Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama ilivyomaliza sakata la kuzikwa Edgar Lungu

Muktasari:

  • Mvutano wa muda mrefu wa kisheria uliodumu kwa takribani mwaka mmoja na uliosababisha msuguano wa kisiasa kati ya Serikali ya Zambia na familia ya marehemu Edgar Lungu hatimaye umemalizika kwa familia kupewa haki.

Mahakama ya Rufaa ya Afrika Kusini imeamua kwa upande wa familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu, katika kesi ya mgogoro wa maziko yake, ikisema familia ndiyo yenye mamlaka ya mwisho kuhusu mahali atakapozikwa.

Uamuzi huo unabatilisha uamuzi wa awali uliokuwa umeitaka Serikali ya Zambia kuusafirisha mwili wa kiongozi huyo na kumzika kwa heshima za kitaifa nchini Zambia, katika makaburi maalum ya viongozi wa taifa hilo.

Lungu alifariki dunia akiwa Afrika Kusini Juni 5, 2025 alipokuwa akipatiwa matibabu, na tangu wakati huo mwili wake umekuwa ukizuiliwa kutokana na mvutano kati ya familia yake na Serikali ya Zambia kuhusu taratibu za maziko.

Serikali ya Zambia ilikuwa ikisisitiza mwili wake urejeshwe nchini humo kwa maziko ya kitaifa, ikisema viongozi wa zamani wa taifa wanapaswa kuzikwa kwa heshima kamili za serikali. Hata hivyo, familia yake ilipinga mpango huo, ikitaka azikwe kwa faragha nchini Afrika Kusini, kwa madai ya kuheshimu matakwa yake binafsi.

Katika uamuzi wake uliotolewa leo Jumanne, Juni 23, 2026, mahakama hiyo imesema kuwa haki za familia katika kupanga maziko zinapaswa kupewa uzito zaidi katika mazingira ya kesi hiyo, hivyo kuipa familia nafasi ya kuamua hatima ya mwili huo.

Uamuzi huo unamaliza mvutano wa muda mrefu wa kisheria uliodumu kwa takribani mwaka mmoja na uliosababisha msuguano wa kisiasa kati ya Serikali ya Zambia na familia ya marehemu, huku pia ukigusa mjadala mpana kuhusu mamlaka ya serikali dhidi ya haki za familia katika maziko ya viongozi wa kitaifa.

Lungu aliongoza Zambia kwa kipindi cha takribani miaka sita, kuanzia mwaka 2015 hadi 2021. Alingia madarakani Januari 2015 baada ya kifo cha Rais Michael Sata, akishinda uchaguzi mdogo kwa ushindani mkali dhidi ya mpinzani wake mkuu Hakainde Hichilema.

Baadaye alichaguliwa tena mwaka 2016 kwa muhula kamili wa miaka mitano, ambapo aliendelea kuiongoza nchi hadi aliposhindwa katika uchaguzi wa 2021.