Wanafunzi 194 Momba wapewa mimba ndani ya mwezi mmoja

Muktasari:
Takwimu hizo zimebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chiwanda wilayani Momba na kuagiza msako mkali ndani ya siku 21.
Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ameagiza kukamatwa ndani ya siku 21 kwa wanaume waliohusika kuwapa mimba wanafunzi 194 wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Momba mkoani Songwe, na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Chongolo amesema mimba hizo zimepatikana ndani ya mwezi mmoja, hata hivyo hakuutaja ni mwezi gani.
“Wilaya ya Momba ina shule za msingi 103 na shule za sekondari 17, cha kushangaza ndani ya mwezi mmoja watoto 194 wamepewa ujauzito, Hii ni hatari kubwa, tunatakiwa tushirikiane kuhakikisha tunatokomeza mimba za utotoni,” amesema Chongolo.
Chongolo amebainisha hayo kwenye ziara yake ya kikazi wilayani humo akikagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Wakati Chongolo akieleza hayo, ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022 inaonyesha mkoa wa Songwe unaoongoza kwa mimba za utotoni ikiwa na asilimia 45.
Mikoa mingine ni Ruvuma (asilimia 37) Katavi (asilimia 34), Mara (asilimia 31) na Rukwa (asilimia 30). Hata hivyo, ripoti hiyo inabainisha kupungua kwa mimba za utotoni kutoka asilimia 27 mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 22 mwaka 2022.
Ongezeko la mimba za utotoni limerekodiwa katika mikoa ya Dar es Salaam ambayo mwaka 2025/2016 ilikuwa kwa asilimia 11.9 ripoti imeonyesha mwaka 2022 kiwango kimefikia asilimia 18.1, Njombe kutoka asilimia 19.7 hadi silimia 25.5 na Ruvuma kutoka asilimia 32 hadi asilimia 37.
Chongolo amesema Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa mitano nchini inayoongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, ubakaji, ulawiti, mimba na ndoa za utotoni, hivyo ni jukumu la wote kuhakikisha wanasimama kidete kupiga vita tabia hizo.
Hivyo, amewaagiza maofisa watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanawafichua wanaume wanaoharibu maisha ya watoto na kutoa taarifa kwenye uongozi wa wilaya ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga alisema wapo katika mikakati ya kuwasaka waliowapa mimba wanafunzi hao na kwamba maagizo ya mkuu wa mkoa ameyapokea na atahakikisha wahusika wanatiwa nguvuni.
“Mimi nina mwezi mmoja na nusu toka niletwe mkoani hapa, nimekuta baadhi ya matukio ya aina hii yametokea, naahidi wahusika wote hawataachwa salama, nawasihi ndugu zangu waacheni watoto wasome, msijiingize kwenye matukio hayo,” amesema Kamanda Senga.
Mkuu wa Wilaya ya Momba, Kenan Kihongosi alimuhakikishia mkuu wa mkoa huo kwamba atatekeleza maagizo aliyompa ndani ya siku 21, na wahusika wote watasakwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili iwe mfano kwa wengine.
Mkazi wa kijiji cha Chiwanda wilayani Momba, Ester Nakawale amesema viongozi wa vijiji wamekuwa wakimaliza kesi za mimba kwa wanafunzi kienyeji na kusababisha kushamiri kwa matukio hayo, kwani hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa wahusika.
Naye Juma Simpasa alisema chanzo cha mimba hizo ni baadhi ya wazazi kutokuwa na nia ya kuwaendeleza watoto wao kimasomo, hivyo ili kukomesha tatizo hili, lazima sheria kwa wahusika iongezwe makali ikiwa ni pamoja na kifungo cha miaka 60 jela, tabia hiyo itakoma.
Mbali ya Momba, inaelezwa pia hali si shwari wilayani Ileje ambayo nayo iko mkoani Songwe ambako wakazi wake wanakiri kuna binti wa kuanzia miaka 20 kama hajaolewa na kuwa na watoto, hufanyiwa tambiko kwa kudhani kuwa wana mkosi ndiyo maana hapati mume wala mimba.
Ndiyo maana ni kawaida kwa binti wa kuanzia miaka 16 kuolewa huku usiri wa wazazi ukitajwa kuwa chanzo kinachokwamisha jitihada za Serikali katika mapambano na mimba za utotoni zinazosababisha mdondoko wa wanafunzi kwa shule za msingi na sekondari.
Josephine Mwashiuya alisema kuwa wazazi ili kuruhusu hilo lifanyike, huwashawishi watoto wao wabebe mimba ili waache shule na baadaye huwaozesha.
“Sasa akifeli shule ni bora aolewe asije kuzalia nyumbani akatupa aibu wazazi wake kuwa hatukuweza kumlea vizuri,” amesema Halison Mwazembe.
Umaskini nao ni moja ya sababu inayofanya mabinti wengi kujikuta katika mimba za utotoni hasa baada ya kuhitimu elimu ya msingi na wazazi kukosa fedha za kuwaendeleza.
“Mimi binti yangu aliolewa lakini ni kwa sababu nilikosa fedha za kumsomesha alipomaliza darasa la saba, alipenda kusoma ila sikuweza,” amesema Mzamillu Mwakyusa.
Kwa mujibu wa utafiti wa Mwananchi, mimba hizi zinachochewa zaidi na wazazi ambao wakati mwingine wanalazimisha watoto wao kujifelisha shule kwa makusudi ili wasiweze kuendelea na masomo na kuolewa.
Hali hiyo huweka ugumu katika ufuatiliaji kwani wanakuwa nje ya mfumo rasmi wa elimu, ambao unaweza kuwabana wazazi ikiwa mtoto hakuonekana shule kwa siku kadhaa.
Na wakati mwingine hali hii inatokea pindi tu mwanafunzi anapomaliza masomo.
Zechen (si jina halisi) ni moja ya mabinti waliomaliza kidato cha nne mwaka jana lakini tayari ana mimba ya takribani miezi saba.
“Nilipata baada ya kumaliza shule, mwenye mimba yuko Tunduma ambapo nilienda nilipohitimu shule, nilipopata ujauzito nilirudi kijijini kwetu Bupigu na mawasiliano yetu na mwenzangu si mazuri,” amesema.
Akiwa anaishi na mama yake kwa sasa ambaye hakuweza kuongea chochote kuhusu mimba ya binti yake, tangu arudi kijijini hapo na hakuwahi hata kumuuliza mimba ni ya nani kutokana na kukasirishwa na suala hilo.
Akilizungumzia hilo, mwanasaikolojia, John Ambrose alisema wasichana wengi walio na umri mdogo wanakuwa katika hatari ya kupata sonona baada ya kujifungua.
“Mara zote wanahisi kelele kama wanaambiwa unatakiwa uwe umesoma, uwe shuleni, una hili, akiwaza majukumu anayotakiwa kufanya kama mama, wengine huwa wanafikia kipindi cha kupiga mtoto kwa sababu wanakuwa na msongo wa mawazo hata wanafikia hatua ya kutupa mtoto chooni,” amesema John.
Amesema wengine hushikwa na wasiwasi kiasi cha kushindwa kuwashika hata watoto wao jambo ambalo linawafanya watu kuanza kuwafundisha taratibu.