Kashkashi alizopitia mpinzani wa Rais Putin, utata wa kifo chake

Miaka minne iliyopita Alexei Navalny aliulizwa nini angewaambia raia wa Russia,  ikiwa atauawa kwa kumpinga Rais Vladimir Putin.

Alijibu: "Hauruhusiwi kukata tamaa... Ikiwa wataamua kuniua, maana yake ni kwamba tuna nguvu sana na tunahitaji kutumia nguvu hizo."

Magereza nchini Russia Jumamosi iliyopita, Machi 16, mwaka huu, ilitangaza kuwa Navalny alikufa gerezani huko Arctic ambako alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 19 kwa tuhuma za kuwa na itikadi kali dhidi ya Serikali ya Rais Vladmir Putin. Kifo chake kilizua masuto duniani kote kwamba aliuawa.

Kulingana na shirika la habari la Associated Press (AP) la nchini Marekani, wapinzani wengi wa Putin ni wamekufa, wamekimbilia uhamishoni nje ya nchi na wengine wamefungwa katika magereza ya Russia.

Lakini Alexei Navalny ni nani? Kwa nini  auawe? Yeye alikuwa kiongozi wa upinzani nchini Russia, wakili, mwanaharakati wa kupinga ufisadi na mfungwa wa kisiasa.

Alipanga maandamano dhidi ya serikali ya Putin na kugombea kiti cha rais ili kutetea mageuzi dhidi ya ufisadi nchini humo na dhidi ya Rais Putin na Serikali yake.

Navalny ni mwanzilishi wa Taasisi ya Kupambana na Ufisadi (FBK). Alitambuliwa na shirika la haki za binadamu la Amnesty International kama mfungwa wa kisiasa, na alitunukiwa Tuzo ya Sakharov kwa kazi yake juu ya haki za binadamu.

Tuzo ya Sakharov ni ya heshima kwa watu binafsi au vikundi vilivyojitolea maisha yao katika kutetea haki za binadamu na uhuru wa mawazo.

Agosti 20, 2020, kiongozi huyo wa upinzani na mwanaharakati wa kupinga ufisadi aliwekewa sumu aina ya Novichok akiwa kwenye ndege kutoka Tomsk kwenda Moscow.

Aliugua na akapelekwa hospitalini huko Omsk baada ya ndege kutua kwa dharura, na kisha alilazwa hospitalini akiwa amepoteza fahamu.

Siku mbili baadaye, watu wake walifanikiwa kumtorosha na kumpeleka katika hospitali ya Charite katika Jiji la Berlin, Ujerumani. Sumu hiyo ilithibitishwa na maabara tano zilizoidhinishwa za Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) la nchini Ujerumani.

Septemba 7 ya mwaka huo, madaktari walitangaza kwamba walipunguza sumu mwilini na Navalny kuanza kupata fahamu, kwa mujibu wa BBC Septemba 7, 2020.

Septemba 22, 2020 aliruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya hali yake kuimarika. OPCW ilisema sumu hiyo aina ya Novichok iligundulika katika damu, mkojo, sampuli za ngozi na chupa yake ya maji.

Wakati huo huo, ripoti ya OPCW ilifafanua kuwa Navalny aliwekewa sumu ya aina mpya ya Novichok, ambayo haikujumuishwa katika orodha ya kemikali zinazodhibitiwa za Mkataba wa Silaha za Kemikali.

Navalny alimshutumu Rais Putin kuhusika kumwekea sumu, lakini Serikali ilisema tuhuma hizo "hazina msingi kabisa" na kwamba ni "matusi" kwa Serikali, pia ikamtuhumu Navalny kuwa alikuwa akilifanyia kazi Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).


Kutokana na tukio hilo, Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Uingereza ziliweka vikwazo kwa Mkurugenzi wa Shirika la Kijasusi la Russia (FSB) Alexander Bortnikov, maofisa wengine wakuu watano wa Russia na Taasisi ya Utafiti ya Jimbo la Kemia na Teknolojia ya Kikaboni (GosNIIOKhT).

Kwa mujibu wa EU, Navalny angeweza tu kulishwa sumu "kwa idhini ya Ofisi ya Rais" na kwa kushirikiana na FSB.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa maisha ya Navalny kutiwa majaribuni. Aprili 27, 2017, alishambuliwa na wasiojulikana nje ya ofisi yake katika taasisi yake ya kupambana na ufisadi ambao, walimwagia usoni kimiminika cha rangi ya kijani kibichi, ambayo inawezekana kilikuwa kimechanganywa na vitu vingine.

Hilo lilikuja kujulikana kama 'shambulio la Zelyonka' ambalo alidai kuwa jicho lake la kulia lilipoteza asilimia 80 ya uoni wake.

