Mashirika ya kimataifa yasisitiza kusitishwa mapigano Gaza

Muktasari:

  • Mashirika ya kimataifa pamoja na wadau mbalimbali duniani wameelezea kusikitishwa kwao kutokana na mapigano yanayoendelea ukanda wa Gaza kati ya wanamgambo wa Hamas na jeshi la Israel, huku wakitaka vita hivyo kukoma.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesisitiza kusitishwa vita inayoendelea kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas kwa ajili ya kutolewa misaada ya kibindamu.

Guterres ameyasema hayo kwenye ujumbe wake alioutoa Novemba 19, 2023. "Nasisitiza wito wangu wa kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa ajili ya misaada ya kibinadamu,” amesema Guterres.

Mbali na Guterres pia Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN, Volker Turk amesema inashangaza kuendelea kwa matukio  mabaya huko Gaza.

Turk amesema kuuawa kwa watu wengi katika shule zilizogeuzwa kuwa makazi, ni vitendo vinavyopingana na ulinzi wa msingi ambao raia wanapaswa kupewa chini ya sheria ya kimataifa.

"Wenzetu wa UN walitembelea eneo hilo jana, na kushuhudia moja kwa moja wanachokiita 'eneo la kifo'. Hakuna sehemu salama Gaza,” amesema.

Amesema Wapalestina waliohamishwa na waliokosa msaada wa kuokoa maisha yao kutokana na vizuizi vikali, wanapambana kukidhi mahitaji yao ya msingi, wakilazimika kujificha sehemu zilizojaa watu, uchafu na hatari.

"Sheria za kimataifa za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kanuni tofauti, uwiano na tahadhari wakati wa kufanya mashambulio, lazima zifuatwe kikamilifu. Kutozingatia sheria hizi kunaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.

"Ubinadamu kwanza. Kusitisha mapigano kwa misingi ya kibinadamu na haki za binadamu ni jambo linalohitajika sasa. Watu wangapi watapoteza maisha? Hii lazima ikome" amesisitiza.

Naye, Katibu Mkuu Msaidizi wa masuala ya kibinadamu na msimamizi wa misaada ya dharura (OCHA), Martin Griffiths amesema chanzo cha madhara kwa raia ni  matumizi ya silaha za mlipuko zenye athari kwa watu wengi.

"Chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, pande zote zinapaswa kulinda raia na mali zao. “Kuhakikisha majeruhi na wagonjwa wanapata huduma ya matibabu, hospitali zina kinga maalumu. Hii inamaanisha kuwa hazipaswi kutumiwa kama ngao ya malengo ya kijeshi," amesema.

Wakati Griffiths akiyasema hayo naye mwakilishi maalumu wa UN kwa maeneo ya Palestina, Francesca Albanese amesema kilichotokea katika makazi ya watu Palestina hasa Gaza ni uvunjaji kamili wa kanuni zote za msingi ambazo sheria ya kimataifa inazikubali.

"Nimetoa onyo mara tatu kuhusu hatari kwamba Israel inaweza kuwa inatekeleza uhalifu wa mauaji ya halaiki huko Gaza. kumekuwa na wito wa kusambaratisha Gaza, kuifuta Gaza kwenye uso wa dunia, na kuua watu wake kwa sababu nao 'wanawajibika kwa kile Hamas imefanya' na hakuna tofauti hapa kati ya raia na wapiganaji,”amesema.

Ameongeza kuwa nchi za magharibi, viongozi wa kisiasa na vyombo vya habari wanachezea hatari kwa kutochukua jukumu la kuwajibika kwa kutowasilisha ukweli kama ulivyo, na mara nyingine wanachanganya masuala ya kisheria.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema wagonjwa wengi ni waathirika  wa majeraha ya vita.  Shirika lina wasiwasi juu ya usalama na mahitaji ya afya ya wagonjwa, wafanyakazi wa afya na watu waliokimbia makazi katika hospitali chache zilizobaki zenye uwezo mdogo kaskazini.

Hospitali hizo zinakabiliwa na hatari ya kufungwa kutokana na ukosefu wa mafuta, maji, vifaa vya matibabu, chakula, na mashambulio. WHO inasisitiza ombi lake la kutaka kufanyika jitihada za pamoja kumaliza mapigano na janga la kibinadamu Gaza.

“Tunatoa wito kusitishwa kwa mapigano, mtiririko endelevu wa misaada ya kibinadamu kwa kiwango kikubwa, upatikanaji wa mahitaji ya kibinadamu, kuachiliwa kwa mateka wote bila masharti na kusitisha mashambulizi kwenye huduma za afya na miundombinu mingine muhimu.

Pia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani  (WFP), limesema kuna uwezekano wa raia kukabiliwa na njaa kutokana na usambazaji wa chakula na maji kutokuwepo eneo hilo la Gaza, na kwa uchache mahitaji hayo yanapitishwa kupitia mipakani.

"Hakuna njia ya kumaliza suala la njaa kwani mpaka sasa ni mpaka mmoja tu unaofanya kazi. Matumaini pekee ni kufungua njia nyingine salama kwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu ili kuleta chakula kitakachookoa maisha Gaza"imesema sehemu ya taarifa ya WHO.

Kwa upande wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeeleza wasiwasi wake baada ya kuona picha za kutisha za watoto na raia wanaouawa Ukanda wa Gaza.

“Vurugu lazima ziishe. mateso lazima yaishe. Ndoto za kutisha kwa watoto lazima ziishe sasa. UNICEF na washirika wengine wanasaidiana kusajili watoto 31 waliozaliwa mapema (njiti) ili kusaidia kuwatambua na kuwarudisha pamoja na wazazi wao na wanafamilia inapowezekana,” limesema Shirika hilo.

Nalo, Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) limesema lazima mwisho wa vita hiyo ufike.  

"Mzozo wa kibinadamu Gaza umekuwa ni janga. Bila kusitisha mapigano mara moja, athari hii yenye kuhuzunisha itaendelea kuongezeka, ikiweka maisha mengi ya watu wasio na hatia hatarini. Dunia haitakiwi kujifanya kipofu.”imeeleza sehemu ya taarifa ya shirika hilo.