Joe Biden, Trump kazi imeanza

Rais wa Marekani, Joe Biden

Muktasari:

Wakati Donald Trump akilaumiwa kwa kuteua wagombea wasiochagulika, Rais Joe Biden amesema uchaguzi huo ni ushindi kwa demokrasia. Ni uchaguzi ambao Trump (76) alitarajia kupata ushindi kwa kuwa na viti vingi kwenye Baraza la Wawakilishi na Bunge la Seneti na alipanga Novemba 15, 2022 angetangaza kugombea urais mwaka 2024.

Wakati Donald Trump akilaumiwa kwa kuteua wagombea wasiochagulika, Rais Joe Biden amesema uchaguzi huo ni ushindi kwa demokrasia. Ni uchaguzi ambao Trump (76) alitarajia kupata ushindi kwa kuwa na viti vingi kwenye Baraza la Wawakilishi na Bunge la Seneti na alipanga Novemba 15, 2022 angetangaza kugombea urais mwaka 2024.

Hata hivyo, wafuasi ndani ya chama chake cha Republican wamemtaka afikirie upya uamuzi wake huo kwa kuwa wagombea wote aliowateua (Trump) wameshindwa kwenye uchaguzi.

Wakati Trump alitahadharishwa na wafuasi wake, Rais Biden wa Democrats ambaye mwezi huu atatimiza umri wa miaka 80, alisema shabaha yake ni kugombea tena urais mwaka 2024.

Trump, ambaye bado anasisitiza uchaguzi wa Rais wa mwaka 2020 aliibiwa kura, amemuonya Gavana wa Florida, Ron DeSantis asijaribu kuanza kampeni za kutaka kugombea urais.

Japokuwa baadhi ya wafuasi ndani ya Republican wanamuona DeSantis (44) anaweza kugombea urais, Trump aliendelea kusisitiza kama (DeSantis) atagombea urais atakivuruga chama hicho.

“Sijui kama atagombea. Nafikiri kama atagombea atajiumiza vibaya sana. Sijui kama itakuwa vizuri kwa chama,” alisema Trump.

Uchaguzi huu matarajio ya Trump na Republican ilikuwa ni kushika udhibiti wa mabunge yote mawili ya Wawakilishi na Seneti.

Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa Trump ambaye ni Rais wa 45 wa Marekani wamemlaumu kwa kusababisha chama kushindwa kwenye ngome zake muhimu, wakimponda kuwa ni mbinafsi aliyejali masilahi yake na amekiingizia chama gharama kwa wagombea wasiochagulika.

Ilitolewa mfano wa mgombea wa Seneti katika Jimbo la Pennsylvania, Dk Mehmet Oz ambaye ameshindwa na mgombea wa Democrats kwenye uchaguzi huo, kwamba hakuwa na mvuto.

Hata hivyo, Trump amemlaumu mkewe, Melania kwa kumshawishi kumpigia debe mgombea asiyeuzika. Republican ilitumia hoja ya uchumi mbaya na ongezeko la mfumuko wa bei kama kete yao ya ushindi kwenye uchaguzi huo.

Hata hivyo, chama hicho kinaelezwa kuadhibiwa kwa kampeni yake ya kupinga kurejeshwa ruhusa ya utoaji mimba.

Rais Biden kwenye kampeni zake akifahamu atavutia wapiga kura aliahidi kuruhusu tena utoaji mimba, kitu ambacho mahakama ya juu ya Marekani ilikizuia na kurudisha maamuzi yawe yanafanywa na Serikali za majimbo.

Majimbo mengi, hasa yanayoongozwa na Republican walitumia fursa hiyo kuzuia utoaji mimba.


Kuelewana na Republican

Rais Biden ameahidi kufanya kazi na Republican kutokana na chama hicho kuwa na viti vingi kwenye Baraza la Wawakilishi.

“Niko tayari kuelewana na Republican kwenye hoja ambazo zitaleta mantiki kwa Taifa. Nafikiri Wamarekani wanatutaka tusonge mbele na kuwatumikia wao,” alisema Rais Biden.

Alisema kuna maeneo ambayo hawawezi kuelewana kama kupiga marufuku utoaji mimba. Kuhusu uchumi, Rais Biden alipingana na wanaosema uchumi wa Marekani unaelekea kuporomoka.

“Hatuko kwenye hatari ya kuporomoka kwa uchumi wetu. Nafikiri tuko kwenye kile wachumi wanaita kutua salama,” alisema huku akiongeza kuwa Serikali yake inakwenda kupambana na suala la mfumuko wa bei.


Mtoto wa Rais Biden

Imeelezwa kama Republican watashika udhibiti wa Baraza la Wawakilishi wataanzisha uchunguzi dhidi ya mtoto wa Biden, Hunter kwa tuhuma mbalimbali za jinai. Wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais mwaka 2020, Trump kwenye kampeni zake alimshambulia Biden akiita familia yake kuwa ‘kundi la wahalifu.’

Hunter Biden ambaye ni mtoto pekee wa Biden, amekuwa akichunguzwa juu ya uwezekano wa kukiuka sheria za kulipa ushuru na utakatishaji wa fedha tangu mwaka 2018.

Pia, anachunguzwa iwapo hakuripoti mapato yake yote, na iwapo alilaghai matumizi yake ya mihadarati wakati aliponunua bunduki ya mkononi mitaani.

Trump na washirika wake walidai Hunter kwenye mikataba yake ya biashara, hususan katika nchi za China na Ukraine, inaonyesha kuwepo kwa ufisadi, ikiwamo utumiaji wa mihadarati.

Hata hivyo, wakati Trump akipambana kudhibiti Baraza la Wawakilishi, Kamati ya Bunge nayo imepanga kumhoji kuhusu vurugu za wafuasi wake waliovamia Bunge wakipinga ushindi wa Biden. Kamati hiyo ilikuwa ikichunguza vurugu zilizotokea Januari 6, 2021 baada ya wafuasi wa Trump kuvamia Bunge wakijaribu kuzuia wabunge kutambua ushindi wa Biden.

Trump ametakiwa kufika mbele ya kamati hiyo kwa mahojiano ifikapo Novemba 14, mwaka huu.


Uchaguzi wa katikati ya muhula

Novemba 8, mwaka huu Marekani ilifanya uchaguzi wa katikati ya muhula kuchagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Seneti na Magavana. Uchaguzi huu hufanyika katikati ya kipindi cha miaka minne ya urais. Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Marekani utafanyika 2024. Vyama vinavyoshindana zaidi kwenye uchaguzi ni Democrats cha Biden na Republicans cha Trump.

Uchaguzi huu ndio hutoa mwelekeo chama gani kinaweza kushinda nafasi ya urais huku Democrats na Republicans vikiendelea kukabana koo.

Ni uchaguzi unaoelezwa kuwa tangu Vita vya Pili vya Dunia, chama kilicho nje ya madaraka kimeweza kushinda wastani wa viti 28 katika Baraza la Wawakilishi na wastani wa viti viwili kwenye Seneti.

Matokeo yaliyokuwa yametoka hadi Novemba 9, mwaka huu kwenye Baraza la Wawakilishi, Democrats ilikuwa imepata viti 183 na Republicans viti 207. Ili chama kidhibiti bunge hilo kinahitaji kupata viti 218.

Kwenye Bunge la Seneti, Democrats wana viti 48 na Republicans viti 49, ili kudhibiti bunge hilo chama kinatakiwa kuwa na viti 51.

Kwa upande magavana, Democrats ina viti 22 na Republicans viti 24, bado viti sita havijapigiwa kura.