Rais Samia akipigia debe Kiswahili Comoro, aahidi msaada wa walimu, vifaa

Muktasari:
- Rais Samia apigia chapuo lugha ya Kiswahili ifundishwe shuleni na itambulike rasmi nchini Comoro.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Kiswahili ndicho lugha pekee ya Kiafrika inayoweza kuunganisha watu wa bara zima katika nyanja za mawasiliano, elimu na biashara.
Ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja kabla ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika Julai 7, 2025.
Pia, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, imeelezwa kuna zaidi ya watu milioni 200 wanaozungumza lugha ya Kiswahili duniani kwa sasa na idadi inatarajiwa kuongezeka kutokana na namna kinavyotangazwa kimataifa.
Amesema hayo leo Julai 6, 2025, wakati akihutubia kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Taifa la Comoro zilizofanyika katika Uwanja wa Malouzini Omnisport mjini Moroni.

“Rais Samia ni miongoni mwa wakuu wa nchi na Serikali waliohudhuria sherehe za taifa hilo lililopata uhuru wake kutoka katika kwa ukoloni wa Ufaransa.
"Eneo letu la Kusini mwa Afrika kumegawanywa kuendana na lugha za watawala wa kikoloni. Wapo wanaoongea Kiingereza, Kifaransa na Kireno. Lugha pekee ya Kiafrika inayoweza kuwaunganisha watu wetu ni Kiswahili.
"Ili kujenga umoja nipendekeze kwamba Kiswahili kiwe lugha ya mawasiliano, elimu na biashara kati yetu ifundishwe shuleni na kutambulika rasmi hapa Comoro. Tanzania iko tayari kusaidia kutoa walimu na vifaa vya kufundishia," amesema.
Amesema lugha hiyo ni daraja la pamoja la maendeleo kati ya nchi hizo na ni urithi wa pamoja, hivyo nchi hizo zitaendeleza urafiki uliodumu kwa muda mrefu sasa.
Uhusiano na Comoro
Rais Samia amesema Tanzania itaendelea kudumisha na kutunza uhusiano kati yake na Taifa la Comoro katika nyanja za kiuchumi, kidiplomasia, kijamii na kiutamaduni.
Amesema muingiliano wa mataifa hayo mawili ulianza zamani na una historia ndefu, ukijengeka katika misingi ya moyo wa ujamaa, lugha ya Kiswahili, diplomasia ya amani na imani ya pamoja, huku akieleza kuwa kwa sasa inakadiriwa kuwa kuna Wacomoro wapatao 10,000 wanaoishi Tanzania.

"Wapo Watanzania wengi kule Unguja, Dar es Salaam, Tanga na Moshi ambao asili yao ni Comoro na wapo Wacomoro ambao Tanzania ni nyumbani kwao. Dar es Salaam tuna msikiti wa Wangazija na makaburi ya Wangazija pia. Hii inaonyesha watu wa Comoro wamejikita Tanzania muda mrefu," amesema Rais Samia.
Tangu Comoro ipate uhuru mwaka 1975, nchi hizo zimeendelea kudumisha uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliojengwa juu ya misingi ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi na kijamii, huku Tanzania ikiendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya Taifa hilo.
Sekta ya afya
Katika sekta ya afya, amesema ushirikiano umekua na kuimarika na Wacomoro 12,000 walipata huduma za afya nchini Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2024/25.
Amesema mwaka jana 2024, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ilihudumia zaidi ya watu 2,700 kutoka visiwa vya Ngazija na mwaka huu inatarajiwa kufanyika kambi ya tiba nchini humo.
Kwa upande wa changamoto, Rais Samia amesema mabadiliko ya tabianchi yanakabili nchi zote, ikiwemo kuongezeka kwa maji ya chumvi na nyuzijoto.
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Comoro kulinda ikolojia yetu kwa faida ya sasa na baadaye.
Ameeleza zaidi kuwa Tanzania na Comoro ni ndugu wa damu na washirika wa karibu, wenye mila na tamaduni zinazoshabihiana, ambao wanatenganishwa tu na Bahari ya Hindi
Ikumbukwe, Tanzania na Comoro zilitia saini hati nne za makubaliano kwenye kilele cha mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya mataifa hayo uliofanyika Julai 24, 2024 jijini Dar es Salaam.

Hati zilizosainiwa katika kikao hicho zilijumuisha nyanja za ushirikiano wa kidiplomasia, biashara na viwanda, afya na teknolojia ya habari. Rais Samia amesema baada ya makubaliano hayo biashara imeongezeka kati ya mataifa hayo.
Utiaji saini hati hizo ulishuhudiwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia nchi za Kiarabu, nchi zinazozungumza Kifaransa, diaspora na utangamano wa Afrika, Mohamed Mbae.
Aidha, katika sherehe hizo, kikosi cha wanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kimekuwa moja ya washiriki wa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa nchi hiyo.
Lugha ya Kiswahili
Wakati Rais Samia akizungumzia umuhimu wa lugha ya Kiswahili kuliunganisha Bara la Afrika, Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) liliteua Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani na maadhimisho yalianza mwaka uliofuata.
Pia, Umoja wa Afrika (AU) uliidhinisha Kiswahili kuwa lugha yake rasmi ya kikazi ndani ya umoja huo zikiwamo za Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa na Kireno.
Lugha ya Kiswahili pia ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Takwimu mbalimbali zinaonyesha wazungumzaji wa Kiswahili wamesambaa katika nchi zaidi ya 14 zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Visiwa vya Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Msumbiji, Malawi, Sudan Kusini, Somalia, Zambia, Oman na Yemen katika Mashariki ya Kati.
Pia, baadhi ya mataifa ya kusini mwa Afrika, kama vile Afrika Kusini na Botswana, yameiingiza shuleni, huku Namibia ikifikiria kufanya hivyo. Chuo Kikuu cha Addis Ababa cha Ethiopia hivi karibuni kilitangaza kwamba kitaanza kufundisha Kiswahili.
Historia ya Kiswahili
Wazo la Kiswahili kuwa lugha ya Kiafrika lilianzishwa miaka ya 1960 na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliyetumia lugha hiyo kuunganisha taifa lake baada ya uhuru.
Mwalimu Nyerere alichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa Kiswahili, akitambua kuwa Watanganyika walihitaji lugha hiyo kwa ajili ya biashara na kuelewana, lakini pia kwa dhana ya Uafrika na aliiona kama aina ya ukombozi kwa nchi ambazo hazijapata uhuru.
Hayo yalithibitishwa pia na mwandishi wa vitabu wa Nigeria, Wole Soyinka, ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya 1986, aliposisitiza matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kuvuka bara.