Israel yadai sehemu ya Hamas imesambaratishwa, vita vikiingia mwezi wa nne

Picha iliyopigwa Jumamosi Januari 6, 2024 ikionyesha moshi juu ya anga ya mji wa Khan Yunis katika Ukanda wa Gaza Kusini wakati wa mashambulizi ya Israel dhidi ya Kindi la Hamas la Palestina. Picha na AFP

Muktasari:

  • Israel imetamba 'kusambaratisha" uongozi wa kijeshi wa Hamas kaskazini mwa Gaza wakati vita vyake dhidi ya kundi la Palestina vikiingia mwezi wa nne Jumapili leo Januari 7, 2024.

Israel imesema "imesambaratisha" uongozi wa kijeshi wa Hamas kaskazini mwa Gaza wakati vita vyake dhidi ya kundi la Palestina vikiingia mwezi wa nne Jumapili leo Januari 7, 2024.

Wakati ikisema hayo, Shirika la Habari la AFP limesema leo kuwa hofu imeongezeka kwamba mzozo huo unaweza kuenea hadi katika nchi jirani ya Lebanon.

Watu sita wameuawa mapema Jumapili wakati wa uvamizi wa Israel huko Jenin katika Ukingo wa Magharibi, wizara ya afya ya Palestina inayoongozwa na Hamas imesema.

Mashuda wameripoti kuwa Israel pia imefanya mashambulizi ya anga katika mji mkuu wa kusini wa Gaza wa Khan Yunis.


Jeshi la Israel lilisema jana Jumamosi jioni kuwa "limekamilisha kuvunja mfumo wa kijeshi wa Hamas, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza" na vikosi vyake sasa vitalenga maeneo ya kati na kusini mwa eneo hilo.

Huku matarajio ya vita vikubwa yakiibuka, msemaji wa Jeshi la Israel, Daniel Hagari ameonya kwamba kundi la Lebanon linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah, "linaiingiza Lebanon kwenye vita visivyo vya lazima".

Kundi hilo lilirusha makombora zaidi ya 60 katika kambi ya kijeshi ya Israel siku ya Jumamosi kujibu mauaji ya wiki hii huko Beirut, ya naibu kiongozi wa Hamas.

Vita huko Gaza vilichochewa na shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israeli lililoanzishwa na Hamas Oktoba 7, 2023 ambalo lilisababisha vifo vya karibu watu 1,140, ​​wengi wao wakiwa raia, kulingana na hesabu ya AFP na takwimu rasmi za Israeli.

Wanamgambo hao pia walichukua karibu mateka 250, 132 kati yao wakiwa wamesalia mateka, kulingana na Israeli. Takriban 24, wakiwemo Watanzania wawili, wameuawa.

Katika kujibu shambulizi hilo, Israel inafanya mashambulizi ya mabomu na uvamizi wa ardhini, hatua ambayo imeua takriban watu 22,722, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliapa kuwa Israel itaendeleza kampeni yake ya "kuiondoa Hamas, kuwarudisha mateka wetu na kuhakikisha kuwa Gaza haitakuwa tishio tena kwa Israel".