Chongolo ashtuka kasi ya mimba za utotoni

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo akizungumza na wananchi wa Kata ya Ndola Juu  kuhusu namna ya kukabiliana na mimba za utotoni. Picha na Denis Sinkonde

Muktasari:

  •  Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amesema Wilaya ya Ileje kimkoa inaongoza kwa mimba za utotoni

Songwe. Kutokana na ongezeko la mimba za utotoni, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ametangaza msako mkali kwa watakaobainika kuhusika.

Chongolo ametangaza msako huo leo Jumanne Aprili 30, 2024 wakati akizungumza na wananchi wilayani Ileje ikiwa ni  mwendelezo wake ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.

Amesema mkoa huo unaongoza kitaifa kwa kuwa na asilimia 45 ya mimba za utotoni huku takwimu zikionesha miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu  watoto 170 wameripotiwa kupata ujauzito.

Chongolo amesema takwimu hizo hazifurahishi hata kidogo na kwa kuwa kapewa dhamana ya kusimamia Songwe, atahakikisha wanashirikiana na timu ya usalama mkoa na wilaya kushughulika na wanaume wote wanaowapa mimba wanafunzi hao.

"Hapa nipo Wilaya ya Ileje ambayo kimkoa inaongoza kwa mimba za utotoni, kamanda wa polisi upo hapa hakikisha wakaidi wanakamatwa, mkuu wa Takukuru upo hakikisha rushwa haifanyiki kwa watakaokamatwa, mkuu wa gereza upo utaletewa sana wanaowapa mimba watoto," amesema Chongolo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Gallus Hyera amewatangazia kiama wanaume wenye tabia za kujihusisha kimapenzi na watoto akieleza kuwa  jeshi hilo litahakikisha linashughilika nao kutokana na tabia ya kukatisha ndoto za wanafunzi.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi amesema wazazi na walezi wanatakiwa kuonyesha ushirikiano kwa vyombo vya dola ili wanaoamatwa kwa kosa la kusababisha mimba wachukuliwe hatua.

"Niwasihi wazazi na walezi muache kumalizana kienyeji kwa kesi za mimba za utotoni, mnakwisha jitihada za Serikali kukomesha vitendo hivyo, mtakaobainika mnamalizana kindugu wote tutawakamata,"amesema Mgomi.

Jenifa Msomba, mkazi wa Kijiji Cha Ibungu amesema ili kutokomesha mimba kwa watoto wadogo sheria ya kuwafunga miaka 30 wanaokutwa na makosa haitoshi iongezwe iwe sambamba na viboko.