Kichwa cha mwanajeshi wa Israel chauzwa Sh25 milioni

Muktasari:

  • Mwanajeshi wa Israel Adir Tahar (19) aliuawa na wapiganaji wa Hamas Oktoba 7, 2023 na wauaji kukata kichwa chake na kukinadi kwa Dola za Marekani 10,000 (Sh25 milioni).

Tel Aviv.  Baba wa mwanajeshi wa Jeshi la Israel (IDF) aliyekatwa kichwa na wanamgambo wa Hamas, amesema kichwa cha mwanaye kimetangazwa kuuzwa zaidi ya Sh25 milioni.

 Kituo cha televisheni cha CNN cha Marekani kilionyesha video ya mauaji ya askari wa IDF na kukatwa vichwa na taarifa yake pia ilichapishwa kwenye gazeti la The Times of Israel.

David Tahar, ambaye mtoto wake wa kiume Adir Tahar (19) aliuawa Oktoba 7, 2023 kwenye mapigano kati ya Hamas na Israel, aliliambia gazeti la ‘The Times of Israel’ kuhusu kupatikana kichwa cha mwanaye aliyemzika bila kichwa.

Amesema wanamgambo wa Hamas waliokamatwa na wanajeshi wa IDF, walifichua na kuwezesha kupatikana kwa kichwa cha Adir kilichopotea kutoka Gaza. CNN ilionyesha video tofauti ya kukata kichwa mwanajeshi huyo.

Tahar amesema mgambo kutoka Ukanda wa Gaza alimkata kichwa mwanaye aliyeuawa katika mapigano ya Oktoba 7, 2023 na baadaye alijaribu kuuza kichwa chake kwa dola 10,000.

“Kwa muujiza kichwa kilipatikana na kurudishwa Israel  kwa mazishi,” amesema Tahar.

Amesema mwanaye Adir, aliyepangiwa jukumu kwenye kituo kilicho jirani na mpaka wa Gaza, aliuawa na wanajeshi wenzake wa kikosi chake cha Golani Brigade walipokuwa wakipigana na wanamgambo wa Hamas Oktoba 7, 2023 ambao walisababisha vifo vya watu zaidi ya 1,200.

Tahar amesema mwanaye alikuwa mvulana mwerevu, mwenye kipaji na mnyenyekevu.

“Mnamo Oktoba 7, magaidi wapatao 3,000 wanaoongozwa na Hamas walipovamia kusini mwa Israel kutoka Ukanda wa Gaza, Adir alikuwa miongoni mwa kundi la wanajeshi 18 wa IDF waliokuwa wakikabiliana nao,” amesema Tahar.

Amesema Adir aliuawa kwa mashambulizi ya guruneti yaliyorushwa kwake na walimkata kichwa.

“Mwili wa Adir ulitambuliwa kutokana na vitambulisho vyake, upimaji wa DNA, na vitu vya kibinafsi katika mifuko yake,” amesema.

Amesema mabaki ya mwili wa Adir yalipelekwa Israel na kuzikwa kwenye makaburi ya kijeshi ya Mlima Herzl huko Jerusalem.

Tahar amesema alitaka kuona mwili wa mwanaye ingawa maofisa wa IDF walimuonya kuwa itakuwa bora ikiwa hatatazama mwili huo.

Amesema nusu saa kabla ya mazishi, wakati yeye na mpwa wake walikuwa peke yao na jeneza, alifungua ili kumwangalia mtoto wake.

“Nilielewa vizuri kile nilichokuwa nikizika. Nilijua nilikuwa nikizika mvulana bila sehemu muhimu," amesema Tahar.

Tahar amesema kwa muda wa miezi miwili alijaribu kila awezalo kujua kichwa cha mwanaye kilikuwa wapi.

"Haikuwa rahisi, haikuwa rahisi," amesema huku akikumbuka kutazama video kadhaa za mauaji ya Hamas ambayo yalitumwa kwenye mitandao ya kijamii.

Amesema alipata video iliyoonyesha mwili wa mwanaye bila kichwa chake na Desemba mwaka jana "muujiza" ulifanyika kwa kichwa kupatikana.

Amesema wapiganaji wawili wa Hamas walikamatwa na vikosi vya Israeli na kuhojiwa na idara ya usalama ya Shin Bet, ambapo walifichua kwamba mmoja wao alijaribu kuuza kichwa cha askari wa IDF kwa dola 10,000 na alitoa maelezo sehemu kilipokuwa kichwa hicho.

Amesema kichwa cha mwanaye kilirudishwa Israel na vipimo vya DNA na meno vilionyesha kuwa kilikuwa kichwa cha Adir na baadaye kilizikwa.

Tahar amesema kutokana na kifo hicho familia yake imeamua kumuenzi mtoto wao kwa kuanzisha kituo cha usaidizi cha ujirani kwa vijana walio katika hatari ya kutoweka.

Amesema video fupi zilizorushwa na CNN ndio zilimuonyesha mwanamgambo wa Hamas akiwa na msumeno kwenye shingo za Waisraeli waliokufa wakikatwa vichwa.

Tahar alisema mtangazaji wa CNN, Jake Tapper alionyesha klipu hiyo katika kipindi chake cha "The Lead."

"Ushahidi wa kukatwa vichwa, unaoimarisha mtazamo wa Israel kwamba Hamas ni sawa na makundi ya jihadi kama al-Qaeda na Islamic State (ISIS)."

Wakati wa shambulio lililoongozwa na Hamas, magaidi walivamia jumuiya na vituo vya kijeshi, na kuwachinja wale waliowakuta.

Familia nzima iliuawa walipokuwa wamekusanyika pamoja katika nyumba zao. Wanawake walibakwa na genge kisha kuuawa.

Shahidi mmoja alieleza gazeti la Sunday Times akimwona mwanamke akijitetea dhidi ya magaidi waliokuwa wakijaribu kumbaka kwenye tamasha la muziki la nje ambapo watu 360 waliuawa.

Magaidi hao pia waliwateka zaidi ya watu 240 ambao walichukuliwa mateka hadi Gaza.

Katika kujibu mashambulizi hayo, Israel ilianzisha kampeni ya kijeshi ya kuiangamiza Hamas, kuiondoa madarakani, na kuwakomboa mateka ambapo mpaka sasa inakadiriwa watu wasiopungua 24, wameuwawa Gaza wengi wao ni watoto na wanawake.

Israel imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba ukatili unaofanywa na Hamas unaonyesha kuwa ni kundi la kigaidi lililo sawa na Islamic State na lazima litokomezwe.


(Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mashirika)