Israel kortini tuhuma za mauaji ya Wapestina, yapinga mashtaka, yasema ni lazima ijilinde

Polisi wakiwatawanya waandamanaji nje ya Mahakama ya ICJ mjini The Hague. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Kufuatia vifo vya zaidi ya Wapalestina 24,000 katika mashambulizi yanayofanywa na Israel huko Gaza, Israel imekana mashtaka yaliyowasilishwa na Afrika Kusini kwamba nia yake ni kuua raia na kusema ni lazima ijilinde.

Uholanzi. Israel imekanusha madai yaliyowasilishwa na Afrika Kusini katika Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa kwamba, operesheni yake ya kijeshi huko Gaza ni kampeni ya Serikali ya mauaji kwa raia wa Palestina.

Ikijitetea katika Mahakama hiyo jana Ijumaa Januari 12, 2024, Isarel imesema dhamira yake ni kujilinda, na vifo vya Wapalestina vimetokea wakati ikipambana na Hamas.

Israel imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutupilia mbali kesi hiyo,  na kukataa ombi la Afrika Kusini la kuiamuru kusitisha mashambulizi yake Kaskazini mwa Gaza.

"Haya sio mauaji ya halaiki," Wakili Malcolm Shaw anayeitetea Israel amesema mahakamani hapo.

Afrika Kusini iliiambia Mahakama Alhamisi ya Januari 11, 2024 kwamba mashambulizi ya anga na ardhini ya Israel ambayo yameharibu sehemu kubwa ya eneo hilo na kuua karibu watu 24,000, yana lengo la kuwaua wakazi wa Gaza.

Israel imekataa madai hayo huku ikisema inaheshimu sheria za kimataifa na ina haki ya kujitetea.

Israel ilianzisha vita vyake huko Gaza baada ya mashambulizi ya Hamas ya kuvuka mpaka Oktoba 7, 2023 ambapo watu 1,200 waliuawa na 240 walichukuliwa mateka.

Mshauri wa sheria wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Tal Becker ameiambia Mahakama kuwa mateso kwa Waisraeli na Wapalestina ni matokeo ya mashambulizi ya  Hamas ya Oktoba 7, 2023.

Timu ya ulinzi ya Israel imedai ilikuwa inafanya kila iwezalo kupunguza madhara ya kibinadamu huko Gaza, ikiwa ni pamoja na juhudi za kuwataka Wapalestina kuhama.

Kwa mujibu wa BBC, Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi baadaye mwezi huu, juu ya uwezekano wa hatua za dharura ikiwa ni pamoja na ombi la Afrika Kusini kwamba iamuru Israel kusitisha mashambulizi yake.

Wafuasi wa Palestina wakiwa na bendera walipita mjini The Hague na kutazama matukio ya kilichokuwa kikiendelea mahakamani kwenye runinga kubwa nje ya mahakama. Wajumbe wa Israeli walipozungumza mahakamani, waliimba: "Mwongo! Mwongo!"

Alipoulizwa anafikiria nini kuhusu hoja za Israel kwamba mashambulizi yake huko Gaza ni kujilinda, Neen Haijjawi, Mpalestina anayeishi Uholanzi amesema, "Inawezekanaje Israel kusema inajilinda wakati imekuwa ikiwakandamiza Wapalestina kwa miaka 75. Israel imedai Afrika Kusini ni msemaji wa kundi la Hamas, ambapo Afrika Kusini imekanusha madai hayo.

Tangu majeshi ya Israel yaanze mashambulizi yao, karibu watu wote milioni 2.3 wa Gaza wamefukuzwa kutoka kwenye makazi yao na  wengi kuelekea Gaza Kusini.