokana na uhaba mkubwa na kupanda kwa bei.

Wiki iliyopita, Serikali ilifunga taasisi na shule zisizo za lazima kwa wiki mbili ili kupunguza safari kwa sababu ya uhaba wa nishati.

Hospitali kadhaa kote nchini ziliripoti kupungua kwa kasi kwa mahudhurio ya wafanyakazi wakiwamo matabibu kutokana na uhaba wa mafuta.

Waziri Mkuu, Ranil Wickremesinghe, Jumatano iliyopita alilionya Bunge kwamba matatizo zaidi yanakaribia.

“Uchumi wetu umekabiliwa na hali ya kuporomoka kabisa,” Wickremesinghe alisema. “Sasa tunakabiliwa na hali mbaya zaidi ya uhaba wa mafuta, gesi, umeme na chakula.”

Nchi hiyo haikuweza kulipa deni lake la nje la dola 51 bilioni. Serikali ilitangaza kuwa haikulipa Aprili na inajadiliana na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya uokoaji unaowezekana.

Wickremesinghe ameonya kuwa taifa hilo lenye watu milioni 22 “linakabiliwa na hali mbaya zaidi.”