Baadaye alidai kuwa shambulio liliongozwa na mtu aliyeitwa Aleksandr Petrunko, ambaye Navalny alidai alikuwa na uhusiano na naibu spika wa bunge la nchi hiyo, Pyotr Olegovich Tolstoy. Pia limtuhumu Pyotr kuwa alifadhiliwa na Putin.

Tukio lingine lilitokea Julai 2019, wakati Navalny alipokamatwa na kufungwa. Julai 28 alilazwa hospitalini akiwa na majeraha makubwa kwenye macho na ngozi yake. Huko hospitalini, aligunduliwa na athari ya mzio, ingawa utambuzi huu ulipingwa na Anastasia Vasilyeva, mmoja wa madaktari wake wa binafsi.

Julai 29, 2019, Navalny alitolewa hospitalini na kurudishwa gerezani, licha ya daktari wake kupinga.

Agosti 2020, ikiwa ni siku chache kabla ya kuwekewa sumu, Navalny alikuwa akichapisha video kwenye chaneli yake ya YouTube iliyoonyesha kuunga mkono maandamano ya demokrasia ya 2020 ya Belarusi, ambayo yalichochewa na uchaguzi wa rais wa Belarus wa 2020 uliokuwa na ushindani mkubwa.

Navalny pia aliandika kwamba aina ya 'mapinduzi' yaliyokuwa yakifanyika katika nchi jirani ya Belarus pia yangefanyika Russia siku za karibuni.

Baada ya kuzinduka hospitalini Septemba 7, 2020, hospitali ya Charite alikokuwa amelazwa nchini Ujerumani iliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwaambia:

"Hali ya Alexei Navalny... imeimarika. Mgonjwa amepata fahamu na ameondolewa kwenye mashine za kumsaidia kupumua. Lakini, bado ni mapema sana kupima athari za muda mrefu za sumu yake kali."

Septemba 10, vyombo vya habari viliripoti kuwa ulinzi wa polisi nje ya hospitali ya Charite ulikuwa umeimarishwa, na kwamba Navalny amepata fahamu na anaweza kuzungumza tena.

Siku tatu baadaye, Septemba 14, Hospitali ya Charite ikasema afya ya Navalny imeimarika kiasi kwamba anaweza kuondoka hospitalini, na siku moja baadaye ikajulikana kuwa alikuwa na mpango wa kurejea Russia.

Akiwa anapata ahueni baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali ya Charite, Navalny alisema: "Ninasisitiza kwamba (Rais) Putin ndiye aliyehusika na uhalifu huu, na sina maelezo mengine ya kile kilichotokea. Ni watu watatu pekee wanaoweza kutoa amri ya kuchukua hatua hii na kutumia (sumu ya) Novichok..."


Januari 2021, Navalny alirudi Russia, lakini alipofika tu alikamatwa na kuwekwa kizuizini kwa madai kuwa alikiuka masharti ya parole alipokuwa amelazwa hospitalini nchini Ujerumani.

Kufuatia kukamatwa kwake, maandamano makubwa yalifanyika kote Russia. Baadaye alidaiwa kuwa ana itikadi kali za kisiasa.

Machi 2022, Navalny alihukumiwa kifungo cha ziada cha miaka tisa gerezani baada ya kupatikana na hatia ya ubadhirifu na kudharau mahakama. Alikata rufaa lakini ikatupiliwa mbali.

Alihamishiwa kwenye gereza lenye ulinzi mkali. Agosti 2023, Navalny alihukumiwa kifungo cha ziada cha miaka 19 kwa mashtaka ya kuhusika na itikadi kali.

Desemba 2023, Navalny alitoweka gerezani kwa karibu wiki tatu. Baadaye ikajulikana anashikiliwa kwenye gereza jingine.

Februari 16, mwaka huu, maofisa wa magereza nchini Russia waliripoti kuwa Navalny amefariki akiwa na umri wa miaka 47.

Kifo chake kilizua maandamano nchini Russia na katika nchi nyingine mbalimbali. Shutuma dhidi ya Serikali ya Putin juu ya kifo chake zimetolewa na serikali nyingi za Magharibi na mashirika ya kimataifa.

Siku mbili baada ya kifo chake kuripotiwa, Rais Putin alitaja hadharani jina la Alexei Navalny kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi mbele ya waandishi wa habari, akisema:

“Kuhusu Navalny. Ndiyo, aliaga dunia. Hili ni tukio la kusikitisha kila wakati... Baadhi ya wenzetu siku kadhaa kabla ya kufa kwake walikuwa wamependekeza kubadilishana Navalny na baadhi ya watu ambao, wako gerezani katika nchi za Magharibi. Nilikubali wazo hilo, alimradi tu kiongozi wa upinzani hakurudi tena Russia, lakini, kwa bahati mbaya kilichotokea kilifanyika. Inatokea. Unaweza kufanya nini? Hayo ndiyo maisha.”