Kimbunga chaua watu 23 Marekani

Muktasari:

  • Kimbunga kimeua watu 23 nchini Marekani baada ya kulikumba Jimbo la Mississippi na kusababisha uharifu mkubwa huku wengine wakihofiwa kufunikwa kwenye vifusi.

Mississippi. Takriban watu 23 wamefariki dunia baada ya kimbunga kukumba Jimbo la Mississippi nchini Marekani usiku wa kuamkia leo Jumamosi Machi 25, 2023.

Watu wengine wanadhaniwa wamenaswa chini ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa na kimbunga hicho.

Kimbunga hicho kilisababisha uharibifu katika miji kadhaa ya mashambani, ambapo miti na nyaya za umeme zilikatwa na kusababisha kukatika kwa umeme katika maeneo mengi.

Majimbo mengine kadhaa ya kusini pia yanakabiliwa na dhoruba kali.

Mvua ya mawe iliripotiwa katika maeneo kadhaa ya jimbo hilo.

Wakazi wa Rolling Fork, mji mdogo ulioko magharibi mwa Mississippi, walisema kuwa kimbunga kilipeperusha madirisha ya nyumba zao ambapo uharibifu katika eneo hilo unaripotiwa kuwa mbaya.

Cornel Knight ameliambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba yeye, mke wake na binti yao mwenye umri wa miaka mitatu walikuwa katika nyumba ya jamaa yao huko Rolling Fork na kwamba hali ilikuwa ya kutisha kutokana na kimbunga hicho.


Amesema kimbunga hicho kilipiga nyumba ya jamaa mwingine, ambapo ukuta ulianguka na kuwanasa watu kadhaa ndani.

Mtabiri mmoja wa hali ya hewa wa eneo hilo, akiwa na wasiwasi kutokana na nguvu za kimbunga karibu kupiga mji wa Amery, alisimamisha kwa muda utabiri wake wa televisheni ili kuwaombea wakazi wa mji huo.

Gavana wa Mississippi, Tate Reeves, amesema kwenye Twitter kwamba timu za utafutaji na uokoaji zilikuwa zikitoa msaada wa matibabu kwa wale walioathiriwa.