Israel, Hamas wakubaliana kusitisha vita kwa siku nne

Dar es Salaam. Nchi za Israel na Palentina zimefikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku nne eneo la Ukanda wa Gaza ambapo pande zote zinatakiwa kutangaza uamuzi huo katika muda wa saa 24 zijazo.

Nchi ya Qatar ambayo ni mpatanishi wa mzozo huo, imesema idadi ya wanawake na watoto wa Kipalestina wanaozuiliwa katika magereza ya Israel wataachiliwa kwa kubadilishana na mateka 50.

Hamas imesema Wapalestina 150 wataachiliwa chini ya makubaliano hayo.

Shirika la Human Rights Watch liliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana Jumatatu Novemba 21,2023 limesema kwamba kulikuwa na takribani Wapalestina 7,000 katika vizuizi vya Israel, wakiwemo wanawake 200 watoto takribani 60.

“Baadhi ya watoto walikamatwa kwa makosa kama kurusha mawe," Mkurugenzi wa Programu wa HRW, Sari Bashi.

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema linaendelea na operesheni yake kutoka angani, ardhini na baharini katika Ukanda wa Gaza kabla ya mapumziko ya siku nne ya mapigano.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Palestina, tangu kuanza vita hiyo, jumla ya watu 14,128 wamefariki wakiwemo watoto zaidi ya 5,840 na wanawake 3,920, na idadi ya waliojeruhiwa imeongezeka hadi 33,000.

Israel na Hamas zimekubaliana kusitisha mapigano kwa siku nne ili kuruhusu misaada ya kibinadamu na mafuta kuingia Gaza.

Kundi la kwanza la mateka linatarajiwa kuachiliwa kesho Alhamisi ikiwa ni makubaliano ya utekelezaji wa kusitishaji mapigano.