Kimbunga ‘Daniel’ chaua 200 Libya

Muktasari:
- Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Libya limetangaza kutokea kwa vifo vya watu 200 baada ya kimbunga ‘Daniel’ kuikumba nchi hiyo.
Libya. Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Libya limetangaza kutokea kwa vifo vya watu 200 baada ya kimbunga ‘Daniel’ kuikumba nchi hiyo.
Hata hivyo, mashirika mbalimbali ya tathmini yanadai huenda vifo vilivyotokea vikafika zaidi ya 2,000.
Kimbunga na dhoruba hiyo kilianza siku ya Jumapili, na kusababisha mamlaka kutangaza hali ya hatari iliyokithiri.
Wanajeshi saba wa jeshi la Libya wametoweka wakati wa juhudi za uokoaji zinazoendelea. Maafisa mashariki mwa Libya wameweka amri ya kutotoka nje, huku shule na maduka yakiamriwa kufungwa.
Miji ya iliyoathiriwa zaidi na kimbunga hiko ni pamoja na; mashariki ya Benghazi, Sousse, Derna na Al-Marj.
Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya vifo, Shirika la Msalaba Mwekundu la Libya lilitoa taarifa na kusema kuwa takriban nyumba 150 zimeharibiwa.
Mkuu wa mtandao wa misaada ya kibinadamu wa ‘Red Crescent’ amesema takriban vifo 150 vimetokea Derna pekee, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Video ambazo hazijathibitishwa za dhoruba hiyo zimekuwa zikisambazwa mtandaoni, ikiwa ni pamoja na klipu inayoonyesha mafuriko yakisomba mtu. Picha zingine zinaonyesha madereva wakiwa wamekwama kwenye juu ya magari yao.